RIPOTA MAALUMU
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko alitaka Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) kutekeleza kwa kasi miradi ya umeme itakayounganisha Mkoa wa Kigoma kwenye Grifi ya Taifa.
Agizo hilo amelitoa hivi karibuni mkoani Kigoma wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 132, kutoka Kijiji cha Igamba hadi Kijiji cha Kidahwe na kituo cha kusambaza umeme, msongo wa kV 400/200/132/33 cha Kidahwe.
Alisema Mkoa wa Kigoma unapaswa kuacha kutumia umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta mazito ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Dk. Biteko alisema Serikali inatumia Shilingi bil. 3.5 kila mwaka kununua mafuta mazito ya kuendesha jenereta za kuzalisha umeme wakati makusanyo ya Tanesco ni Shilingi bil. 16 na kusisitiza kuwa uzimaji jenereta zinazozalisha umeme kwa mafuta mazito itafanyika pia katika mikoa ambayo haijafikiwa na umeme wa Gridi ya Taifa.
“Kigoma inaingia kwenye historia ya kuwa na umeme wa Gridi ya Taifa. Itapata umeme kutoka Nyakanazi kwa msongo wa kV 400 na kV 220 na njia nyingine ni kutoka chanzo cha Malagarasi hadi kidahwe kutokea Mkoa wa Katavi kwa msongo wa kV 400 na la laini ya reli ya mwendo kasi (SGR) kutoka Dar es Salaam ya kV 220,” alisema Dk. Biteko.
Wakati huo huo, Dk, Biteko alitoa mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Kidahwe na aliahidi Serikali kujenga kituo kingine cha afya na katika Kijiji cha Igamba itajenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 20.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Felchesmi Mramba ambaye pia alikuwepo kwenye hafla hiyo alisema Mkoa wa Kigoma utaungwa kwenye Gridi ya Taifa kwa njia saba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Gissima Nyamo – Hanga alisema gharama za mradi huo ni Dola za Marekani milioni 144.14, ambazo ni sawa na Shilingi bil. 398 ambazo zimetolewa na Serikali na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
Alisema Serikali imetoa Dola za Marekani milioni 4.14 na AfDC imetoa Dola za Marekani 140 huku mkandarasi atayejenga bwana na kituo cha kuzalisha umeme akimtaja kuwa ni Kampuni ya Dongfang Electric Intenational Corporation ya China.
Mhandisi Nyamo -Hanga alisema mkandarasi atakayejenga njia ya kusafirisha umeme ni Kampuni ya Shyma Power India Limited.
.