DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe na msingi la mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kusambaza mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Matanki hayo yanajengwa eneo la Kigamboni na wakandarasi wabia kutoka China ambao ni Kampuni ya China Railway Major Bridge Engineering Group (CRMBEG) na Kampuni ya Wuhuan Engineering kwa gharama ya Shilingi bilioni 678.6.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Samia amesema mradi huo ni hatua ya kimkakati wa kuiimarisha Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji kikanda na kimataifa.
Rais Samia ameitaka Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vya kimataifa ili kukidhi hitaji la ushindani wa soko la dunia.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kusambaza mafuta. Hafla hiyo imefanyika leo Kigambani, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kabla ya Rais Samia, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema mradi huo utaongeza uwezo wa bandari kuhudumia meli za mafuta na utaifanya Tanzania iaminike na wadau wa sekta ya usafirishaji wa ndani na kimataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) , Plasduce Mbossa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kusambaza mafuta leo, Jijini Dar eas Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Plasduce Mbossa amesema watanzania wameshuhudia jitihada za wazi za Rais Samia kuendeleza na kuimarisha uwezo wa tija za Bandari ya Dar es Salaam.
Mbossa amesema ujenzi wa matanki hayo sasa umefikia asilimia 41 na utakapokamilika utaongeza ufanisi na kupunguza muda wa meli kusubiri kutoka siku 22 hasi siku saba tu.

Wananchi na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) waliofika kushuhudia uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kusambaza mafuta, iliyofanyika Kigamboni, Jijini Dar es Salaam.




