MASHIRIKA YA HABARI YA KIMATAIFA
MUIGIZAJI filamu mashuhuri wa Uingereza, Idris Elba (52) (pichani hapo juu) anakusudia kuhamia Zanzibar ndani ya mitano hadi kumi ijayo.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Elba mwenye asili ya Afrika anakusudia kuhama Uingereza na kuweka makazi yake katika Visiwa Zanzibar, Ghana na Sierra Leone.
Elba ameliambia BBC kuwa ana mpango wa kujenga studio ya filamu ya kisasa katika Visiwa vya Zanzibar na Accra, Ghana.
Wazazi wa nyota huyo aliyezaliwa London, Uingereza ni waafrika, baba yake anatoka Sierra Leone na mama anatokea Ghana.
“Ninataka kutumia uwezo wangu kuunga mkono biashara ya filamu inayoendelea kukua barani Afrika. Nataka waafrika wasimulie hadithi zao wenyewe.
Muigizaji wa filamu wa Uingereza, Idris Elba akiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Ninafikiri na kwa hakika nitahama Uingereza katika kipindi cha miaka mitano au kumi ijayo Mungu akipenda. Nitaishi Zanzibar, Accra, Ghana na Freetown, Sierra Leone,” anasema Elba.
Anasema kukuza biashara ya filamu katika Bara la Afrika ni mchakato na hawezi kutimiza lengo lake hilo akiwa nje ya Bara la Afrika.
Elba anasema anaamini watazamaji wengi wa filamu duniani wanaijua miji ya Marekani na Ulaya bila kuitembelea kwa sababu filamu nyingi zinaziigizwa kwenye miji hiyo, hivyo miji mingi ya Afrika itafahamika duniani kwa kuigiza filamu ndani ya miji hiyo.
“Ukitazama filamu yoyote au kitu chochote kinachohusiana na Afrika utakachoona ni kiwewe, jinsi tulivyokuwa watumwa, jinsi tulivyotawaliwa na vita lakini ukifika Afrika unagundua kuwa siyo kweli, yapo mengine mengi.
“Kwa hiyo ni muhimu sana tuwe na hadithi zetu wenyewe juu ya mila, utamaduni, lugha, tofauti ya lugha moja na nyingine na desturi zetu. Ulimwengu haujui hayo,” anasema mwigizaji huyo.
Anasema amegundua uwepo wa vipaji vya uigizaji katika Bara la Afrika lakini kinachokosekana ni vifaa vya kisasa hivyo njia sahihi ni kushirikiana na Serikali za Afrika zilizo tayari kuunda mazingira wezeshi ya kuendeleza tasnia ya filamu.