Google search engine

WAHARIRI, WAANDISHI WAJIPANGA KUMWANIKA JAJI MUTUNGI

Share

*Wasema watafichua pesa alizokuwa akipokea kuendesha Gazeti la LAJIJI

RIPOTA PANORAMA

SAKATA la Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kudaiwa Shilingi milioni 10.1 na wahariri na waandishi wa habari waliokuwa wakifanya kazi kwenye Gazeti la LAJIJI analolimiki, lipo mbioni kufichua mambo mazito.

Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki iliyopita na mmoja wa wahariri wanaomdai Jaji Mutungi, Eckland Mwaffisi alipozungumza na Tanzania PANORAMA Blog iliyomuuliza hatua waliyofikia kuhusu kudai stahili zao.

Alisema hakuna mrejesho wowote waliopata kutoka kwa Jaji Mutungi hivyo wanajipanga kueleza yote wanayoyajua kuhusu Jaji Mutungi na gazeti lake la LAJIJI.

Mwaffisi alisema, wataipigania haki yao bila woga kwa kutoa ushahidi mzito mahakamani ambao utaeleza pesa alizokuwa akipokea Jaji Mutungi kuendesha Gazeti la LAJIJI zilikuwa zikitoka wapi, maelekezo aliyokuwa akiwapa wahariri na lengo la kuanzishwa gazeti hilo.

Kwa mujibu wa barua ya Wakili Komba, fedha ambazo wahariri na waandishi wa habari wanamdai Jaji Mutungi ni malimbikizo ya mishahara yao ya kuanzia mwaka 2020/2021.

Disemba 2, 2022, Wakili Komba kupitia Kampuni ya Uwakili ya Haki Kwanza Advocates, alimuandikia Jaji Mutungi barua yenye Kumb. Na. HKA/JIJI/ ECHO/MSHAHARA, 2020 akimtaka awe amewalipa wateja wake ndani ya siku 14, kabla ya Disemba 15, 2022.

Barua hiyo inasema, Jaji Mutungi amekataa kulilipa deni hilo bila sababu zozote za msingi wa kisheria akitambua kuwa anavunja sheria za ajira na nchi kwa makusudi wakati yeye ni mwanasheria wa hadhi ya Jaji.

Pia barua inasema, Jaji Mutungi ni kiongozi ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenye kiapo cha viongozi wakuu wa taasisi za umma, uaminifu kwa Katiba ya nchi, utii, maadili ya uongozi wa umma.

“Iwapo hutalipa fedha yote kwa mkupuo ndani ya muda tuliokupatia, tumeagizwa na wateja wetu tukuchukulie hatua za kisheria hususan kukushtaki mahakamani kwa kesi ya madai ambayo utalipa fedha nyingi zaidi.

“Fedha hiyo itajumuisha riba ya kimahakama, usumbufu uliowafanyia wateja wangu kiasi cha wao wenyewe na familia zao kukosa mahitaji muhimu, gharama za kesi na nafuu nyingine ambazo mahakama itaona inafaa,” ilisema sehemu ya barua hiyo kwenda kwa Jaji Mutungi.

Awali akizungumzia deni hilo, Mwaffisi alisema wamelidai muda mrefu kwa kumkumbusha Jaji Mutungi lakini amekuwa akitoa ahadi za kulilipa bila kuitimiza.

Alisema Jaji Mutungi alikuwa akidaiwa na kiwanda kilichokuwa kikichapa magazeti yake, deni hilo amelilipa lakini hataki kulipa deni analodaiwa na wahariri na waandishi wa habari.

“Mimi binafsi niliacha kazi Gazeti la LAJIJI Septemba, 2021 baada ya Jaji Mutungi kushindwa kunilipa mshahara wangu kuanzia Novemba, 2020. Ilipofika Novemba, 2021 alipunguza deni la Novemba-Disemba, 2020 kwa wafanyakazi wote baada ya baadhi ya wafanyakazi kulalamikia malimbikizo ya mshahara wao kwenye Mtandao wa Jamii Forum,” alisema.

Mwaffisi alisema baada ya Jaji Mutungi kupunguza deni hilo, aliendelea kumkumbusha ili aweze kumalizia pesa wanazomdai kupitia simu yake ya mkononi (WhatsApp).

“Awali Jaji Mutungi alikuwa akionyesha ushirikiano kwa kutoa ahadi ya kulipa deni letu lakini baadaye aliamua kukaa kimya kila nilipomkumbusha, ” alisema.

Kutokana na usumbufu huo, Mwafffisi alisema Februari 10, 2022 aliuandikia barua uongozi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Waziri na Katibu Mkuu) ili waingilie kati jambo hilo, waweze kulipwa malimbikizo yao.

Alisema uongozi wa wizara uliahidi kufuatilia na ilipofika Juni 4, 2022 wizara ilisema malalamiko hayo ni madai hivyo ilishauri yafikishwe mahakamani ili wafanyakazi waweze kupata stahiki zao.

“Ndio maana kupitia mwanasheria wetu, amemuandikia barua Jaji Mutungi na kumpa siku 14 awe ametulipa pesa zetu, asipotulipa tutakwenda mbele zaidi,” alisema.

Alisema wakati wakiendelea kudai malimbikizo ya mshahara wao, Jaji Mutungi aliendelea kuchapa Gazeti la LAJIJI zaidi ya miezi mitatu mfululizo bila kujali deni alilokuwa akidaiwa na wafanyakazi.

Gharama za uchapaji zilikuwa sh. 1,050,000 kwa kopi 3,000 mbali na gharama za usafirishaji gazeti mikoani.

Read more

Local News