Tuesday, December 24, 2024
spot_img

JINA LA TUNDU LISSU LINAPOANDIKWA KATIKA KITABU CHA HUKUMU

 

NA CHARLES MULLINDA

 KWA mara nyingine, historia ya siasa za Tanzania inaandikwa upya baada ya jina la Tundu Lissu kuchomekwa katika kitabu cha hukumu likiwa limeandikwa kwa wino uliokolea unaoumba maandishi yanayoumiza macho kuyasoma.

Jina la Lissu sasa linasomeka katika kitabu cha hukumu kuwa ni mwanasiasa aliyerejea nchini akitokea Ubelgiji alikokuwa akiishi baada ya kutibiwa na kupona matobo zaidi ya 10 ya risasi alizomiminiwa na magaidi wa utu wa mtu.

Halijaandikwa katika chapta moja, kuna chapta nyingine inayomuelezea Lissu kuwa mwanasiasa aliyegombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa staili ya kucheza na akili za Watanzania wachache hasa vijana wasiokuwa na mbele wala nyuma ili kutimiza dhamira yake ovu ambayo kwa hakika haikuwa kuwa Rais wa Tanzania, bali kuwa Mtanzania wa kwanza kuwasaidia wazungu kushika vizuri mpini wa kisu kuichinja Tanzania.

Lissu, mwanasiasa mwenye taaluma ya sheria sasa anasomeka katika kitabu cha hukumu kuwa mwanasheria aliyeitumia elimu yake ya sheria kuzitikisa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuangalia vipengele vya sheria vinavyotoa mwanya wa kuzishambulia moja kwa moja ofisi hizo, na au kuchagua maneno yenye ukakasi ambayo yalikuwa hayamfungi kisheria kuwashambulia washindani wake wakati wa kinyang’anyiro cha kuusaka urais na wakati mwingine vyombo vya dola.

Kitabu cha hukumu sasa kinamtaja Lissu kuwa mwanasiasa aliyefanikiwa sana kwa hila za kisiasa na pia mtu aliyefanikiwa kuwashambuliwa kwa maneno ya hovyo na kwa namna mbaya kabisa viongozi wakuu wa Tanzania pasipo kuchukuliwa hatua zozote kwa sababu siasa ni mchezo mchafu hivyo wanaoucheza wanaruhusiwa kuchafuana.

Anasomwa kwa bidii na watoto na wajukuu zetu kuwa mtu aliyehamasisha vurugu ili nchi iingie katika machafuko na pia mzushi wa kupindukia  aliyethubutu kuzusha uongo wa makusudi kwa watendaji wa serikali pasipo kuchukuliwa hatua yoyote.

Lissu ameandika historia mpya katika taifa letu kwa maneno na matendo yake ya hovyo yenye kila viashiria vya uovu dhidi ya taifa.

Chapta ya mwisho yenye wasifu wake inamwelezea Lissu kuwa ni mwanasiasa mtata, muongo, mjuvi wa sheria, mvurugaji, mtumishi wa wazungu aliyetumwa na mabwana zake kuja kufanya vurugu za kisiasa katika nchi ya baba na mama zake ili wamwage damu na hatimaye taifa liangamie lakini akashindwa kwa hoja zenye mashiko za mwanasiasa asiyecheka na nyani ambaye kwa sababu ya ucha Mungu wake, alimsamehe dhambi zake zinazosameheka.

Kitabu cha hukumu kinapoandikwa upya sasa, kinawakumbusha Watanzania kufanya mabadiliko ya sheria kadhaa zinazoongoza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na NEC ili kuziba mianya kwa watu wa aina ya Lissu kutumia kivuli cha uanasiasa kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

Ili kitabu hicho kihukumu kwa haki itailazimu kielezea mafanikio ya uovu wa Lissu yaliyoanza kuonekana mapema baada ya kutoka hospitalini Ubelgiji alikokuwa akitibiwa majeraha ya risasi alizopigwa katika shambulio baya lilitokea jijini Dodoma zaidi ya miaka mitatu iliyopita wakati akitokea bungeni kurejea nyumbani kwake kwa mapumziko ya mchana.

Lissu aliitumia vizuri nafasi hiyo kwa kuanza kuzunguka kwenye nchi mbalimbali za Ulaya na Amerika kuwaomba Watanzania wanaoishi huko pamoja na wazungu wamwangalie kwa jicho la huruma, wamchangie pesa za kujikimu yeye mwenyewe na pia za kuitunza familia yake na kusomesha watoto wake.

 

 


kulainisha mioyo ya aliokuwa amewalenga kumpa pesa, Lissu aliishambulia kwa namna ya kuisingizia serikali na vyombo vya dola kuwa ndivyo vilivyomshambulia na kwa sababu waafrika wasiokuwa na akili sawasawa wamejengewa mawazo kuwa staili ya serikali nyingi za wazungu kuwashambulia na hata kuwaua wanasiasa wa upinzani ndiyo inayotumiwa pia na serikali za kiafrika, aliaminika kirahisi. Akajazwa mapesa.

Mbali ya kupita akiombaomba kwa wananchi wa kawaida na taasisi mbalimbali za wazungu, Lissu alipitapita pia kwenye taasisi zinazohubiri na kutekeleza matendo ya dhambi ambazo nazo zilimchangia na alifanya nazo mazungumzo ambayo yanahitaji uwanja mwingine kujadili.

Jambo moja lililobainika katika ziara za Lissu kwenye baadhi ya mataifa ya Ulaya na Amerika kuombaomba ni kuwa, watu wengi, waafrika na wazungu ni bendera fuata upepo na ama huwa hawana muda wa kufikili sawasawa hivyo haikuwa kazi ngumu kwa Lissu kuwaaminisha kile alichotaka yeye waamini.

Hawakuwa na muda wa kujiuliza tangu lini mzungu alimpenda muafrika kwa moyo wa dhati, hawakujiuliza wema wa wazungu kwa Lissu hata kubeba jukumu zito la kugharamia matibabu yake pamoja na malazi na chakula kwa wategemezi wake aliokwenda nao Ubelgiji ulitoka wapi.

Wazungu wenyewe wabelgiji! ambao juzi tu walikuwa wakiwaita waafrika nyani! Wabelgiji waliokuwa wakiwakata vichwa na mikono waafrika waliochoka kwa kutumikishwa kazi ngumu na madhefuli hao, Wabelgiji wezi wakubwa wa rasilimali za Afrika, ghafla wakawa malaika walinzi wa Lissu!

Waafrika wenzetu hawa walishindwa kabisa  kutumia mbongo zao kujiuliza maswali mepesi kuwa ni kwanini Lissu baada ya kupona hakutaka kurudi nyumbani na badala yake alianza kuzunguka Ulaya na Marekani akiichafua nchi yake, hawakijiuliza nauli ya kuzunguka Ulaya na Marekani aliipata wapi kama aliishiwa hadi pesa ya kula na ya kulipa karo ya watoto wake.

Binadamu wanaojidanganya wana akili walishindwa kuzitumia akili zao kujiuliza ni kwanini Lissu aliamua kwa makusudi tu kukaidi maagizo ya mwajiri wake (Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) lililokuwa likimlipa mshahara mnono na marupurupu kibao ili afukuzwe kazi (Ubunge) na kuendelea na ziara ya kuichafua Tanzania na Watanzania kwa kivuli cha kuombaomba?

Hakuna hata mmoja kati ya waliomchangia aliyejiuliza ni nani aliyelipa gharama za matibabu ya Lissu katika Hospitali ya bei mbaya Ubelgiji ambaye alishindwa kumpa pesa ya kujikimu lakini akaweza kumkatia tiketi ya ndege kuzunguka Ulaya na Marekani kuitukana Tanzania duniani kote.

Waafrika wote waliomchangia walitumia moyo badala ya akili kuyapima maneno yake. Kwa sababu ya udhaifu wa mioyo yao wakadanganyika na ghilba zake wakammiminia mapesa, Waafrika wepesi sana kudanganywa. Lissu akiwa na mapesa yao akaendelea kula kuku Ulaya huku akiwaamisha kuwa iwapo atarejea Tanzania maisha yake yatakuwa hatarini.


Akiwa huko huko Ulaya, Chadema kikafanya uchaguzi kikamchagua kuwa makamu mwenyekiti taifa bila yeye mwenyewe kuwepo. Hakuna mjumbe wa mkutano ule wala mwanachama aliyehoji kuwa mtu ambaye hawezi tena kurudi Tanzania ana umuhimu gani kuliko wengine wote katika kundi hilo hata kupewa wadhfa huo? Lakini pengine ni kwa sababu walijua atarejea kuja kufanya aliyoyafanya wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2020 na hata baada ya uchaguzi mkuu.

Lissu, tofauti na alivyoutangazia ulimwengu kuwa hawezi kurejea nchini kwa sababu ya kuhofia usalama wake, siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu alirejea na kupokelewa kwa amani na chereko chereko na wanachama na mashabiki wa kikundi chake.

Safari yake kurejea nchini ilikuwa ya kuja kufanya kazi maalumu aliyoifanya kwa miezi mwili wakati wa kampeni ambayo Watanzania na dunia nzima waliiona.

Aliianza kwa kasi kubwa kwani baada tu ya kutua alimuongoza Mbowe na  viongozi wengine wa Chadema kukiuka utaratibu wa kufika msibani kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Hayati Benjamin Mkapa, Rais wa Awamu ya Tatu.

 


Alipoelezwa kuwa amekiuka utaratibu kwa makusudi hivyo hataruhusiwa kuingia uwanjani mpaka atakapoufuata akapaza sauti kuwa serikali imeanza kumuonea. Wasiokuwa na akili wakaungana naye kupayuka anaonewa na uongo huo ukasambazwa na wazungu waliomtuma lakini serikali iliupuuza na haina shaka iliupuuza kwa kutumia busara ya kawaida kabisa ya waungwana hawazozani msibani.

Hilo lilipita na walioaminishwa na Lissu kuwa akirejea Tanzania maisha yake yatakuwa hatarani bado wanasubiri mpaka leo yawe hatarini. Wakiwa kwenye kusubiri ndipo alianza kucheza na akili za vijana wachache wa kitanzania ili wamsaidie kuiangamiza Tanzania. Twende taratibu ili tuelewane vizuri.

Lissu kwa sababu anajua vijana wengi wa kiafrika wenye akili kama za kwake hawapendi kwao na vya kwao alianza kampeni zake kwa kuhubiri kuwa Watanzania hawana uwezo wa kujitegemea!  Eti! wao ni tegemezi tu kwa wazungu.

Akaenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa mafanikio yaliyofikiwa sasa na Watanzania katika sekta ya madini si lolote wala chochote hivyo akichaguliwa yeye kuwa rais, madini ya Tanzania atayakabidhi kwa wazungu waliomtuma kuja kulichonganisha taifa ili Watanzania wamwage damu.

Haina shaka hata kidogo kuwa kauli hii ys hovyo ya Lissu kuhusu kuyatoa madini yetu kwa wazungu ilibeba makubaliano yake na vinara wa uuzaji madini duniani wakati mataifa yao hayana chembe ya madini.

Wapo Watanzania walioshangilia na walishangilia kwa sababu wana njaa na wana njaa kwa sababu hawataki kufanya kazi. Lissu alicheza na njaa njaa zao, akawadanganya kuwa akiwapa wazungu madini yetu wataishi maisha ya kula bure.

Genge la Watanzania hawa, limesahau kuwa ni juzi tu kabla ya kurekebishwa kwa sheria ya madini, wazungu  waliokusudiwa kupewa madini yetu na Lissu walikuwa wakiwatandika waafrika kama mbwa huko migodini. Wamesahau kuwa dada zetu walikuwa wanafanyishwa mapenzi na mbwa. Tamaa yao ni kula bure. Kwa akili ya kichokonozi, hawa kama walijiandikisha kipiga kura nadhani ndiyo waliompigia kura Lissu.

Wezi, vibaka, majambazi, wazinzi na wazururaji, Lissu amefanikiwa sana kuziteka akili zao. Amewaaminisha wahalifu hawa kuwa amani ni kitu cha hovyo na wao wamemuelewa sana kwa sababu katika machufuko na pasipo na ulinzi na usalama wa raia na mali zao, wahalifu hufaidika kwa kutekeleza vitendo vya kihalifu.

Lissu kwa kutambua akili mbaya za makundi haya alichokifanya ni kuchochea moto katika akili za wezi, vibaka na majambazi wanaokosa vipato haramu kwa sababu serikali inapambana nao kwa kutumia jeshi la Polisi.

Alifanya hivyo kwa sababu anajua Serikali ya Rais John Pombe Magufuli, imefanikiwa sana katika mapambano dhidi ya wezi, vibaka na majambazi. Taifa sasa liko salama ili kulivuruga lazima kuyachochea makundi ya kihalifu yaanzishe vurugu.

Amani na mshikamo kwa raia wema wa Tanzania ni wa kiwango vya juu sana. Watanzania wachache wahalifu waliofanikiwa kukwepa mikono ya sheria hivyo wapo uraini, wanaishi kwa tabu sana. Na hawa ndiyo aliowalenga Lissu katika harakati zake za kuusaka urais tangu aliporejea nchini.

Hakuna raia mwema wa Tanzania anayeweza kuwa na mawazo ya  kuingia barabarani kuharibu amani ya nchi baada ya mipango ya Lissu kuharamisha utanzania wa watanzania kushindwa, bali wezi, vibaka na majambazi ndiyo wanaoweza kufanya hivyo.

Lissu alitaka yafanyike maandamano ili polisi waje kuwatawanya waandamanaji kisha wao wakaidi, itokee vurugu, wavamie maduka na nyumba za raia wema waibe.

Hilo lingetokea damu ingemwangika na hapo ndipo waliomtuma Lissu wangeshupaza mishipa ya shingo kutaka kuja kutavamia kwa kisingio cha kulinda amani.

Tayari Lissu ameishakimbilia kwa wazungu kwenda kujificha hata kabla hajaulizwa kwanini amepungukiwa adabu hata ile ya kusingiziwa tu. Ili tuwe salama hatuna budi kuwakataza wafuasi wake aliowaacha kwa staili inayorandana na matendo yao maovu.

Historia ni mwalimu mzuri na hutenda haki kwa kila mmoja na kwa kila tukio. Kitabu cha hukumu ni sehemu ya historia. Kama ambavyo historia imekuwa ikitenda haki siku zote, itaendelea kutenda haki kwa kutunza simulizi ya mambo ya hovyo ya Tundu Lissu na genge lake. Tusome historia.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya