RIPOTA PANORAMA
NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Zanzibar (ZPDC) yamesaini makubaliano ya kushirikiana katika mambo mbalimbali.
Akizungumza mapema wiki bungeni mjini Dodoma, Kapinga alisema makubaliano hayo yalisainiwa Februari, 2022 na hivi sasa, pamoja na mambo mengine TPDC na ZPDC zinashirikiana kwa kubadilishana ujuzi na utaalamu.
Akijibu swali la Mbunge wa Kwahani, Khamis Yussuf Mussa Mkenge aliyeuliza ni lini serikali itainufaisha Zanzibar katika matumizi ya Nishati ya Gesi ili iweze kutumika katika magari, alisema ajenda iliyopo sasa ni kupeleka gesi Zanzibar.
“Mheshimiwa Spika katika ushirikiano huu, suala la kupeleka gesi Zanzibar ni mojawapo ya ajenda kuu. Pande zote mbili bado zinaangalia namna bora ya kufikisha gesi asilia Zanzibar ili iweze kupatikana kwa bei nafuu kwa watumiaji,”. alisema Kapinga