
MAKUMBUSHO ya Chifu Mtwa Mkwawa wa Kabila la Wahehe, iliyopo Kitongoji cha Wanji, Kijiji cha Kalenga, Kata ya Kalenga mkoani Iringa ina vivutio vingi vinavyoweza kumfanya mtalii kuiona picha ya maisha ya mashujaa wa Afrika wa miaka ya 1800, katika hisia zake.
Makumbusho hiyo, imehifadhi historia binafsi ya maisha ya ukoo wa Chifu Mkwawa, historia ya Himaya ya Wahehe, vita vilivyopiganwa na Wahehe dhidi ya himaya za kichifu za makabila mengine ya Tanzania na zana za kivita zilizotumiwa na wapiganaji wa Kihehe.
Pia kuna Gobole alilotumia Chifu Mkwawa kujiua yeye mwenyewe na mlinzi wake, barua ya Chifu Mkwawa ya kutaka wakoloni wa Kijerumni wasitishe vita dhidi yake ili apambane na majeshi ya machifu waliomsaliti pamoja na mambo mengine mengi.
Makala haya yanakupitisha kwenye baadhi ya vivutio vya kuvutia na kusisimua vilivyopo kwenye Makumbusho ya Chifu Mtwa Mkwawa.
GOBOLE LA SULTANI ABUSHIRI ALILOTUMIA CHIFU MKWAWA KUJIUA

Gobole la Chifu Abushiri wa Pangani ambalo Chifu Mtwa Mtwawa alilitumia kujiua katika Kijiji dha Mlambalasi mwaka 1898. Chifu Mkwawa alichukua Gobole hili kutoka kwa Sultani Abushiri wakifanya biashara ya kubadilishana bidhaa.
Mtalii anayetembelea Makumbusho ya Chifu Mkwawa ataona Gobole lenye zaidi ya miaka 200 lakini bado lina hali nzuri.
Gobole hilo, awali lilimilikiwa na Sultani wa Pangani, Abushiri ambaye alikuwa akifanya biashara ya kubadilishana bidhaa na Chifu Mkwawa.
Bidhaa walizobadilishana ni Pembe za Ndovu na ngozi za wanyama ambazo Chifu Mkwawa alizitoa Ruaha na Sultani Abushiri alimpatia Chifu Mkwawa shanga, mavazi na silaha.
Chifu Mkwawa alichukua Gobole kutoka kwa Sultani Abushiri wakati wa biashara zao na yeye akatengeneza Gobole lake akiigiza alilopewa na Sultani Abushiri.

Gobole lililotengenezwa na Chifu Mtwa Mkwawa akiigiza alilopewa na Sultani Abushiri.
Mwaka 1898, Chifu Mkwawa akiwa msituni katika Kijiji cha Mlambalasi, alilitumia Gobole alilopewa na Sultani Abushiri kujiua yeye mwenyewe na mlinzi wake baada ya kubaini hataweza tena kupambana na kuwashinda wakoloni wa Kijerumani waliokuwa wamevamia Himaya yake ya Uhehe.
MABAKI YA MABOMU YA WAJERUMANI YALIYOVUNJA NGOME YA LIPULI

Mabaki ya mabomu ya Wajerumani.
Mabaki ya mabomu na risasi vilivyotumiwa na wakoloni wa Kijerumani kushambulia na kuivunja ngome imara ya Lipuli iliyojengwa na Chifu Mkwawa kwa miaka minne, yamo ndani ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa.
Wajerumani walitumia risasi na mabomu kwenye vita ya pili baina yao na Chifu Mkwawa na wanajeshi wake. Hiyo ilikuwa baada ya Chifu Mkwawa kupigana na kuwashinda Wajerumani katika vita ya kwanza ya mwaka 1891.
Katika vita hiyo ya pili iliyopiganwa mwaka 1894, wakoloni wa Kijerumani, wakisaidiwa na wapiganaji wa himaya za kichifu zilizopata kupigana na Himaya ya Uhehe iliyoongozwa na Chifu Mkwawa na kupingwa, walivamia ngome ya Chifu Mkwawa wakitokea milima ya Tosa.
MIKUKI YA WANAJESHI WANAFUNZI WA CHIFU MKWAWA.

Mikuki ya wanajeshi wanafunzi.
Kuna mikuki ya mbao ambayo askari wanafunzi wa Chifu Mkwawa waliitumia kwenye mafunzo. Ilitengezwa kwa miti imara na wapiganaji wanafunzi waliitumia katika mazoezi ya kukabiliana ana kwa ana na adui badala ya mikuki ya chuma ili wasidhurike.
MKUKI MCHOME NA MKUKI MCHOME MPAKA AFE

Mkuki mchome na mkuki mchome mpaka afe.
Ndani ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa imo mikuki yenye ncha ya chuma iliyotumiwa na wapiganaji wa Kihehe vitani pamoja na ngao.
Mikuki hii ni ya aina mbili, wa kwanza ni mrefu ambao ulitumika kumshambulia adui kwa kumrushia. Mkuki huu unaitwa Mchome.
Mkuki wa pili ni mfupi ambao ulitumika kumshambulia adui kwa karibu. Huu ulikuwa wa kumalizia kazi baada ya adui kurushiwa mkuki mrefu ukamchoma, mpiganaji alikwenda kummaliza adui kwa karibu kwa kumchoma na mkuki huu. Mkuu huo unaitwa Mchome Mpaka Afe.
BARUA YA KIVITA ILIYOANDIKWA KWA LUGHA YA KIARABU NA CHIFU MKWAWA

Barua ya kivita ya Chifu Mtwa Mkwawa
Barua ya Chifu Mkwawa aliyoiandika kwa Lugha ya Kiarabu mwaka 1894, kwenda kwa mwakilishi wa Umoja Mataifa, aliyetumwa kuja Tanganyika kuangalia mwenendo wa wakoloni wa Kijerumani dhidi ya babu zetu. Barua hiyo ipo ndani ya makumbusho hii.
Chifu Mkwawa aliandika barua hiyo akitaka wakoloni wa Kijerumani wasitishe vita dhidi yake ili apambane kwanza na majeshi ya machifu waliokuwa wakimsaliti; na akishamaliza nao ndiyo vita yake na Wajerumani iendelee.
Chifu Mkwawa alitaka apambane kwanza na Chifu Kiwanga wa Njombe, Chifu Begele wa Morogoro na Chifu Chabruma wa Ruvuma ambao walikuwa wakiwasaidia Wajerumani kupambana naye.
MEDALI YA CHIFU ADAMU SAPI MKWAWA

Medali ya Chifu Adam Sapia Mkwawa.
Chifu Adam Sapi Mkwawa ambaye alikuwa Spika wa Kwanza wa Bunge la Tanganyika ni mjukuu wa Chifu Mkwawa.
Adamu Sapi alipigana vita bega kwa bega na majeshi ya Uingereza nchini Ethiopia dhidi ya majeshi ya Ujerumani. Alikuwa mpiganaji hodari na baada ya vita kuisha na majeshi ya Uingereza kuyashinda ya Ujerumani, alitunikiwa Nishani. Nishani hiyo imo ndani ya Makumbusho ya Chifu Mkwawa.
BOKSI LILILOHIFADHI FUVU LA KICHWA CHA CHIFU MKWAWA UJERUMANI

Boksi lililohifadhi fuvu la kichwa cha Chifu Mtwa Mkwawa nchini Ujerumani.
Chifu Mkwawa baada ya kujiua kwenye msitu wa Mlambalasi, Wajerumani walitaka kujua alikuwa na ubongo wa aina gani kutokana na mbinu za kivita alizokuwa nazo.
Ilitolewa amri kutoka Ujerumani kuwa kichwa chake kikatwe kipelekwe Ujerumani kwa ajili ya kuchunguza uwezo wa ubongo wake kwa sababu haikupata kufikiriwa kuwa Mwafrika anaweza kuongoza wapiganaji wake kupambana na wanajeshi wa Kijerumani na kuangamiza jeshi lao lote.
Mwaka 1891, Chifu Mkwawa aliwaongoza wapiganaji wake kupigana na Wajerumani na kuua kikosi kizima cha wanajeshi zaidi ya 300, akiwemo kamanda wao. Vita hiyo ilipiganwa eneo la Lugalo, Iringa.
Baada ya uchunguzi wao, fuvu la kichwa chake walilihifadhi kwenye boksi maalumu huko Ujerumani. Boksi hilo lipo kwenye makumbusho ya Chifu Mkwawa.
BOKSI LA SHABA LILILOTUMIKA KUSAFIRISHA FUVU LA KICHWA CHA CHIFU MKWAWA KUTOKA UJERUMANI HADI TANGANYIKA

Boksi la Shaba lililotumika kusafirisha fuvu la kichwa cha Chifu Mtwa Mkwawa.
Mbali na boksi lililohifadhi fuvu la kichwa cha Chifu Mkwawa huko Ujerumani, pia lipo boski la shaba lililotumika kusafirirsha fuvu hilo kutoka Ujerumani kuja hapa nchini.
NGOMA YA CHIFU MKWAWA ILIYOTENGENEZWA KWA NGOZI YA CHATU

Ngoma ya Chifu Mkwawa
Machifu walikuwa na ngoma zao. Ngoma za machifu zilikuwa zinatengenezwa kwa ngozi ya nyoka aina ya chatu. Chifu Mkwawa alikuwa na ngoma aliyokuwa akiipiga kijiburudisha, ngoma hiyo alipewa na rafiki yake, Chifu Mazengo wa Dodoma. Ipo ndani ya makumbusho yake.
Chifu Mazengo alimpa pia Chifu Mkwawa zawadi ya wanawake vigoli wawili, hivyo kati wake 62 wa Chifu Mkwawa, wawili walitokea Dodoma.
MJELEDI WA CHIFU MKWAWA ULIOTENGENEZWA KWA NGOZI YA KIBOKO

Ngozi ya Kiboko
Chifu Mkwawa hakuwa mtu wa mchezo mchezo. Alikuwa akitoa adhabu kali kwa wakosaji na moja ya adhabu alizotoa ni viboko. Alikuwa na mjeledi maalumu uliotengenezwa kwa ngozi ya Kiboko. Mjeledi huo upo ndani ya makumbusho yake.
KITI CHA CHIFU MKWAWA

Kiti cha Chifu Mtwa Mkwawa.
Chifu Mkwawa alikuwa na kiti chake maalumu cha kiutawala, kiti hicho kilitengenezwa kikiwa na miguu mitatu na kila mguu ulikuwa na maana yake. Mguu wa kwanza ulimaanisha akili, wa pili kilimo na wa tatu nguvu.
FUVU LA KICHWA CHA CHIFU MKWAWA

Ramani ya Ngome ya Chifu Mtwa Mkwawa.
Fuvu la kichwa cha Chifu Mkwawa ambalo lilipigwa risasi mbili, moja aliyojipiga yeye mwenyewe akajiua na ya pili aliyopigwa na wanajeshi wa Kijerumani waliomkuta ameishajiua lakini kwa sababu walikuwa wakimuogopa, walijawa na hofu wakidhani kwamba bado ni mzima anaweza kusimama akawaangamiza, hivyo walimpiga risasi nyingine kichwani kuthibitisha kuwa kweli amejiua. Fuvu lake hilo lipo kwenye Makumbusho yake.
JENGO LA MAHAKAMA YA MWANZO

Jengo la Mahakama ya Mwanzo.
Wakoloni wa Kiingereza walijenga uhusiano mwema na machifu ili wawawezesha kuishi kwa usalama. Kufanikissha hilo walisaidia kuimarisha mifumo yao wa utawala. Jengo hilo ni Mahakama ya Mwanzo iliyojengwa na wakoloni wa Kiingereza.
NYUMBA YA VIJAKAZI WA CHIFU MKWAWA
Vijakazi wa machifu nao walikumbukwa. Hiyo ni nyumba ya vijakazi wa Chifu iliyojengwa na wakoloni wa Kiingereza.
CHOO
Ni wakati huo wa wakoloni wa Kiingereza ndiyo ustaarabu ulianza kuota mizizi Afrika. Utaratibu wa kujistili vichakani uliwekwa kando. Hapo juu ni choo cha vijakazi wa Chifu kilichojengwa na wakoloni wa Kiingereza.
NYUMBA YA CHIFU ADAM SAPI MKWAWA

Iliyokuwa nyumba ya Chifu.
Hii ni nyumba ambayo wakoloni wa Kingereza waliijenga kwa ajili ya Chifu wa Kabila la Wahehe. Nyumba hii ilipata kutumiwa na Chifu Adamu Sapi Mkwawa. Tembelea Makumbusho ya Chifu Mkwawa ukaone iliposhi Adamu Sapi Mkwawa kabla ya kuwa Spika.
MTI WA MSOSA

Mti wa Msosa.
Unaitwa Mti wa Msosa kwa Lugha ya Kihehe. Chifu Mkwawa alikuwa akifanyia matambiko yake kwenye mti huo. Sasa una zaidi ya miaka 200 lakini haujawahi kunyauka, iwe jua au mvua majani yake yamechipua ukijani.
Bado unatumiwa na ukoo wa Chifu Mkwawa na watu wa kabila la Wahehe kufanya matambiko.
Unaitwa mti wa Msosa kwa sababu juu una umbo linalofanana na Sahani. Umbo hilo kwa Wahehe linamaanisha kupokea, wanaamini ni mti unaopokea. Wahehe hufanya matambiko yao hapo wakiamini kuwa mizimi yao ipo ndani ya mti huo na kwa umbo lake kama sahani juu, mizimu iliyo ndani ya mti huo hupokea maombi yao.
NYOKA MWENYE VICHWA 12, KIMOJA CHA KUKU

Ndani ya mti huu wa Msosa panaaminika kuna nyoka mwenye vichwa 12, kimoja kinafanana na cha Kuku (jogoo), kuna nyuki wa mizimu na huwa unawaka moto wakati wa usiku.
Ndani ya mti wa Msosa inasadikika kuna nyoka mkubwa sana mwenye vichwa 12; kichwa kimoja kina umbo la kichwa cha kuku (jogoo).
Nyoka huyo akifurahi huwa anawika kama jogoo na akichukia huwa analia kwa sauti ya kutisha ambayo wazee wa kimila wanajua kutafasili maana ya mlio huo.
Nyoka aliye ndani ya mti huu huwa haonekani kwa macho ya kawaida isipokuwa kwa akina mama waliovaa mavazi meusi na wanaume waliovaa mavazi meupe.
NYUKI WA MIZIMU
Pia kuna nyuki. Nyuki na nyoka ni mizimu ya kabila la Wahehe.
Majani ya mti wa Msosa ni dawa ya magonjwa mbalimbali na mtu yoyote anaruhusiwa kuyachuma na kuyatumia kwa kadri ya imani yake.
Juu ya mti wa Msosa kuna miti mingine miwili ya aina tofauti iliyoota kutoka kwenye matawi ya mti huo. Mmoja unaitwa Mlangale na mti mwingine ulioota juu ya Msosa unaitwa pogoli.
MTI UNAOWAKA MOTO

Miti mingine miwili iliyoota ndani ya mti wa Msosa inavyoonekana juu.
Inasadikika kuwa mti wa Msosa huwa unawaka moto usiku na pia huwa unahama kutoka sehemu moja hadi nyingine.
HIVI NI VIONJO TU VYA MAMBO YALIYO NDANI YA MAKUMBUSHO YA CHIFU MKWAWA, TEMBELEA MAKUMBUSHO HIYO UFAHAMU MENGI ZAIDI.