![]() |
Sehemu ya eneo la ufukweni mwa Bahari ya Hindi linalomilikiwa na Ras Bamba |
MWANDISHI WA PANORAMA
KWA zaidi ya miaka 20 sasa, kipande cha ardhi chenye ukubwa wa ekari 250 ambacho sehemu yake kubwa imehifadhiwa na mmiliki wake kwa ajili ya kutunza misitu na mazingira, lengo likiwa kuvutia biashara ya utalii kimekuwa katika mgogoro mkubwa unaodaiwa kuzaa chuki, dhuluma na vitisho.
Inadaiwa ardhi hiyo ambayo hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 ilikuwa mithili ya jangwa, ilimilikishwa kwa Flora M’mbugu Schelling, mwanamke Mtanzania aliyeolewa na Dieter Schelling, raia wa Uswisi aliyepata kuishi hapa nchini kwa miaka mingi akifundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye akawa mtumishi wa Benki ya Dunia, ambaye aliliendeleza eneo hilo kwa kupanda miti ya asili na kujenga hoteli na mabanda ya kupumzikia ya kitalii.
Taarifa zilizokusanywa na Tanzania PANORAMA Blog katika uchunguzi wake kuhusu kiini cha mgogoro wa ardhi hiyo ambao ni baina ya mwekezaji (Schelling) na Serikali ya Wilaya ya Kigamboni inayodaiwa kutaka kulinyakua eneo hilo kwa mabavu zimeonyesha kuwa baada ya kuendelezwa na kuwa la kuvutia, lilianza kugombaniwa na baadhi ya wafanyabiashara huku baadhi ya viongozi wa Serikali wakichukua mwelekeo mwingine kuhusu uhalali wa umiliki aliokuwa amepewa Schelling na Serikali.
![]() |
Nyumba ya kiasili kwa ajili ya malazi kwa watalii iliyo upenuni mwa ufukwe wa Bahari ya Hindi katika eneo la Ras Bamba |
Uchunguzi wa Tanzania PANORAMA Blog umeonyesha kuwa eneo hilo la ardhi linamilikuwa na Kampuni tatu ambazo ni Oyster Camp Limited, Ras Bamba Sailing Club Limited na Ras Bamba Hotel Limited ambazo mkurugenzi wake ni Flora Schelling.
Baadhi ya nyaraka zilizoonwa na Tanzania PANORAMA Blog katika uchunguzi wake zimeonyesha kuwa eneo hilo linalofahamika zaidi kwa jina la Ras Bamba lina viwanja vinne, cha kwanza kikiwa ni plot namba 4 chenye hati namba 43672 iliyotolewa mwaka 1994 ambacho kinamilikiwa na Kampuni ya Oyster Camp Ltd.
Zinaonyesha zaidi kuwa kiwanja cha pili ambacho ni ‘Farm’ namba 2595 chenye hati namba 43868 iliyotolewa mwaka 1994 nacho kinamilikiwa na Kampuni ya Oyster Camp Ltd na viwanja vingine viwili vilivyopimwa lakini havikupata kupewa hati lakini vipo kwenye eneo lililo ndani ya ramani ya mipango miji nambari 1/690/192 na 1992.
Kwa mujibu wa nyaraka, kati ya hivyo, kiwanja kimoja kinamilikiwa na Kampuni ya Ras Bamba Sailing Club Ltd, kikiwa na ukubwa wa ekeri 3.3 na kingine kina ukubwa wa ekari 4.4 kikimilikiwa na Kampuni ya Ras Bamba Hotel Ltd.
Moja ya nyaraka ambazo Tanzania PANORAMA Blog imeziperuzi katika uchunguzi wake wa iwapo taratibu za umiliki wa viwanja hivyo zilifuatwa, ambayo iliwasilishwa na kupokelewa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Machi 23, 2020 inasomeka;
“Taratibu za kuomba kumilikishwa ardhi hii ya Ras Bamba zilianza tangu mwaka 1989/1990. Ili tuweze kuwekeza katika ardhi yetu tulichukua jukumu la kuiomba Wizara ya Ardhi kuliweka eneo hili katika ramani ya mipango miji ili tuweze kuwekeza bila kukinzana na sheria ya mipango miji ya mwaka 1992, eneo lote liliwekwa katika ramani ya mipango miji. Tulilipa ghamaza zote za upimaji wa hili eneo.”
Inasomeka zaidi kuwa “Mwaka 2010 tuliona ili tuweze kuwekeza vizuri zaidi katika eneo letu tuliamua kujiandikisha na Tanzania Investiment Center (TIC), mwaka huo huo tulipata hati ya usajili yenye namba 031467. Usajili huo ulitupa motisha ya kuweza kuendelea kuwekeza katika eneo hili. Tumewekeza zaidi ya shilingi bilioni tatu. Katika uwekezaji wetu tumejenga majengo, miundombinu, maji na tumevuta umeme kutoka umbali wa kilomita 2.2”
Uchunguzi umeonyesha kuwa mgogoro katika eneo hilo ulianza mwaka 2004 baada ya Wizara ya Ardhi kubatilisha hati ya ploti namba 4 lakini mmiliki aliendelea kudaiwa kodi ya ardhi na kulipa na baadaye 2017 kiongozi mmoja wa Wizara ya Ardhi (jina linahifadhiwa kwa sababu hajapatikana kuzungumza) alitoa ruhusa kwa mmiliki kuendelea na shughuli zake za uwekezaji lakini asitishe kulipa kodi ya kiwanja namba 4 mpaka atakapomilikishwa upya.
![]() |
Moja ya maeneo ya kupumzika watalii iliyozungukwa na miti ndani ya eneo la Ras Bamba iliyo upenuni mwa ufukwe wa bahari |
Aidha, alielekeza kuwa ‘farm’ namba 2595 ibadilishwe matumizi lakini viwanja viwili, kimoja kinamilikiwa na Kampuni ya Ras Bamba Sailing Club na kingine kinamilikiwa na Kampuni ya Ras Bamba Hotel Ltd, Kamishna wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam ashughulikie hati zake, lakini hadi sasa maelekezo hayo hayajatekelezwa.
Baadhi ya wenyeji wa eneo hilo waliofikiwa na kuhojiwa kuhusu mgogoro wa ardhi hiyo walieleza kuwa mgogoro wa pili uliibuka baada ya mtu waliyemtaja kwa jina la Petro Haule kuvamia kiwanja kilicho chini ya Kampuni ya Ras Bamba Sailing Club kilicho kwenye ramani ya mipango miji nambari 1/690/192.
“Huyo Haule yeye alikwenda mahakami akishtaki kuwa ndani ya kiwanja hicho ana eneo lake lakini alishindwa kesi mwaka 2017 na alilipa gharama za kesi.
“Haikushia hapo, yaani hapa licha ya kuwa pana utamu wake lakini pana machungu yake kwa sababu kuna migogoro kweli kweli, huyo mwekezaji amekutana na misukosuko mingi sana, mgogoro mwingine ulihusisha kiwanja cha Ras Bamba Hotel Ltd chenye ekari 4.4 ambacho kundi la watu, mimi sitaki kulitaja bwana nyie fuatilieni tu mtawajua liliuza viwanja ndani ya eneo hilo na hata Quality Group ile ya Yusuf Manji nayo iliuziwa kiwanja kwenye eneo hilo, kiwanja namba 15. Hapo napo hapako sawa.
Baadaye uliibuka mgogoro mwingine kwenye eneo lake jingine huyo mwekezaji, liko kule linaitwa kisiwa dege. Kuna mama alikuja, anaitwa Jamila Jumbe akadai ni lake, akawatingisha mpaka wakasitisha kuliendeleza halafu akapotea na hivi sasa limegeuka kuwa la wachoma mkaa, hakuna tena shughuli za uwekezaji hapo,” alisema mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyeomba jina lake kuhifadhiwa.
![]() |
Moja ya nyumba za makazi ya wafanyakazi wa Ras Bamba. Kampuni ya Ras Bamba ilikuwa imeajili wafanyakazi 10 kabla ya kusitisha shughuli zake. |
Mwenyekiti wa kikundi cha wavuvi wanaofanya shughuli zao ndani ya eneo la mwekezaji huyo kinachofahamikwa kwa jina Beach Management Unit (BMU), Fundi Mussa ambaye naye amefanya mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo, pamoja mambo mengine ameeleza kuwa kiini cha mgogoro huo ni wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa na madalali wa ardhi wakishirikiana na baadhi ya viongozi kuanzia ngazi ya kata, wilaya hadi wizarani kulimezea mate kutokana na kuwa liko ufukweni na lina uoto wa asili.
![]() |
Mwenyekiti wa kikundi cha wavuvi cha BMU, Fundi Mussa (katikati aliyevaa fulana ya njano) akielezea kiini cha mgogoro wa eneo la Ras Bamba kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) |
“Unajua hili eneo kwa Mkoa wa Dar es Salaam yote huwezi kukuta eneo kama hili, kwanza lipo ufukweni lakini pia hii hali yake ya kuwa na uoto wa asili ambao huu uoto wa asili lakini ni wa kupandwa. Huyu mwekezaji alipokuja alianza kupanda hii miti yote kwenye hili eneo na ile mikoko kule yote kapanda yeye na kupaendeleza mpaka pakawa hivi.
“Kununua kipande cha ardhi kidogo tu kwenye eneo hilo kwa sasa ni mamilioni ya pesa ndiyo maana pana migogoro kila siku lakini sasa inakuwa mbaya zaidi viongozi kuhusika ingawa nao ni binadamu wanaweza kuwa na tamaa lakini wangezingatia dhamana walizonazo za uongozi ingekuwa safi zaidi.
“Hapa ni pazuri sana kweli, lakini kwa zamani kabla yule mwekezaji hajakimbia, hivi sasa kila siku kuna hekaheka, wanakuja watu mara kupima viwanja, wengine madalali, ni vurugu tu,” alisema Fundi Mussa.
Tanzania PANORAMA Blog lilipata taarifa na kuthibitisha kuwa eneo hilo ambalo awali mmiliki wake aliyejisajili TIC kuwa mwekezaji, lilikuwa likitumiwa zaidi kwa biashara ya utalii na hoteli, hivi sasa shughuli hizo zimesitishwa kutokana migogoro ya kuligombea na mmiliki wake amekimbilia nje ya nchi kwa kile kinachodaiwa ni kuhofia
Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa migogoro ya ardhi hapa nchini na baadhi ya watumishi wa Wizara ya Ardhi wamekuwa wakinyooshewa vidole kwa kuhusika na migogoro hiyo.
Wiki iliyopita, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete akiwa Mkoa wa Geita, aliitaja wizara hiyo kuwa kinara ya changamoto za kuiongoza kutokana na watumishi wake kuandamwa na tuhuma za kuijihusisha na migogoro ya ardhi.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, anayedaiwa kuwa katikati ya mgogoro huo, amefanya mahojiano mara mbili na Tanzania PANORAMA Blog na kueleza kuwa hayuko kwenye nafasi ya kuzungumza kutokana na kuandamwa na majukumu ya kazi na hivi karibuni alisema amekwishazungumzia mgogoro huo mara kadhaa kisha akaongeza kuwa yupo msibani atafutwe atakaporejea.
![]() |
Wavuvi wanaotumia ufukwe ulio ndani ya eneo la Ras Bamba wakikokota mtumbwi wao kwenda kuugesha baada ya kutoa kuvua samaki baharini |
Jitihada za kumpa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuzungumzia mgogoro huo hazikuweza kufanikiwa baada ya simu kutopatikana.
Tanzania PANORAMA inaendelea na uchunguzi wa mgogoro huo.