CIDAT YAIPONGEZA TPA KWA KUPUNGUZA TOZO

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bandari Kavu Tanzania (CIDAT), Bw. Meleck Shange, amepongeza uamuzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wa kupunguza ada ya Uendelezaji wa Miundombinu Mipya ya Bandari (PID) kutoka asilimia 9 hadi asilimia 4.5 ya kodi ya forodha.

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Shange ameeleza kuwa hatua hii ni faraja kubwa kwa wadau na itasaidia kutekeleza mpango kabambe wa uwekezaji wa Shilingi trilioni 16.1 kwa kutumia mapato ya ndani badala ya kutegemea mikopo.

“Na katika kusikiliza kilio cha walio wengi wameweza kutoka 9% mpaka 4.5% jambo mbalo kwa kweli ni la faraja sana kwa wananchi na natumaini kwamba hata sasa hivi inapoenda kutumika basi wadau wote watakuwa tayari wako radhi kuipokea”, ameeleza Shange.

Amesema tozo hii ya 4.5% itatumika kuboresha bandari kuu zote za kimkakati ambazo ni Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, pamoja na maandalizi ya ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo.

Aidha, ameeleza kuwa umuhimu wa tozo hii ni kuwezesha ujenzi wa magati mapya ya ziada ili kuzuia meli kusubiri nje ya bandari hatua itakayoshusha bei ya bidhaa masokoni. Aidha amebainisha kuwa upanuzi wa magati utaleta mnyororo chanya wa kiuchumi kwani utavuta shehena kubwa ya mizigo, mizigo hiyo ikiongezeka, Bandari Kavu (ICDs) zitapata kazi nyingi zaidi, jambo litakalolazimisha kuongezwa kwa watendaji na hivyo kuzalisha ajira mpya kwa vijana wa Kitanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here