Meya wa Jiji la Arusha, Mhe. Maxmillian Iranqhe, amefanya kikao kazi kilichowakutanisha Maafisa Afya kutoka kata zote 25, wakandarasi wa huduma ya uzoaji taka pamoja na mawakala wa ukamataji wa wachafuzi wa mazingira, kwa lengo la kuimarisha usafi wa jiji hilo wakati wote, hususan kuelekea michuano ya AFCON 2027. Kikao hicho kimefanyika leo, Aprili 1, 2026.




Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Iranqhe alieleza kuwa Jiji la Arusha lina hadhi ya kipekee kwa kuwa makao makuu ya taasisi mbalimbali za kimataifa, zikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu pamoja, Shirika la Posta Afrika (PAPU) na taasisi zingine mbalimbali.
Amesisitiza kuwa hadhi hiyo inalazimu jiji kuwa na mazingira safi, salama na yanayovutia wakati wote.
Aidha, amebainisha kuwa Arusha ni mwenyeji wa mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa, jambo linaloongeza umuhimu wa kudumisha viwango vya juu vya usafi wa mazingira ili kulinda taswira ya jiji na kuwavutia wageni.
Mhe. Iranqhe alisisitiza kuwa ukusanyaji wa taka unapaswa kufanyika kwa wakati na kwa ufanisi ili kuhakikisha maeneo yote ya jiji yanabaki safi.
Ameongeza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la pamoja, akihimiza ushirikiano madhubuti kati ya maafisa afya, wakandarasi wa uzoaji taka, mawakala wa ukamataji pamoja na timu ya uongozi wa jiji ili kufikia matokeo chanya na endelevu.
Katika kuimarisha utekelezaji wa sheria, aliwaelekeza mawakala wa ukamataji kuhakikisha wanachukua hatua stahiki dhidi ya wachafuzi wa mazingira kwa kuwatoza faini ya shilingi 50,000, sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa kuzingatia sheria na taratibu, bila kutumia nguvu zisizo za lazima.
Akifafanua msisitizo wa utekelezaji, Mstahiki Meya alitumia kauli mbiu ya “tembeza kichapo” kumaanisha utekelezaji madhubuti wa sheria kupitia utozaji wa faini kwa wote watakaobainika kuchafua mazingira, ili kudhibiti na kuondoa vitendo hivyo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kutokana na hadhi ya Jiji la Arusha kama kitovu cha utalii nchini, ni muhimu jiji hilo kuwa kinara wa usafi wa mazingira, na hivyo kuwa mfano wa kuigwa kitaifa na kimataifa.
o



