Wednesday, March 12, 2025
spot_img

AFRIKA YAIPA KIPAUMBELE NISHATI SAFI

TERESIA MHAGAMA

BARA la Afrika lina mchango mdogo katika uchafuzi wa hali hewa duniani lakini liko mstari wa mbele kutekeleza ajenda ya mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipokuwa akifungua mkutano wa awali kuelekea kongamano na maonesho ya petroli ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) unaoanza leo, Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo wa awali ulilenga kujadili mipango na mikakati itakayowezesha matumizi ya nishati safi katika maeneo mbalimbali.

Dkt. Biteko alisema Bara la Afrika linatekeleza ajenda ya mabadiliko ya tabianchi kwa kuijumuisha katika mifumo yake ya kisheria na udhibiti, likihakikisha linahama kwenye matumizi ya nishati chafu ili kuiepusha dunia na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika hotuba yake hiyo ya ufunguzi, Dkt. Biteko alisema mkutano wa EAPCE’25 ni jukwaa muhimu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wadau wengine kujadili mipango na mikakati ya matumizi ya nishati safi, ikizingatiwa kuwa dunia inapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazochangiwa na shughuli za binadamu.

Alisema tafiti za kisayansi zinaonesha viwango vya utoaji wa hewa ya ukaa vimeongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya mapinduzi ya viwanda duniani.

“Nataka nichukue nafasi hii kuwaomba wote muutumie mkutano huu kujadili masuala ambayo yatatufanya Afrika Mashariki tuhame kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyokuwa safi kwenda kwenye matumizi ya nishati safi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati) akiimba wimbo wa Taifa wakati wa mkutano wa awali kuelekea Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) linaloanza rasmi leoJijini Dar es
Salaam. Mkutano huo wa awali ulilenga kujadili mipango na mikakati itakayowezesha matumizi ya nishati safi. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga na kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

“Ni muhimu mtambue mkutano huu wa awali haujatokea kwa bahati mbaya. Kama jamii tunayo kazi ya kufanya kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi kwenda matumizi ya nishati safi,” alisema Dkt. Biteko.

Alisema sheria nyingi zinazopitishwa sasa barani Afrika zinahimiza uchumi wa kijani, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuwa na maendeleo endelevu na EAC imeandaa sera ya mabadiliko ya tabianchi.

Alitaja baadhi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kuwa ni ukame mkali, mafuriko, kupotea kwa viumbe hai, kupungua kwa vyanzo vya maji safi, kuyeyuka kwa barafu na ongezeko la magonjwa yanayohusiana na tabianchi.

“Mabadiliko ya tabia nchi yanatiliwa
mkazo pia katika ngazi ya dunia ndiyo maana kuna mikataba mbalimbali ya kimataifa ukiwemo wa Kyoto, Montreal na Paris ambapo nchi zilizoendelea na zinazoendelea zinaandaa na kutekeleza mikakati inayohusiana na tabianchi ikiwemo kujikita katika matumizi ya nishati safi,” alisema.

 Akizungumzia upatikanaji umeme, alisema Afrika ndiyo bara linalokabiliwa na upungufu mkubwa wa nishati duniani likiwa na asilimia 75 ya watu wanaokosa nishati hiyo.

Alisema Afrika inafanya juhudi za kuwa na nishati ya umeme wa uhakika na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati uliofanyika Tanzania mwezi Januari mwaka huu, uliweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.

“Mabadiliko yanahitajika ili kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi. Kwa Tanzania, takribani asilimia 81 ya kaya zinatumia kuni na mkaa kama vyanzo vikuu vya nishati ya kupikia na kusababisha takribani hekta 469,420 za misitu kufyekwa kila mwaka.

 “Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amechukua hatua madhubuti za kutekeleza mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia (2024–2034) ambao unalenga asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” alisema Dkt. Biteko.

Aidha, alisema matumizi ya gesi asilia kama nishati ya kuendeshea vyombo vya usafiri ni muhimu na Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira kwa wawekezaji binafsi kushiriki katika ujenzi wa vituo vya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) pamoja na kuboresha sera na mifumo ya udhibiti.




Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya