Mkurugenzi Mtendani wa Kampuni ya Mafuta ya Oryx, Kalpesh Mehta |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
KAMPUNI ya Mafuta ya Oryx sasa imeeleza kwamba ina kesi nne zinazoendelea kusikilizwa mahakamani pamoja na shauri moja la jinai lililo chini ya uchunguzi wa polisi.
Uongozi wa kampuni hiyo umedai kuwa haiwezi kujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari kwa kuwa kesi hizo zinaibana kampuni kuzungumzia tuhuma hizo nje ya utaratibu wa kisheria.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx, Kalpesh Mehta katika barua yake ya Agosti 15, 2022 iliyokuwa ikijibu barua ya Tanzania PANORAMA Blog ya Mei 17, 2022 iliyobeba maswali kadhaa kwenda kwa kampuni hiyo ikiomba kupatiwa majibu na ufafanuzi.
Katika barua yake hiyo, Mehta anaeleza kuwa kampuni anayoiongoza inafuata sheria na taratibu za nchi na pia inatunza maadili katika utekelezaji wa majukumu yake na hivyo kwa kutambua hilo haiwezi kutoa taarifa yoyote ambayo itaingilia mwenendo wa kesi hizo na shauri linalochunguzwa na polisi.
Kalpesh anazitaja kesi hizo kuwa ni kesi ya madai namba 258 ya mwaka 2020, kesi ya madai namba 19 ya mwaka 2019 na kesi za madai namba 10 na namba 45 za mwaka 2021, ambazo zinaendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Mahakama ya Wilaya Moshi na Mahakama ya Wilaya ya Hai, Bomang’ombe.
Aidha, Kalpesh anaeleza kuwa Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kilimanjaro inaendelea na uchunguzi wa kesi ya madai yenye namba KR/C/PE/09/2022. Kesi hiyo pia inaihusisha kampuni anayoiongoza na anaeleza zaidi kuwa kwa kutambua hayo, kampuni yake haipaswi kutoa taarifa yoyote wakati kesi zikiendelea.
Meia 17, 2022, Tanzania PANORAMA Blog iliwasilisha maswali kwa maandishi Makao Makuu ya Ofisi ya Kampuni Oryx yaliyopo eneo la Victoria, Dar es Salaam ikiomba kupatiwa majibu na ama ufafanuzi dhidi ya tuhuma na madai yaliyotolewa na mfanyabiashara Peter Kaale dhidi ya kampuni hiyo.
Miongoni mwa maswali hayo yalisomeka hivi; mosi, zipo taarifa kuwa Kampuni ya Oryx Oil Company Limited inao utaratibu wa kutuma wakaguzi kwenda kukagua mwenendo wa ubora wa huduma unaotolewa na wafanyabiashara walioingia mikataba nao kuendesha biashara zake za vituo vya mafuta. Taarifa hizi ni za kweli?
Na ni kweli kwamba Agosti, 2013 Oryx Oil Company Limited ilituma wakaguzi wake kwenda kukagua vituo vyake viwili, kilichopo Barabara ya Taifa na kilichopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Arusha (KIA) pamoja na mgahawa wa kisasa wa MEKUS PUB na kubaini havikuwa katika viwango bora vya utoaji huduma?
Pili, inaelezwa kuwa Septemba 13, 2013 mfanyabiashara Alphonce Mwasha aliyekuwa na mkataba na Oryx Oil Company Ltd wa kuendesha vituo vyake vya mafuta vya KIA na kilichopo Barabara ya Taifa pamoja na MEKUS PUB aliiandikia barua Oryx Oil Company Limited akitoa taarifa ya kutokuwa na uwezo wa kifedha wa kufanya ukarabati ulioelekezwa na Oryx Oil Company Limited. PANORAMA inaomba kujua, ni kweli Oryx walipokea barua hiyo?
Tatu, inadaiwa kuwa Septemba 18, 2013,, Oryx Oil Company Limited iliandika barua ya kukiri kupokea barua ya Alphonce Mwasha na katika barua hiyo ikikubali ombi lake la kushirikiana na kampuni nyingine katika biashara na ukarabati wa vituo vya mafuta vya KIA na Barabara ya Taifa pamoja na Mgahawa wa MEKUS PUB. Madai haya yana ukweli?
Nne, inadaiwa kuwa vituo vya mafuta vya KIA na kile cha Barabara ya Taifa pamoja na Mgahawa wa kisasa wa MEKUS baada ya kukamilika kwa ukarabati. Oryx ilimwandikia barua Alphonce Mwasha ya kutaka kumuondoa kwenye biashara zake kwa nguvu na bila kufuata utaratibu. Jambo hili ni kweli?
Tano, Je ni kweli kwamba mnamo Agosti 22, 2022 Alphonce Mwasha aliifungulia kesi mahakamani Kampuni ya Oryx. Na je kweli ni kwamba Septemba 20, 2017 Kampuni ya Oryx ilipokea wito wa kuitwa mahakamani.
Na ni kweli kwamba Oryx Oil Company Ltd iliomba shauri hilo liondowe mahakamani na badala yake litafutiwe suluhu nje ya mahakama? Na je, taarifa kwamba Oryx Oil Company Ltd na Mwasha walifikia makubaliano nje ya mahakama nazo zina ukweli wowote? PANORAMA Blog inaomba kujua makubaliano hayo yalizingatia nini?
Sita, inaelezwa pia kuwa Septemba 18, 2013 Oryx Oil Company Ltd iliandika barua ya kumtambua mpangaji wake mpya, Kampuni ya Community Petroleum Limited na kumpa jukumu la kuendesha biashara zilizokuwa zikisimamiwa na Mwasha, hili lina ukweli kiasi gani?
Saba, zipo taarifa kuwa Aprili 29, 2019 vituo vya mafuta vilivyopo barabara ya Taifa na KIA na Mgahawa wa MEKUS PUB vilivamiwa na mabaunsa waliokuwa wameongozana na viongozi wa Oryx Oil Company Limited na kutishia kuua wafanyakazi kwa silaha za moto, kuharibu nyaraka na kuiba pesa za mauzo katika vituo vya mafuta na Mgahawani. Hili unalizungumziaje?