Thursday, September 11, 2025
spot_img

ANAYEDAIWA KUJIPATIA MALI ZA MAREHEMU KWA ULAGHAI APAMBANA

 NA MWANDISHI WA PANORAMA

SAKATA la kujipatia mali kwa njia ya ulaghai linalomuandama mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Dali Yusuph Musa sasa limeanza kuibua maswali mengi yenye utata baada ya mfanyabiashara huyo kufanya mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog na kueleza kuwa yupo tayari kwa mapambano ambayo yatamuweka huru.

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika jana eneo la Magomeni Moroko, Dali alisema tuhuma na shutuma anazoelekezewa na baadhi ya ndugu zake kuwa amejimilikisha mali zinazohamishika na zisizohamishika za marehemu Yusuph Dali aliyefariki mwaka 2019 nchini Italia zina lengo la kumpoka haki yake ya urithi aliyopewa na marehemu baba yake kabla ya kukutwa na umauti.

Alisema amekuwa akipambana kimya kimya na wanaotaka kumpoka haki yake ya urithi katika mahakama na kwenye mabaraza ya dini ambako kote alishinda lakini anazidi kuandamwa hivyo sasa yupo tayari kusimama hadharani kupambana ili hatimaye aishi kwa amani.

Miongoni mwa mambo aliyoyatolea ufafanuzi ni tofauti ya majina yake yanayoonekana katika cheti chake za kuzaliwa, cheti cha kumaliza elimu ya msingi na kile cha kumaliza kidato cha nne ambapo kwa maneno yake mwenyewe alisema; “Jina langu halisi ni Dali Yusuph, hilo Darlington ni a.k.a yangu wakati nasoma, nadhani na wewe unafahamu kwamba unapokua, unakuwa na a.k.a. Ndiyo maana hata leo ukiingia facebook, ni mtandao wa zamani nimesajili facebook nadhani ‘form two’ nikitumia Dali Yusuph Mussa.

“Dali Mwasubila ni jina ambalo nilikuwa nikilitumia wakati nasoma shule ya msingi, wakati huo sijamtambua baba yangu mzazi ni nani, nadhani hiyo ‘point’ hapo umeilewa.

“Baada ya kufika la saba baba yangu alijitokeza kwamba mwanangu kutokana na yote yaliyopita, mimi nilikuwa niko nje katika harakati ya kutafuta. Mawasiliano yako nilikuwa sina na hata ambao nilikuwa nikiwatuma waje kwako walikuwa hawafiki.

“Kwa njia ya simu alikuja baba yangu mdogo, anaitwa Issa Zawayai ambaye yeye na baba yangu, yeye amezaliwa na mwanaume baba amezaliwa na mwanamke ndiyo kunipa simu, siku ya kwanza kusikia sauti ya mzee wangu.

Sehemu ya Jiji Rome Italia



“Ndiyo kuanza hapo nikakata kitambulisho changu cha uraia mpaka kitambulisho changu cha kura vyote vinasoma Dali Yusuph Musa.

“Na mpaka mzee kabla hajafa wakati wa uhai wake kwa sababu kuna vitu walikuwa wanasimamia watu, akaamuru kupitia ‘power of attorney’ ambayo nimeisajili enzi za uhai wake kwamba Dali mwanangu naomba usimamie vitu vyote na uviendeshe wewe ila huna ruhusa ya kuviuza ila viendeshe kama mtoto wangu wa pekee.

“Ameainisha mle na mpaka ‘power of attorney’ nimeisajili, ninayo na nililipia ardhi kwa hiyo hata ‘copy’ mkitaka na nyie kama kumbukumbu au moja ya vielelezo ninawapa.

“Mbeya shuleni nilikuwa natumia kama nilivyokwambia awali, nilikuwa nakaa na baba mlezi ambaye alinilea vizuri tu kama baba yangu kwa hiyo sikuweza kuona shaka yoyote kwa sababu malezi aliyonipa kama wenzangu na nilikuwa katika familia yenye furaha.

“Lakini nikiwa ninasoma na kwa sababu mimi ni mtoto sijui chochote, nilitumia jina la Dali Mwasubila Simon.

“Kwenye cheti sasa hapo sasa, kwenye cheti linasoma Dali Yusuph Mussa baada ya mimi kukua sasa, cheti cha darasa la saba kinasoma Dali Yusuph Mussa…” alisema Dali kabla ya kukatishwa na mdogo wake aliyemweleza kuwa cheti chake cha kumaliza darasa la saba kimeandikwa jina la Dali Mwasubila Simon.

Alisema alizaliwa Mkoa wa Mbeya na kuanza elimu ya msingi huko kabla ya kuhamishiwa Mkoa wa Dar es Salaam kwa amri ya baba yake aliyekuwa akiishi Italia, aliyetaka aje afahamiane na ndugu zake pamoja na kufahamu mali zake.

Dali alisema baada ya kuhamia Dar es Salaam alibadilisha jina la ubini wake na kuanza kutumia la Yusuph Musa badala la Mwasubila Simon lakini hakueleza alipokelewaje shuleni kwa jina tofauti na lile alihitimu nalo elimu ya msingi.

“Nilikuwa nikiishi kule kule, baada ya kumaliza elemu ya msingi, nilianza shule moja inaitwa Southern Highland, nilisoma pale kwa jina la Dali Yusuph Mussa kuanzia ‘form one.’

“Baada ya hapo tena mzee akasema natakiwa nije Dar es Salaam kwa sababu nijue vitu vilipo na ndugu zangu wapo wapi kwa hiyo nikahama shule ile nikahamia Kibaha, nikahamia shule moja inaitwa Philibert Bayi, nikaanza tena upya ‘form one’ kwa sababu ‘syllabus’ za kule zilikuwa tofauti, za kiingereza ambazo wanasoma wengine lakini kufika huku nakakutana na syllabus ya Kenya kwa hiyo nikashindwa ‘kucop’ na wenzangu, ikabidi nianzae upya ‘form one’

‘Baadaye nikahama shule nikaenda kusoma shule moja inaitwa St George ipo Kongowe, huko ndiko nikamaliza mpaka ‘form four,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu mwenendo wa maisha yake baada ya kumaliza elimu ya msingi alisema, “Baada ya hapo sasa maisha yangu yakawa na vitendawili kwa sababu gani? mamlaka baba alikuwa ameshawapa watu ya kusimamia vitu umenieleawa? kulikuwa kuna magari, kulikuwa na godown, unaona ee, kulikuwa kuna nyumba, ambazo ndugu walikuwa wamejigawia wao kama wao sasa mimi wakati ule nikawa nimetengenezewa kundi la kuwa, la kuonekana ni adui kwenye familia kwa hiyo nikawa naundiwa tume tofauti tofauti.

“Ukienda kwa baba mdogo anazungumza na yule mwenzie, ukienda kwa huyu anazungumza na mwenzie kwa hiyo ni mtoto ambaye nimetengezewa vikundi ambavyo havina usalama kwangu kwa sababu ni mtoto wa pekee kwanza zingatia, umeona.

“Kwa hiyo sasa nikawa ni mtoto ambaye ninaishi kwa shida, baadaye nikwambia mzee, baba akapiga simu ya kufoka, moja, mbili, tano, nikamwambia hapana mzee hilo unalosema halipo mimi naomba nirudishe ulikonitoa Mbeya. Baba akagoma, akasema hapana kama maisha ya kukaa kwa watu umeshindwa basi ngoja nikutafutie nyumba, kweli akachukua jukumu la kunitafutia nyumba ambayo ilikuwa Magomeni.

Magomeni



“Na hapo wakati nimefika magomeni nimetoka likizo kukaa pale kulikuwa kuna watu tena wakiishi pale, ni watu tu baki ambao yeye nadhani walikuwa na uhusiano mzuri na mzee mmoja marehemu kwa sasa Mwenyezi Mungu amrehemu, alikuwa anaitwa Sheikh Abilahi, ndiyo alifanya manunuzi ya nyumba hiyo pamoja na mtoto wake anaitwa Mabruki.

“Kwa hiyo kukatokea mzozo ambao yule akataka mimi, Mabruki ambaye alikuwa akiishi pale akataka mimi aniwekee ‘defence’ kwamba ionekana tu nitoke pale ili yeye awe huru nikamwambia mimi kule ninakokaa nataabika ndiyo maana mze amesema nije nikae hapa na hapa naomba wewe unipishe ili nipangishe ili niweze kukimu maisha yangu. Sijui unanielewa vizuri mzee wangu.

“Basi kutokana na hayo nikawa ni mtu ambaye sasa nimefanikiwa, nimepata pa kuishi lakini shule tena hapo nimerudishwa ada sina uwezo wa kusoma, ndugu wana mali, nikajaribu kuwashirikisha, bwana nahitaji pesa. Mimi mwenyewe mtihani nimeende kufanya tayari nadaiwa, tayari nimefukuzwa ada. walimu tu kwa huruma kwamba huyu mtoto inabidi amalize tu mtihani,” alisema Dali.

Alipoulizwa ilikuwaje akakwama kulipa ada wakati baba yake alimtoa Mbeya na kumtafutia shule Dar es Salaam alisema; “Baba yuko Italia, sasa hapo ana matatizo lakini nilikuwa sipewi taarifa kamili, wengine wananiambia anaumwa kwa hiyo nikawa ni mtu ambaye nimechanganyikiwa ambaye sina msaada.

“Na wale ndugu vile ambavyo walikuwa wamevikumbatia, kwa maslahi yao wao kwa hiyo mimi nilikuwa nimetengezewa mazingira ya kuwa mtoto wa mtaani umenielewa? kuwa mtoto ambaye sisikii lakini kwa makusudi ya Mwenyezi Mungu, wao walivyopanga iwe na Mungu hakutaka iwe hivyo kwa sababu ndiyo ikawa imenisimamisha mpake leo unaniona hivi ambapo nina kampuni ambayo ninaiendesha mimi na mdogo wangu kutokana na mapito niliyopitia.

“Kwa hiyo sikuwa na furaha kule, nilikokuwa kulikuwa kuna amani na furaha kwa baba mlezi siyo kwa baba mzazi. Hiyo ndiyo ‘short story’ kutokana na maisha niliyopitia baada ya kumjua mzazi wangu kwa hiyo huku kulikuwa kuna maisha magumu. Baba mlezi alinisomesha ‘international,’ shule ya gharama na bila kubaguliwa kwa chochote wala bila kuishi tofauti

“Lakini nilipokuja kwa babaangu ndiyo nikakutana na shida nyingi, chuki kwa sababu watu wengi hawakuwa na kazi za kujishughulisha, alizowea kuwasidia, kuwasomeshea watoto, kwa hiyo baada ya kuja mimi ikajengwa chuki kubwa kwa hiyo nikawa ni mtoto ambaye sitakiwi kwa sababu tu ya mali lakini mimi nilikuwa tayari kuishi na ndugu zangu wote kwa sababu ndiyo ndugu zangu nitafanyaje.

“Ndiyo maana baba akachukua hatua ya kuniandikia ile ‘power of attorney kwamba wewe leo mimi nipo kesho mimi sipo utataabika hao siyo watu wazuri kwa sababu mimi wakati mwingine nakubali kuongea nao maneno ili nijue mtoto wangu wanakuweka kwenye ‘position’ gani.

“Ndiyo akaniandikia ile ‘power of attorney ya kwanza nikaipeleka ardhi ikadunda wakasema haijajiridhisha. Ikaja ya pili ambayo ilikuwa na picha yangu na ya kwake tukazibana ndiyo ardhi wakaipokea na penyewe bado mimi baba nikamgusia, ukisema kutangulia ni kazi ya Mungu naweza nikaanza hata mimi ukifanya hivyo unakuwa unakufuru Mungu.

“Lakini sikujua nini Mungu mzee wangu alimuonyesha mbele, sikujua alikiona nini mbele yake kwamba alijua anataka kufariki, sikujua kwa sababu baada ya mwezi akafariki… baba yangu alikuwa daktari, anatibu watu wakubwa tu kule, sasa kuna mtu alimtibu akafa kwa hiyo akafungwa mpaka alipokufa,” alisema.

ITAENDELEA

 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya