ZERUBABEL CHUMA, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Taka Mkoa wa Dar es Salaam kupunguza gharama za uendeshaji wa mradi wa maji wa Wilaya ya Ubungo.
Chalamila alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Serikali katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema mradi huo ulio chini ya Wizara ya Maji umegharimu zaidi ya Sh. bilioni 36 na unahudumia Kata ya Kwembe na nyingine za jirani huku gharama za uendeshaji wake kwa mwezi zikiwa Sh. bilioni 2.
“Nimefurahishwa na mradi huu ambao serikali imeutekeleza katika wilaya hii, lakini pia kuna mradi wa tenki la maji la Bangulo ambao utahudumia eneo hili sambamba na mradi huu.
“Ushauri wangu kwa DAWASA, mradi huu upunguze gharama za uendeshaji zinazolipwa kwa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), nawashauri mfanye ushirika na Wizara ya Nishati, mtafute namna nzuri ya kuzalisha umeme wenu ili mchangie kiasi cha umeme. Njia hiyo itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendesha mradi huu,” alisema Chalamila.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange akizungumza kwenye mkutano wa hadhara ambao Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alikuwa akisikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo jana.
Katika hatua nyingine ya ziara yake jana, Chalamila alitembelea jengo la zahanati lililopo eneo la Mpiji, Kata ya Mbezi, ambako aliweka jiwe la msingi.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi, alisema ujenzi wa zahanati hiyo umegharamiwa na nguvu za wananchi na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kulipa kodi.
Chalamila alimtaka fundi ujenzi, Yassin Athuman Juma aliyepewa kandarasi ya kujenga jengo la Zahanati ya Mpiji- Majohe kutekeleza kazi hiyo kikamilifu.
“Nimefanya ukaguzi katika jengo hili, lakini sijaridhishwa na ukarabati wa mwisho katika mbao za milango na sakafu chini. Huu ni mradi unaotokana na kodi za wananchi hivyo lazima ziheshimiwe.
“Namkumbusha huyu fundi hata kama ni fundi wa kawaida, asifanye vitu vya kawaida. Anapaswa kufanya kazi kwa ubora hivyo niseme siku moja nitakuja hapa kwa kushtukiza, nikikuta marekebisho niliyoyataja hapa hayajafanyiwa kazi nitamchukua nitamkabidhi kwenye vyombo vya dola,” alisema.
Wakati huo huo, Chalamila alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo kutoa Shilingi milioni mia moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Saranga.
Agizo hilo alilitoa jana alipokuwa akizungumza na wakazi wa Saranga kabla ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na serikali katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Chalamila aliwataka wakazi wa Saranga kuwa wavumilivu wakati serikali ikichukua hatua ya kutatua kero ya muda mrefu ya ubovu wa barabara katika eneo hilo.
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA WAKATI YA ZIARA YA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM, ALBERT CHALAMILA KUKAGUA MIRADI INAYOTEKELEZWA NA SERIKALI KATIKA MKOA WA DAR ES SALAAM JANA.





