RIPOTA PANORAMA
KAMPUNI ya Erolink Tanzania inadaiwa kuchota mabilioni ya shilingi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kwa njia za udanganyifu.
Inadaiwa, Kampuni ya Erolink yenye mkataba na Tanesco wa kuendesha kituo cha miito ya simu kilichopo Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam, ikishirikiana na baadhi ya waliowahi kuwa mameneja wa shirika hilo la umma, wametengeneza mtandao wa kudai malipo hewa ambayo yamekuwa yakiidhinishwa pasipo kuwa na nyaraka za kuyathibitisha.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Erolink Tanzania, Maximilian Tumaini (pichani hapo juu) amekanusha madai hayo akisema hayana ukweli hata kiasi cha chembe ya haradani kwani kampuni yake inafanya kazi kwa kufuata taratibu zote za kimkataba.
Taarifa zilizofikishwa Tanzania PANORAMA Blog na wafanyakazi wa Tanesco pamoja na nyaraka zilizoonwa zinaonyesha kuwa Kampuni ya Erolink ilipewa mkataba wa kuendesha kituo cha miito ya simu wenye thamani ya mamilioni ya shilingi yanayolipwa kila mwezi.
Kwamba kampuni hiyo ambayo inatakiwa kuwa na mawakala wasiopungua 100 ili iweze kutoa huduma inayotakikana kwa wateja wa Tanesco, tangu ilipoanza kusimamia kituo hicho imeshindwa kuwa na idadi hiyo ya mawakala jambo linalosababisha itoe huduma duni huku ikilipwa malipo yake kama ilivyo kwenye mkataba.
Aidha, Kampuni ya Erolink Tanzania inadaiwa kudai na kulipwa malipo ya kuikodishia Tanesco magari na madereva huku shirika hilo likiwa na madereva na magari mengi nchi nzima.
Inadaiwa, baadhi ya maafisa wa Tanesco wanaolipwa mshahara na Serikali pia wamekuwa wakilipwa mshahara mwingine kama watumishi wa Kampuni ya Erolink na baadhi ya malipo mengine yanayodaiwa na kampuni hiyo kwa Tanesco ni ya mawakala hewa.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko.
Kampuni ya Erolink Tanzania inadaiwa kuwa pamoja na kulipwa gharama zake zilizo kwenye mkataba kwa ajili ya kuendesha kituo cha miito ya simu ambazo zinahusisha malipo ya mawakala wake, imekuwa ikiidai Tanesco kulipa gharama za mawakala hao.
Inadaiwa zaidi kuwa Kampuni ya Erolink Tanzania iliongezewa mkataba wa kuendesha kituo cha miito ya simu kwa wateja na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma kwa Wateja (jina lake tunalihifadhi kwa muda kwa sababu hajapatikana kuzungumza) ambaye hana mamlaka ya kuiongeza mkataba jambo linaloashiria kuwepo kwa mchezo mchafu kati ya Erolink na kigogo huyo.
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta Meneja Mkuu wa Kampuni ya Erolink, Maximillian Tumaini na kumuuliza kuhusu madai hayo naye akijibu, alisema yote hayana ukweli.
Akijibu, Tumaini alisema hakuna udanganyifu wowote unaofanywa na kampuni yake kwani vituo vya huduma kwa wateja vinaendeshwa na mifumo hivyo chochote kinachofanyika kinarekodiwa na mifumo na ripoti zote zipo wazi kwa wadau husika.
Tumaini alisema malipo yote ambayo kampuni yake inalipwa na Tanesco yanafanyika kutokana na makubaliano yaliyo kwenye mkataba na kwamba malipo haramu ni yale yanayofanyika nje ya mkataba au makubaliano.
Kuhusu kampuni yake kutakiwa kuwa na mawakala wasiopungua 100, Tumaini alisema mkataba baina ya kampuni yake na Tanesco hauna kipengele hicho na kwamba Erolink wakati wote imetimiza matakwa ya kimkataba.
Akijibu kuhusu mkataba iliyoongezewa kampuni yake na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Huduma kwa Wateja kuwa na vipengele vyenye utata, Tumaini alisema hakuna kipengele chochote kwenye mkataba kinaweza kuongezwa au kupunguzwa bila kufuata taratibu za kisheria.
Akiendelea kujibu, Tumaini alisema madai kuwa kampuni yake inawalipa mawakala malipo kidogo tofauti na inavyoelekezwa kwenye mkataba hayana ukweli wowote kwani Erolink inafanya kazi kwa kufuata taratibu zote za kimkataba na hakuna kipengele hata kimoja kilichokiukwa.
Tumaini alijibu pia madai kuwa kampuni yake iliandikiwa barua ya aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja akiipa kazi Erolink kuikodishia Tanesco madereva. Alisema hakuna Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wateja aliyewahi kuandika barua ya kuipa kazi kampuni yake kuikodishia Tanesco madereva na alishangazwa na madai hayo akieleza kuwa hakuna uhusiano wowote baina ya Kurugenzi ya Huduma kwa Wateja na madereva.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko alipofanya ziara kwenye kituo cha miito ya simu cha Tanesco hivi karibun.i
Wakati Tumaini akikanusha kampuni yake ya Erolink kuandikiwa barua ya kupewa kazi ya kuikodishia Tanesco madereva, Tanzania PANORAMA Blog imeiona barua hiyo ambayo iliandikwa Desemba 6, 2022 ikiwa na kumbukumbu namba MD/DCEC/1/1 na kusainiwa na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi wa Huduma kwa Wateja kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.
Hivi karibuni, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko alifanya ziara kwenye kituo hicho na kueleza kutoridhishwa kwake na huduma kinazotoa.