Saturday, 22 August 2026

HIKI NDICHO KILICHOMFANYA SAMATTA KUSTAAFU TAIFA STARS: SAFARI YA SHUJAA ALIYEIBEBEA TANZANIA MIAKA 15

Mbwana Ally Samatta, jina lililoacha alama kubwa katika historia ya soka la Tanzania, ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, baada ya miaka 15 ya huduma. Ni safari ya mchezaji aliyeamini kipaji chake, akafanya miguu yake kuwa chanzo cha maisha na kuandika historia ambayo imekuwa funzo kwa vijana wengi wanaoota kufikia […]
Licha ya kwamba alianzia African Lyon, ni katika klabu ya Simba Sports ambako nyota yake ilianza kung’aa na milango ya kuondoka Tanzania kufunguka ambapo alielekea TP Mazembe ya DR Congo

Mbwana Ally Samatta, jina lililoacha alama kubwa katika historia ya soka la Tanzania, ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, baada ya miaka 15 ya huduma.

Ni safari ya mchezaji aliyeamini kipaji chake, akafanya miguu yake kuwa chanzo cha maisha na kuandika historia ambayo imekuwa funzo kwa vijana wengi wanaoota kufikia mafanikio katika soka.

Tangu akiwa mtoto, Samatta aliamini kuwa mpira wa miguu unaweza kuwa njia ya kubadilisha maisha yake. Inasimuliwa kuwa aliwahi kumwambia marehemu baba yake, Ally Samatta:

“Baba ninunulie viatu, nataka kuwa mchezaji mkubwa katika Taifa hili la Tanzania.”

Kauli hiyo ndogo ndiyo iliyokuwa mwanzo wa safari kubwa ambayo baadaye ilimfikisha kwenye viwanja vya kimataifa, akicheza katika baadhi ya ligi kubwa duniani.

Mwanzo wa safari: Kutoka Mbagala hadi Simba SC

Mbwana Ally Samatta alizaliwa tarehe 23 Desemba 1992 jijini Dar es Salaam, Tanzania. Tangu akiwa mdogo alionyesha kipaji kikubwa cha soka, jambo lililomfanya kuanza safari yake ya kitaaluma kupitia klabu mbalimbali nchini.

Samatta alianza kujijenga katika soka kupitia klabu ya Mbagala Market, iliyokuwa ikihusishwa na wafanyabiashara wa Soko la Mbagala Zakhiem (sasa eneo hilo likifahamika zaidi kama Mbagala Rangi Tatu).

Baadaye alipata nafasi ya kujiunga na African Lyon, klabu iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu Tanzania wakati huo, ambako kipaji chake kilianza kuonekana wazi.

Uwezo wake wa kufunga mabao, kasi na kujituma uwanjani ulimfanya kuvutia macho ya klabu kubwa nchini.

Hatua iliyofuata ilikuwa kujiunga na Simba SC, moja ya klabu kubwa Tanzania, ambako alianza kupata uzoefu mkubwa wa soka la ushindani.

Akiwa Simba, Samatta alionyesha ubora wake kama mshambuliaji mwenye nguvu, kasi na uwezo mkubwa wa kumalizia nafasi, jambo lililomfanya kuanza kuonekana kama kipaji maalum katika soka la Tanzania.

Mchezo dhidi ya TP Mazembe uliobadili historia yake

Kutoka Simba Sports Club, Samatta alielekea TP Mazembe ambako alikipiga kwa mafanikio makubwa na kuna tetesi kwamba aliwahi kuhitajiwa na Arsenal ya Uingereza, lakini tajiri wa Mazembe, Moise Katumbi akamuongeza dau ili aendelee kukipiga Mazembe

Samatta hakudumu muda mrefu Simba kabla ya kuvutia klabu kubwa barani Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2011, Simba ilikutana na TP Mazembe katika hatua za mashindano hayo.

Tarehe 20 Machi 2011, Simba ikiwa ugenini nchini Congo ilipoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Mazembe, lakini Samatta aliendelea kuonyesha kiwango kikubwa licha ya matokeo hayo.

Katika mchezo wa marudiano uliochezwa Dar es Salaam tarehe 3 Aprili 2011, Samatta aliendelea kuthibitisha uwezo wake baada ya kufunga bao lililoisaidia Simba kusawazisha mchezo huo kuwa 2-2, kabla ya Mazembe kupata bao jingine.

Kiwango hicho kilimfanya TP Mazembe kuvutiwa naye na hatimaye mwaka 2011 akajiunga rasmi na klabu hiyo.

TP Mazembe: Mahali alipoandika historia Afrika

Akiwa TP Mazembe, Samatta alibadilika na kuwa mmoja wa washambuliaji bora barani Afrika.

Alikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya klabu hiyo, akisaidia kutwaa mataji mbalimbali na kuifanya Mazembe kuwa moja ya timu hatari Afrika.

Mwaka 2015 ulikuwa mwaka wa kihistoria kwake baada ya kuisaidia TP Mazembe kushinda Ligi ya Mabingwa Afrika, huku akimaliza akiwa mfungaji bora wa mashindano hayo.

Kutokana na kiwango chake bora, Samatta alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani ya Afrika (CAF African Player of the Year – Based in Africa) mwaka 2015.

Alikuwa Mtanzania wa kwanza kupata heshima hiyo, jambo lililoongeza jina lake katika ramani ya soka la dunia.

Safari ya Ulaya: Kutoka Ubelgiji hadi England

Inawezekana hakutua Arsenal (kama tetesi zinavyoeleza), lakini Mbwana alifanikiwa kukipiga kwenye Ligi maarufu duniani ya Uingereza baada ya kusajiliwa na Aston Villa mwaka 2020

Baada ya mafanikio yake Afrika, Samatta alihamia Ulaya mwaka 2016 kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji.

Akiwa Genk aliendelea kuonyesha uwezo wake na kuwa mmoja wa washambuliaji waliokuwa wakiheshimika katika ligi hiyo.

Msimu wa 2018/2019 ulikuwa wa kipekee kwake baada ya kusaidia Genk kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, huku yeye akiwa mmoja wa wachezaji muhimu katika mafanikio hayo.

Mwaka 2020, Samatta aliandika historia nyingine baada ya kusajiliwa na Aston Villa ya England, na kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligi Kuu ya England.

Pia aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga bao katika ligi hiyo, baada ya kufunga dhidi ya Bournemouth.

Baada ya Aston Villa, aliendelea na safari yake Ulaya kupitia klabu mbalimbali ikiwemo Fenerbahçe ya Uturuki, Royal Antwerp ya Ubelgiji, kurejea tena KRC Genk, kabla ya kujiunga na PAOK Salonika ya Ugiriki na sasa anakipiga katika ligi ya Ufaransa klabu ya Le Havre AC ya Ligue 1.

Miaka 15 ya kuvaa jezi ya Taifa Stars

Samatta alianza kuitumikia Taifa Stars mwaka 2011 na kwa miaka mingi alikuwa mhimili muhimu wa timu hiyo.

Katika kipindi chake cha miaka 15, amecheza zaidi ya mechi 100 za kimataifa na kufunga zaidi ya mabao 20 akiwa na Taifa Stars.

Mbali na kuwa mfungaji, Samatta alipewa jukumu la kuwa nahodha wa timu hiyo kwa takribani miaka 10, akiwaongoza wachezaji wenzake katika kipindi muhimu cha soka la Tanzania.

Moja ya kumbukumbu kubwa zaidi akiwa Taifa Stars ni kuwa sehemu ya kikosi kilichoiwezesha Tanzania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019, baada ya taifa hilo kusubiri kwa miaka 39 kushiriki tena michuano hiyo.

Siku ya kuaga Taifa Stars

Mafanikio yake yalimfanya kuwa nahodha wa Taifa Stars kwa miaka kadhaa na licha ya kwamba huenda Tanzania haikuwahi kunyakua mataji makubwa kwenye ulimwengu wa soka, hakuna ambaye anaweza kutilia shaka ari na moyo wake wa upiganaji pale alipokuwa kwenye jezi ya Timu yake ya Taifa

Tarehe 7 Julai 2026, Mbwana Ally Samatta alitangaza rasmi kustaafu kuitumikia timu ya Taifa ya Tanzania.

Kupitia ujumbe wake, Samatta aliwashukuru viongozi wa TFF, makocha, wachezaji wenzake, wadau wa soka na Watanzania kwa kumuunga mkono katika safari yake yote.

Alisema mafanikio na kumbukumbu alizopata akiwa Taifa Stars zitaendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha yake, huku akiahidi kuendelea kuiunga mkono timu hiyo kama shabiki, mdau wa soka na raia wa Tanzania.

Urithi wa Popaa

Kwa miaka mingi, Samatta amekuwa zaidi ya mchezaji wa soka. Amekuwa ishara ya matumaini kwa vijana wengi wa Tanzania wanaotamani kufika mbali katika mchezo huo.

Kutoka Mbagala, Simba SC, TP Mazembe hadi kwenye viwanja vya Ulaya, safari yake imekuwa ushahidi kuwa kipaji, nidhamu na kujituma vinaweza kumfikisha mtu mbali.

Jina la Mbwana Ally Samatta “Popaa” litaendelea kubaki katika historia ya soka la Tanzania kama mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea.

Si tu kwamba amecheza mpira, bali ameacha urithi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *