
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linachunguza tukio la walinzi wa kimasai kudaiwa kumshambulia kwa kumkata na kitu chenye ncha kali mguuni pamoja na kichwani raia wa China hadi kusababisha kifo chache.
Taarifa zinaeleza kuwa raia huyo wa china alietambulika kwa jina la Bhaozang Ge (50), mmiliki wa kiwanda cha kuchakata chupa kiitwacho XIL LI, ameonekana akiwa na majeraha makubwa kichwani na mguuni jambo linalodhaniwa kusababisha kifo chake, na kwamba baada ya hapo walinzi hao walitokemea kusikojulikana wakiwa na begi lenye fedha tasmili Sh. milioni 10.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi marehemu Bhaozang Ge alishambuliwa na walinzi binafsi wa kiwanda chake Mei 16, 2026 saa 8:00 usiku katika eneo la Mabibo Ubungo Jijini Dar es Salaam.
“Upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili watuhumiwa wachukuliwe hatua kali zaidi za kisheria,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Mdogo wa marehemu Denis Jery, amesema alieuawa ni ndugu yake ambae wametoka tumbo moja, na kwamba tukio hilo limewasikitisha na kusababisha hofu miongoni mwao huku akisisitiza kuwa usalama wa maisha kwa kila mtu ni kitu muhimu kuliko kitu chochote.
“Napenda kuiomba serikali na Jeshi la Polisi kuhakikisha usalama wa maisha unazingatiwa,” amesema.
Meneja wa kiwanda hicho Lucas Shayo, amesema tukio hilo limewaumiza sana kutokana na kwamba shughuli zitasimama na nyuma yao kuna watu wengi wanawategemea ikiwemo familia kwakuwa ndiyo sehemu wanayoitegemea kuingiza kipato, huku akiiomba serikali kuliangalia suala hilo kwa jicho la tatu.







