MAKALA YA MTANGAZAJI
KAMA kuna jambo linaloonesha maendeleo kwa macho na kuguswa moja kwa moja na maisha ya wananchi, basi ni pale unaposhuhudia majengo mapya yakisimama mjini na vijijini, nyumba mpya zikichomoza mitaa mipya na hospitali, shule na maghala yakijengwa kwa kasi isiyoacha maswali.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah
Ndiyo maana leo, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limekuja na ripoti inayotikisa, ripoti inayoonyesha namna sarafu inavyobadilika kuwa matofali, ndoto inavyobadilika kuwa jengo na kaulimbiu ya shirika ya “Tunajenga Taifa Letu” inavyogeuka kuwa uhalisia unaoonekana kila kona ya nchi.
Hii si hadithi ya karatasi wala makabrasha ya ofisini. Hii ni hadithi ya miradi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 185 inayoendelea kutikisa anga za Tanzania; kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kutoka Mtwara hadi Mara na kutoka Lindi hadi Tanga. Hii ndiyo Tanzania mpya inayojengwa kwa mikono ya NHC hatua kwa hatua, jengo kwa jengo na nyumba kwa nyumba.
Utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi, biashara na majengo ya serikali na biashara unaofanywa na NHC umelifanya shirika hilo kuendelea kuwa injini ya maendeleo ya ujenzi nchini, likijipambanua si kama taasisi ya kawaida bali kama mshirika mkubwa wa serikali na wananchi katika kujenga taifa lenye matumaini na ustawi wa kweli.
Na aidha, ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020/2025. Katika ilani ya CCM, ukurasa wa 121 inaainisha miradi iliyofanywa na NHC katika kipindi cha 2015/2020 na ukurasa wa 122 inaelekeza Serikali; pamoja na mambo mengine, kupitia NHC kuendelea kuboresha sekta ya nyumba na makazi kwa kuchukua hatua 13.

Rais Samia Suluhu Hassan. Serikali yake imetekeleza kwa ufanisi mkubwa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu ujenzi wa nyumba za makazi, biashara na majengo ya ofisi za serikali.
Ilani ya CCM inazitaja hatua hizo kuwa ni kuandaa sera mpya ya nyumba na maendeleo ya makazi na kubuni mikakati mbalimbali ya kuwawezesha wananchi mijini na vijijini kujenga nyumba bora na za gharama nafuu kwa kushirikiana na wadau wote.
Kushirikiana na mamlaka za upangaji kuandaa mfumo wa kisasa wa usimamizi wa uendelezaji wa miji ikiwemo upatikanaji na utoaji vibali vya ujenzi wa nyumba.
Kuhakikisha maeneo yaliyopimwa kwa ajili ya makazi na biashara yanawekewa miundombinu ya kisasa ikiwemo barabara, maji, umeme na mawasiliano.
Kutambua na kuanzisha kanzidata ya nyumba zote nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha taratibu za mahusiano kati ya wapangaji na wamiliki wa nyumba na majengo.
Kukamilisha taratibu za kuanzisha chombo cha usimamizi na uendelezaji wa sekta ya milki ambacho pamoja na majukumu mengine, kiratibu kodi za pango la nyumba za makazi na biashara, ufanyaji biashara zihusuzo ardhi na milki, uuzaji wake na ulipaji kodi, usajili wa madalali na uwekaji kumbukumbu zote za milki za makazi na biashara.
Kuandaa mwongozo wa mipango na ujenzi wa nyumba vijijini.
Kuwezesha upatikanaji wa ardhi kwa gharama nafuu kwa ajili ya ujenzi kwa kushirikiana na wadau wote wakiwemo Shirika la Nyumba la Taifa na Wakala wa Majengo pamoja na sekta binafsi.
Kuhamasisha na kuweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanakuwa na nyumba bora, “nyumba bora kwa kila Mtanzania inawezekana.”
Kuendelea kuboresha na kuimarisha Shirika la Nyumba la Taifa ili litekeleze miradi kwa tija na kujenga nyumba, majengo ya Serikali na majengo ya biashara kwa gharama nafuu katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo;
Kuendelea na ujenzi wa nyumba 1,000 za gharama nafuu jijini Dodoma kwa ajili ya kuuza na kupangisha kwa wananchi na watumishi wa Serikali.

Morocco Square
Kukamilisha ujenzi wa nyumba na majengo makubwa ikiwemo Morocco Square, Kawe 711, Golden Premier Residence na mradi wa kiwanja namba 300 Regent Estate katika Jiji la Dar es Salaam.
Kuendelea na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 149 katika eneo la Iyumbu na nyumba 100 katika eneo la Chamwino jijini Dodoma.
Kuendelea na miradi ya vitovu vya miji katika maeneo ambayo yanamilikiwa ya Luguruni (ekari 156.53) Uvumba, Kigamboni (ekari 202) na Kawe (ekari 267.71) katika Jiji la Dar es Salaam na Burka/ Matevesi (ekari 579.2) eneo la Usa River (ekari 296) jijini Arusha na;
Kukamilisha mipango kabambe ya Kawe, Luguruni na Kunduchi Rifle Range iliyopo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya nyumba zilizojengwa na NHC katika mradi wa ujenzi wa Nyumba 68 jijini Dodoma.
Ripoti ya NHC ya Mwezi huu imeweka wazi mafanikio makubwa yaliyopatikana, changamoto zilizopo na mikakati ya kuzitatua. Ripoti hiyo imebeba takwimu na picha halisi za miradi, lakini zaidi ya takwimu ni ushahidi wa namna Shirika linavyotekeleza kwa vitendo ahadi yake ya “Tunajenga Taifa Letu” sambamba na maelezo ya Ilani ya CCM kwa NHC.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zaidi ya shilingi bilioni 185 zilizotajwa hapo juu zimeshaelekezwa kwenye miradi mbalimbali, huku zaidi ya shilingi bilioni 65 zikiwa zimetumika tayari kufikia hatua zilizopigwa hadi sasa.
MIRADI INAYOENDELEA: UFANISI UNAOHESABIKA KWA MACHO
Miradi inayoendelea ni ushahidi wa namna NHC inavyoleta matokeo chanya kila siku. Samia Housing Scheme – Kawe jijini Dar es Salaam imekamilika kwa asilimia 98 na sasa ipo kwenye maandalizi ya kukabidhiwa kwa wananchi, hatua ambayo italeta makazi ya kisasa kwa mamia ya familia.

Mwonekano wa majengo ya Samia Housing Scheme.

Vilevile, nyumba 68 Iyumbu Dodoma, maduka ya Zongomela Kahama, pamoja na majengo ya biashara Masasi na Mtanda (Lindi), yamefikia kati ya asilimia 75 hadi 98. Hii inamaanisha kwamba miradi hii ipo kwenye hatua za mwisho na itakuwa tayari kutumika katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka wa fedha 2025/26.
Akifafanua kuhusu kasi hii, Meneja Habari na Mawasiliano wa NHC, Muungano Saguya alisema: “Hii ni ishara kwamba kazi zetu hazibaki kwenye makaratasi, bali zinaonekana kwa macho ya wananchi. Tuliahidi kuongeza kasi ya utekelezaji na leo tunaona miradi mikubwa ikiwa karibu kumalizika kwa viwango vya kuridhisha.”
MIRADI YA MAKAZI: SULUHU YA PENGO LA NYUMBA
Moja ya changamoto kubwa nchini ni pengo la makazi bora, hususan katika miji mikubwa inayokua kwa kasi. NHC imeendelea kutafuta suluhu ya changamoto hiyo kwa kuanzisha miradi mipya mikubwa ya makazi. Samia Housing Scheme – Kijichi Estate jijini Dar es Salaam na Medeli Phase III mjini Dodoma tayari vimeanza hatua za awali za uchimbaji na ujenzi.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Muungano Saguya.
Ingawa utekelezaji wake uko katika asilimia chache kwa sasa, miradi hii ni uthibitisho wa dhamira ya NHC ya kupunguza pengo la makazi na kuongeza nyumba za kisasa zinazoweza kufikiwa na Watanzania wa kipato cha kati na cha juu.
Saguya alisisitiza umuhimu wa miradi hii kwa kusema: “Tanzania ina upungufu mkubwa wa nyumba, lakini kupitia miradi hii tunaendelea kulipunguza pengo hilo hatua kwa hatua. Lengo letu ni kuleta makazi ya kisasa, salama na yenye hadhi ambayo kila Mtanzania anaweza kujivunia.”
MIRADI YA SERIKALI: DODOMA YABADILIKA KWA KASI
Katika Jiji la Dodoma, NHC inafanya kazi kubwa kuhakikisha makao makuu ya nchi yanapata hadhi stahiki kupitia ujenzi wa majengo ya serikali.

Baadhi ya nyumba za makazi zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoani Dodoma.
Kupitia miradi ya Mtumba Government City, majengo ya wizara mbalimbali yamefikia zaidi ya asilimia 96 ya utekelezaji. Hii siyo tu ni alama ya maendeleo bali ni sehemu ya kutengeneza mazingira bora ya kazi kwa maelfu ya watumishi wa umma na kuboresha sura ya mji mkuu wa nchi.
MIRADI ILIYOKAMILIKA: ALAMA YA MATUNDA
Ripoti ya Agosti pia imeonesha miradi kadhaa mikubwa iliyokamilika. Hii ni pamoja na upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Muhimbili, ujenzi wa machinjio ya kisasa Vingunguti Ilala, maghala ya Masasi Mtwara na hospitali za rufaa za Kanda Kusini (Mtwara) na Kanda ya Ziwa (Mara).

Jengo la Masasi Commercial Complex linalojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)

Kila moja ya miradi hii inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja, iwe ni kwa kutoa huduma za afya za uhakika, nafasi za biashara au usalama wa chakula.
Saguya alibainisha: “Kila jengo tunalojenga, iwe ni hospitali, shule au ghorofa la biashara ni mchango wa moja kwa moja kwa taifa. Ni ahadi yetu kwamba ubora hautakuwa jambo la kujadiliana bali ni kigezo cha lazima.”
UFANISI NA MIKAKATI
Ingawa kuna changamoto za ucheleweshaji wa malipo kutoka kwa baadhi ya wateja wa miradi ya nje, NHC imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha changamoto hizo hazikwamishi kasi ya utekelezaji. Shirika limeimarisha ufuatiliaji wa miradi, kuhimiza uwajibikaji wa wakandarasi na kuweka msisitizo kwenye kukamilisha miradi kwa wakati, ndani ya bajeti na kwa ubora unaokubalika.
Kwa maneno ya Saguya: “Tunajua matarajio ya Watanzania kwa NHC ni makubwa na tunayaheshimu. Ndiyo maana kaulimbiu yetu ya ‘Tunajenga Taifa Letu’ si maneno ya kufurahisha masikio, bali ni mwongozo wa kila hatua tunayochukua.”
HITIMISHO
Hadithi ya NHC ni hadithi ya matumaini, ni utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, si hadithi ya takwimu pekee. Ni hadithi ya Watanzania wanaopata nyumba bora, wafanyabiashara wanaopata maeneo ya kufanyia kazi, wagonjwa wanaopata huduma za afya katika majengo mapya na watoto wanaojifunza katika shule zenye miundombinu mizuri. Kila jengo jipya linaloinuka linaashiria siyo tu mafanikio ya Shirika, bali pia ni alama ya mustakabali wa taifa.
Kwa mtazamo huo, ripoti ya Agosti 2025 ya NHC si karatasi tu yenye takwimu, bali ni kioo kinachoonyesha njia ya Tanzania kuelekea kwenye taifa lenye makazi bora, miundombinu imara na wananchi wenye matumaini mapya.



