Friday, March 14, 2025
spot_img

NYAMO-HANGA: HUDUMA TANESCO ZIMEZOROTA

RIPOTA PANORAMA

MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) Mhandisi Gissimo Nyamo-Hanga amesema huduma zinazotolewa na shirika hilo analoliongoza zimezorota.

Mhandisi Nyamo-Hanga amekiri kuzorota kwa huduma zinazotolewa na Tanesco kwenye waraka aliowaandikia wasaidizi wake kuwaelekeza kusimamia kikamilifu maeneo yao ya kazi.

Waraka huo ambao Tanzania PANORAMA Blog imeuona ukiwa na kumbukumbu namba UB.161/541/01/01 umeandikwa na kusaini na Mhandisi Nyamo-Hanga mwenyewe Februari 3, 2025 kwenda kwa Naibu Mkurugenzi Usambazaji Umeme, wakurugenzi wa kanda, mameneja wa mikoa na wilaya na maafisa huduma kwa wateja.

Katika waraka huo, Mhandisi Nyamo-Hanga ameeleza kuwa kumekuwa na malalamiko mbalimbali ya wateja nchi nzima kuhusu kuzorota kwa huduma zinazotolewa na Tanesco hasa kwenye utatuzi wa changamoto za hitilafu za dharura.

Kwamba malalamiko ya wateja yanahusu pia ucheleweshaji wa kuunganisha umeme kwa wateja wapya hali inayochangia ongezeko la simu nyingi kwenye kituo cha miito ya simu kilichopo Ubungo, Jijini Dar es Salaam.

“Maeneo ambayo yamekuwa yakisababisha wateja kutoa malalamiko hayo ni pamoja na vitendo visivyo vya uadilifu katika kutatua changamoto za wateja kama vile tatizo sugu la ufungwaji wa tiketi za wateja kabla ya kuwafikia kuwapa huduma wala kuwapigia simu,” inasomeka sehemu ya waraka huo wa Mhandisi Nyamo- Hanga.

Anataja sababu nyingine za kuzorota kwa huduma za shirika hilo kuwa ni kuunganisha tiketi zisizohusiana na tatizo moja hivyo kulazimisha wateja kupiga simu wakilalamika kufungwa kwa tiketi zao bila kupatiwa ufumbuzi.

Akiandika sababu zaidi za kuzorota kwa huduma Tenasco, Mhandisi Nyamo-Hanga anataja kufunga tiketi kwa mujibu wa taarifa zisizo sahihi hasa kwa matatizo yanayoripotiwa upande wa mita na kushikilia maombi ya upimaji ya wateja wapya bila kuwajulisha sababu ya kuchelewa kuwapimia hivyo kuendelea kulalamika kwa kupiga simu Tanesco.

Anataja pia kutokujaza kwa usahihi tatizo la mteja lililobainika na ufumbuzi wake, kuchelewa kuwasajili wateja wapya wanaofungiwa umeme kwenye mfumo hivyo kupiga simu mara kwa mara kuuliza jambo lilosababisha usumbufu na pia tiketi zinazohitaji ufumbuzi wa vitengo vingine kufungwa bila kupelekwa kwenye vitengo husika.

Katika waraka huo ambao Mhandisi Nyamo-Hanga ametoa maelekezo 11 ya kusimamiwa na wasaidizi wake ili kuboresha huduma za shirika hilo, anaeleza pia kuwa vitendo alivyovitaja vinachafua taswira nzuri ya shirika kwenye utoaji wa huduma na pia vinaongeza malalamiko ya wateja.

KESHO USIKOSE KUSOMA SKANDALI YA UFISADI WA KUTISHA KATIKA KITUO CHA MIITO YA SIMU CHA TANESCO.  

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya