Wednesday, July 16, 2025
spot_img

UKIFIKA IRINGA NENDA KATALII KWENYE JIWE LINALOONGEA

GANGILONGA, neno la Kihehe, ni jina la jiwe; maana yake ni jiwe linaloongea. Jiwe la miujiza ambalo hapo zamani lilikuwa likiongea.

Jiwe la Gangilonga lipo Iringa mjini na ni kivutio adhimu cha utalii. Jiwe hili lilianza kutumiwa na babu zake Chifu Mtwa Mkwawa kwa ajili ya kufanya matambiko.

Mwanahistoria Zuberi Witala, anasema historia ya jiwe hilo inaonyesha kuwa Chifu Kayila, ambaye ni babu yake Chifu Mkwawa ndiye alianza kulitumia kwa kufanya matambiko.

Mwanahistoria Zuberi Witala akiwa amesimama juu ya jiwe la Gangilonga akitoa historia ya jiwe hilo.

Kwamba mizimu ya Chifu Kayila, iliishi ndani ya jiwe hilo naye alifika mahali hapo kuzungumza nayo kuhusu mwenendo wa hali ya himaya yake na hasa likimpa taarifa za uwepo wa mvua au ukame.

Chifu Kayila alilitumia pia jiwe hilo kumpa taarifa za kiusalama katika himaya yake; kama kuna maadui watavamia hasa wezi wa mifugo na watavamia kutoka upande gani.

Baada ya kufa kwa Chifu Kayila na mwanaye Chifu Mnyigumba kurithi mikoba yake, naye alilitumia jiwe hilo kama alivyokuwa akilitumia baba yake.

Njia ya uchochoro iliyo katikati ya miamba mikubwa inayotumika kupanda kwenye jiwe la Gangilonga.

Sehemu ya juu kabisa ya jiwe la Gangilonga.

Chifu Mkwawa naye, akiwa Chifu wa Himaya ya Uhehe, jiwe hilo ndilo lililomsaidia kujua hali ya usalama na kama kuna matukio yoyote yatakayotokea.

Zuberi anasema jiwe la Gangilonga lilipoteza uwezo wake wa kuongea baada ya kuanguka kwa utawala wa Chifu Mkwawa, ambapo mzimu uliokuwa ndani ya jiwe hilo uliondoka.

Anasema wakati mzimu huo ukitoka ndani ya jiwe hilo, kulisikika sauti za ajabu kutoka kwenye jiwe sambamba na Mlima Chamtinde. Mlima mkubwa ulio nje ya Mji wa Iringa.

Sehemu iliyotumiwa kupumzika na kujiandaa kabla ya kusimama juu na jiwe na Gangilonga kuzungumza nalo.

Mlima Chamtinde unaoonekana kwa mbali mbele ya Mji wa Iringa.

Akinukuu simulizi za watu wa kale wa Uhehe, anasema mzimu uliokuwa ndani ya jiwe la Gangilonga uliitwa Kamselela na wakati unatoka kwenye jiwe hilo ulikuwa ukitamka maneno  makali, kumaanisha kuwa ulikuwa na hasira.

Zuberi anasema mzimu Kamselela ulionyesha hasira zake za wazi kwa baadhi ya Wahehe kumsaliti Chifu Mkwawa katika vita yake na wakoloni wa Kijerumani. Ananukuu maneno yaliyosemwa na mzimu huo kuwa, “Iringa italala kwa usaliti uliofanywa na baadhi ya Wahehe kwa Chifu Mkwawa.”

Wakati mzimu huo ukimtaka maneno hayo kwa hasira,  sauti ya mzimu mwingine ilisikika ikitamka maneno ya kuusihi mzimu Kamselela usiwaache watoto wa Iringa yatima, bali ujichanganye nao kwa sababu Chifu wao amekwishajiua msituni hivyo wakibaki peke yao watakosa pa kukimbilia, watachanganyikiwa.

Mzimu Kamselela ulitoka kwenye jiwe la Gangilonga na kuelekea Mlima Chamtinde, ambako uliendelea kutamka maneno ya hasira huku ngoma zikisikika kupigwa kwenye mlima huo.

Baadhi ya wazee walitoka kuelekea Mlima Chamtinde  ilikokuwa ikisika sauti na ngoma zikipigwa. Wazee waliokwennda kwenye mlima huo walipotea kwa muda wa siku tatu na waliporejea, pamoja na mambo mengine walisema walikuwa wanakula vyakula vya ajabu walivyopewa na mzimu.

Mji wa Iringa unavyoonekana kutoka juu ya jiwe la Gangilonga.

Aidha, walieleza kuwa kila walivyokuwa wakiikaribia sauti na milio ya ngoma, nayo ilizidi kutokomea mbali zaidi ndani ya misitu ya mlima huo.

Witala anaeleza kuwa ngoma zilizopigwa wakati mzimu Kamselela ukitoka kwenye jiwe la Gangilonga, ziliendelea kusikika kwa miaka mingi baadaye na hata wakati wao, akiwa kijana walisikia midundo ya ngoma hizo.

Anasema ngoma hizo zilisikika zaidi wakati wa usiku wa manane na simulizi waliyopewa na wazazi wao kuhusu milio ya ngoma hizo kwenye Mlima Chamtinde ni kwamba wakati wa uhai wa Chifu Mkwawa, alikwenda kwenye pango lililo chini ya mlima huo kudhibiti nungunungu waliokuwa na makazi ndani ya pango hilo; ambao walikuwa wakisumbua watu wa eneo hilo.   

JIWE HILI LIPO, TEMBELEA IRINGA UKALISHUHUDIE.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya