Thursday, July 17, 2025
spot_img

POLISI WAULIZANA FAILI LA DAWA ZA KULEVYA

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (mbele) Ramadhani Kingai

MWANDISHI WA PANORAMA

IKIWA imepita miezi sita sasa tangu kukamatwa kwa vijana saba wakivuta dawa za kulevya na kulima bangi katika nyumba ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, Ramadhani Nyamka iliyoko mkoani Dar es Salaam, jana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni limesema halina uhakika wa mahali lilipo faili la uchunguzi na wapi ulipofikia.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Kamishna Msaidizi, Ramadhani Kingai alisema hana uhakika kuhusu mwenendo wa faili hilo na mahali lilipo, lakini aliahidi kulifuatilia na kutoa taarifa baada tu ya kulipata.

Kamanda Kingai ambaye alikuwa akijibu kuhusu mwenendo wa uchunguzi na hatua zilizochukuliwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa timu iliyoundwa mwaka jana na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo kutafiti chanzo cha kutoroshwa kwa mwanafunzi wa bweni aliyekuwa akisoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya St, Mary’s, Lubna Salim Said, alisema matokeo ya uchunguzi huo anayeweza kuyazungumzia ni Chongolo.

Alipokumbushwa kuwa watuhumiwa hao wa dawa za kulevya na kilimo cha bangi walifikishwa polisi na katika mahojiano yake ya awali alikiri hilo na kuahidi kutoa taarifa baada ya uchunguzi kukamilika, alisema hilo la dawa za kulevya hana uhakika faili lipo wapo lakini mambo mengine yote yaliyomo kwenye ripoti ya kamati, anayeweza kuyazungumzia ni Mkuu wa Wilaya, Chongolo.

Mwanafunzi Lubna Said



“Lakini si unajua kuwa mtoto alipatikana? Alipatikana huko Stakishari. Lakini anayeweza kuzungumza kuhusu hiyo ripoti ni mkuu wa wilaya, mtafuteni mwenyewe ndiyo aseme kilichobainika kwenye uchunguzi… hili la hawa wa dawa za kulevya sina hakika faili liko wapi na limefikia wapi. Ngoja nifuatilie nini kinaendelea, nikipata majibu nakuja kwako,” alisema Kamanda Kingai.

Watuhumiwa hao saba, walikamatwa katika msako wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya St, Mary’s wakiwa katika nyumba ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Nyamka, ambaye pia ni Kamishna wa Utawala na Rasilimali Watu wa Jeshi la Magereza wakivuta dawa za kulevya, wakiwa na dawa za kulevya ndani ya nyumba hiyo na pia kukiwa na shamba la bangi kwenye au unaozunguka nyumba hiyo.

Taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa hao zilitolewa kwa Tanzania PANORAMA Blog na Joseph Kapere ambaye ni Mwenyekiti wa Timu ya Uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya, Chongolo na baadaye kuthibitishwa na Kamanda Kingai.    

Akithibitisha kuwepo kwa tukio hilo Oktoba mwaka jana, Kamandsa Kingai alisema watuhumiwa hao wa dawa za kulevya ni wanafunzi hivyo Jeshi la Polisi limeachiwa kwa ruhusa ya kiutu, kwenda kufanya mtihani wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya St Mary’s, kwa sababu ni wanafunzi katika shule hiyo na watakapomaliza tu kufanya mitihani yao hatua za kisheria dhidi ya tuhuma zinazowakabili zitachukuliwa.

Katika mahojiano hayo ya awali, Kamanda Kingai alikataa kutaja majina ya vijana hao, jina la Kamishna wa Magereza ambaye vijana hao walikutwa nyumbani kwake wakiwa na dawa za kulevya, kukilimwa bangi eneo la uani la nyumba hiyo wala mahali ilipo.

Mapema akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Chongolo, Kapere alisema kubainika kwa vijana hao na nyumba hiyo kulitokana na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Mary’s, Ntipoo Yissambi kuipeleka timu ya uchunguzi katika nyumba aliyokuwa akiishi mwanafunzi Lubna na mpenzi wake baada ya kutoroshwa kutoka shuleni, lakini waliwakosa na badala yake walikuta wavulana saba wakiwa wanavuta bangi.

“Mkuu wa shule anapajua alipotorokea mtoto huyo na alitupeleka kwenye hiyo nyumba. Ni nyumba ya Kamishna wa Magereza ambayo wanaishi watoto wake wawili lakini hapo hatukumta Lubna wala ‘boy friend’ wake, tulikuta vijana saba waliokuwa wanavuta bangi na nyumba nzima ilikuwa imetapakaa misokoto ya bangi.

“Kwa kweli ni hali ya kutisha sana kwa vijana wetu. Walituambia ni kweli Lubna alipotoroka shule alikuwa akiishi hapo na ‘boy friend’ wake na alikuwa mama wa nyumbani kwani alikuwa akiwapikia na kufanya usafi wa nyumba lakini baada ya muda kidogo aliondoka.

“Boy friend wake naye hatukumkuta, wale vijana wavuta bangi walisema anasoma chuo CBE na anaishi hosteli, sasa tumepeleka makachero akakamatwe huko.

“Lakini hiyo nyumba baada ya kuichunguza kwa sababu ina uzio mkubwa sana tulikuta shamba la bangi humo ndani. Yaani bangi inalimwa humo humo nyumbani kwa Kamishna wa Magereza, wanavuna, kisha wanavuta hao vijana.

Basi wale vijana tuliwachukua hadi polisi wamelala huko kwa ajili ya uchunguzi zaidi na taratibu nyingine zitafuata,” alisema Kapere.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime



Kabla ya kufanya mahojiano na Kamanda Kingai, Tanzania PANORAMA Blog lilimtafuta msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime na kumuuliza pamoja na mambo mengine ni kwanini watuhumiwa hao wa kutumia na kulima dawa za kulevya hawajachukuliwa hatua kwa takribani miezi sita sasa lakini alikataa kuzungumza lolote kwa maelezo kuwa anayepaswa kulizungumza ni Mkuu wa Wilaya, Chongolo aliyeunda timu ya kufanya uchunguzi.

Aidha, alipotafutwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Nyamka kuzungumzia suala na kilimo cha bangi katika nyumba yake, kuishi genge la vijana wanaotumia dawa za kulevya na mwanaye kumtorosha shuleni mwanafunzi wa kidato cha tatu, baada tu ya mwandishi kujitambulisha, aling’aka kwa ukali na kuhoji kwa nini mwandishi aliandika habari hiyo bila kumtafuta kwanza.

“Unasema nani? Ndiyo wewe wa Tanzania PANORAMA. Nyamaza kwanza, nataka uniambie ni kwanini aliandika hizo habari bila kunitafuta kwanza. Eeeeeh, nambie, ni kwanini,,,,,?” aling’aka Kamishna Msaidizi Mwandamizi Nyamka.

Mwanafunzi Lubna anadaiwa kutoroshwa na Rahim Nyamka usiku wa Oktoba 4, 2020 ambaye alimpeleka katika nyumba ya baba yake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Nyamka ambako pamoja na mambo mengine alimvutisha bangi.

Taarifa za kutoroshwa kwa mwanafunzi Lubna zilifichwa na uongozi wa Shule ya Sekondari ya St Mary’s hadi ziliporipotiwa katika Kituo cha Polisi cha Stakishari na wazazi wake na kupewa RB  STK/RB/10714/2020 na jalada la upelelezi wa kesi hilo lilikabisdhiwa kwa Askari Polisi Mpelelezi, Gwake Mwakapande.

Polisi Mwakapande alipohojiwa na Tanzania PANORAMA Blog alikiri kuifahamu kesi hiyo na kuieleza kuwa yeye ndiye alikuwa akisimamia upelelezi wake.

Akizungumza kwa mara ya kwanza na Tanzania PANORAMA Blog, kwa maneno yake mwenyewe, alisema ‘hiyo kesi ipo, naifahamu, mimi ndiyo naisimamia, naipeleleza mimi lakini hapa nilipo nipo kwa kinyozi nanyoa nywele, naomba nipe muda kidogo nimalize halafu nitakupigia nikitoka hapa,” alisema

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo



Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Chongolo alipata kuithibitishia Tanzania PANORAMA Blog kuitisha na kuongoza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Wilaya baada ya kupata taarifa za kutoroshwa kwa mwanafunzi Lubna ambapo aliunda timu ya maafisa wa Serikali kufanya uchunguzi.

Katika mahojiano hayo, Mkuu wa Wilaya Chongolo alisema timu aliyoiunda kufanya uchunguzi huo inajumuisha vyombo vya ulinzi na usalama na mwenyekiti wake ni Afisa Elimu Sekondari wa Walaya ya Kinondoni, Joseph Kapere, na wajumbe ni Mdhibiti Ubora wa Shule, RPC Kinondoni aliyekuwa akiwakilishwa na Inspekta Gwaki Mwakapande na Afisa Usalama wa Manispaa ya Kinondoni (DSO), Ngusa Mabula.

Alisema timu itafanya kazi hiyo usiku na mchana mpaka mwanafunzi huyo atakapopatikana na kukabidhiwa ripoti ya uchunguzi na pia aliahidi kutoa taarifa kuhusu sakata hilo.

Jitahida za kumtafuta Mkuu wa Wilaya Chongolo kuzungumzia suala hilo hazijafanikiwa baada ya kutokuwepo ofisini kwa muda mrefu kutokana na kuaandamwa na maradhi na hata alipotafutwa jana, simu yake iliita bila majibu.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya