RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
WANANDOA Simon Lema na Oliva Simon Lema waliotengana baada ya kuishi pamoja kwa miaka 35 sasa wanapambana. Wapo katika mapambano ya kuwania mali walizochuma wakiwa pamoja kwenye maisha yao ya ndoa.
Simon na Oliva walitenganishwa na Mahakama ya Mwanzo Kawe ambayo katika hukumu yake iliyotolewa na Hakimu K. Lugoye inaelekeza mali walizochuma pamoja wawili hao kugawanywa kwa kila mmoja. Hata hivyo kuna sintofahamu ya uhakiki wa mali hizo na sasa Lema anadai kuwa mali nyingi alizopaswa kuzipata zimepokwa na mtalaka wake Oliva ambaye nyendo zake zote kwa sasa zinaangaliwa kwa karibu na kaka yake, Thomas Mallya.
Oliva kwa upande wake anakanusha madai hayo kwa kueleza kuwa mali alizochukua ni zile tu alizogawiwa na mahakama huku akimnyooshea kidole aliyekuwa mumewe Simon kwa kushindwa kumtunza yeye na watoto wao na kwamba amekuwa mwalimu mbaya wa watoto kiasi cha kumlazimu yeye Oliva kuchukua hatua kali zilizowaingiza katika misukosuko mikubwa baada ya Oliva kuwashtaki polisi watoto wake kwa tuhuma za makosa ya jinai na hata kusimamia kukamatwa kwa mwanae wa kwanza wa kiume na kupelekwa katika vituo maalumu vya kuhifadhi watu wenye matatizo ya akili (sober house).
Mvutano unakwenda mbali zaidi ambapo Oliva ameeleza kuwa mali zote zilizopatikana wakati akiishi pamoja na aliyekuwa mumewe Simon zilitokana na jasho lake kwani ni yeye aliyekuwa akihusika kununua chakula cha familia na hata nguo za mumewe Simon ambaye kazi yake ilikuwa kukaa tu huku akitunzwa na mkewe (Oliva).
Lakini kwa upande mwingine wa Simon nao unaeleza kuwa Oliva amekuwa akicheza mchezo mchafu kujimilikisha mali zote walizochuma wakati wa maisha yao ndoa kwa msaada wa ndugu zake na kwamba utekelezaji wa hukumu iliyotokewa na Mahakama ya Mwanzo Kawe una walakini ambapo Oliva ametumia mwanya huo ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya kunyang’anya Simon mali ambazo alistahili.
Ni mgogoro unaotishia amani na usalama wa wanandoa hao pamoja na familia yao na katika makala haya maalumu, Tanzania PANORAMA Blog inaumulika mgogoro huo mzima ikianza na hukumu iliyotolewa na Hakimu Lugoye, mahojiano ya pande zote mbili pamoja na watu wa karibu ya wawili hao, utekelezaji wa hukumu na maoni ya kisheria ya wanasheria dhidi ya tukio zima.
Oliva Simon Lema alifungua shauri la madai ya takaka na machumo katika Mahakama ya Mwanzo Kawe, mwaka 2018. Shauri hilo lilipewa nambari 83/2018 ambapo Oliva alikuwa akidai talaka na machumo kwa mumewe Simon Lema.
Kwa mujibu wa hukumu ya Hakimu K. Lugoye, Simon na Oliva walifunga ndoa Septemba 15, 1984 na katika uhai wa ndoa yao walibahatika kupata watoto watano.
Kwamba matatizo katika ndoa ya Simon na Oliva yalianza mwaka 2008 baada ya mtoto wao wa kike kupata ujauzito ambapo Simon alimfukuza nyumbani mtoto huyo na kuwa; hadi Oliva anakwenda kudai talaka mahakani mtoto huyo alikuwa amepanga.
Hukumu inasomeka kuwa mahakama ilimpelekea Simon wito wa kuitwa mahakamani lakini alikataa kuupokea, ikabidi wito huo upitie kwa mjumbe wa shina zaidi ya mara moja bila mafanikio ndipo mahakama ikalazimika kusikiliza shauri hilo upande mmoja.
Olivia alidai mahakamani hapo kuwa alifunga ndoa na Simon 1984 wakiwa hawana chochote na walijitahidi kujiendeleza kwa yeye Oliva kukopa kwa ndugu zake na kufanya biashara ya duka kwa sababu mumewe hakuwa mtu wa biashara. Kwamba walikuwa na kiwanja ekari 14 eneo la Kimara ambacho Simon alitaka kukiuza.
Alidai zaidi kuwa Simon alikuwa hajali watoto kwani mtoto wao alipomaliza kidato cha nne na kurudi nyumbani akiwa na mimba, taarifa za mtoto huyo kuwa na mimba zilipofikishwa kwa Simon alisema Oliva aondoke na mtoto wake huyo na kuanzia hapo ndipo matatizo yalipoanza kwani baada ya mtoto huyo kujifungua, Oliva alimpeleka tena shule.
Aidha, Oliva alidai mahakamani kuwa walikuwa na nyumba Bunju iliyokuwa na ufa lakini kila alipokuwa akimwambia Simon waikarabati alikataa na kumtaka ajenge ya kwake kwa sababu hawezi kukarabati nyumba isiyokuwa ya kwake na mwaka huo wa 2018 alimtaka aondoke nyumbani ili yeye abaki akifanya kazi na watoto jambo ambalo alilikataa.
Kwamba baada ya kukataa, Simon alimwambia Oliva kuwa kama anataka kuendelea kuwa naye ahamie kwenye nyumba yao nyingine waliyokuwa wamepangisha huko Sinza, akakae huko kwa muda wa miezi mitatu jambo ambalo alilikataa na kuomba achukue kodi ya wapangaji waliokuwa kwenye nyumba hiyo ya Sinza kisha akapange sehemu nyingine kwa muda huo wa miezi mitatu.
Alidai aliondoka na kwenda kupanga hadi alipofungua shauri la takaka na machumo mahakamani kwani kila alipokuwa akimuomba Simon amrudishe nyumbani alikataa na hata kilipokaa kikao baina yao na watoto wao kwa ajili ya kutafuta suluhu Simon alikataa.
Alidai zaidi kuwa baada ya kuondoka, Simon alikuwa akipiga simu kwa watu na kuwaeleza kuwa mkewe Oliva ametoroka hajui alipo na amehamisha kila kitu hivyo aliamua kwenda TAMWA ambako Simon aliitwa na kuitikia wito lakini alifika alikataa kuongea chochote kwa kile alichosena anajisikia vibaya.
Alidai Simon aliwataka TAMWA wamwandikie anachokitaka Oliva na walipopangiwa tarehe nyingine ya kwenda kusikilizwa, Simon hakwenda hivyo Oliva aliambatana na watu wa TAMWA hadi ofisi za Serikali ya Mtaa ambako Simon aliitwa lakini huko nako alikataa kuongea chochote na kudai aandikiwe kinachohitajika.
Oliva alidai mahakamani kuwa Serikali ya Mtaa iliamua kumrudisha nyumbani kwake lakini Simon alikataa kumpokea na kueleza kuwa wakimuacha hapo atamuua.
Hukumu inarejea zaidi madai ya Oliva mahakamani hapo kuwa, alitaja mali alizochuma akiwa na Simon ni nyumba tisa, ya kwanza ikiwa Kimara King’ong’o, Matosa nyumba moja, Bunju nyumba mbili, Sinza nyumba moja, Nyaishozi nyumba moja, nyumba mbili mabwepande na moja ipo Moshi, Kilimanjaro.
Vingine alivyotaja ni baa mbili, moja ipo Bunju na nyingine Nyaishozi, nyumba ya wageni (guest house) ya ghorofa iliyopo Nyaishozi, viwanja vitano kimoja kipo Bunju, kingine kimoja kipo Chasimba, viwili vipo mabwepande (Manzese) pamoja na bwana la samaki na kimoja kipo Temeke.
Alitaja pia viwanja vinne vilivyopo mabwepande, shamba lenye ukubwa wa ekari tatu lililopo Mpiji, shamba la miti likilopo Mkoa wa Kilimanjaro lenye ukubwa wa ekari mbili, machimbo ya mchanga yaliyopo Mpiji ambayo eneo lake lina ukubwa wa ekari mbili, na magari saba ambayo ni tipa la kubeba mchanga, Nadia, Cheser, Corona, Pickup na Hyundai.
Hukumu inarejea zaidi madai ya Oliva mahakamani kuwa Simon alikuwa akisema ana viwanja 20 ambavyo hajui vipo sehemu gani na kwamba wana watoto watano wa mwisho akiwa na umri wa miaka 21 na kwamba anaye mdogo wake anayemhudumia anayeishi kwenye nyumba yao yenye wapangaji huko Sinza.
Oliva alidai zaidi mahakamani kuwa yeye ndiye alikuwa mpambanaji na kwamba ndugu zake Simon wanalijua hilo. Pia kulikuwa na tatizo la Simon kumfukuza nyumbani na kumtamkia kuwa bila wanawake wa nje hawezi kuishi na ndoa yao ilikuwa na umri wa miaka 35.
ITAENDELEA.