Monday, December 23, 2024
spot_img

KUZALIWA PORINI KWA REMMY ONGALLA AKIWA NA MENO MAWILI, AGANO LA KUTONYOA NYWELE HADI KIFO CHAKE AKIWA MLOKOLE

MAKALA MAALUMU

IKIWA imepita miaka 14 tangu marehemu Remmy Ongala alifariki dunia, muziki wake bado unaishi kwenye mioyo ya wapenzi wa muziki wa dansi ulimwengu kote.

Muziki wa Remmy; mwanamuzi aliyejizolea umaarufu mkubwa na mashabiki wengi ndani na nje ya Tanzania kutokana na tungo zake za kuvutia na ujumbe aliokuwa akiufikisha kwa jamii kupitia muziki wake, historia ya maisha yake imefichika tofauti na wasanii wengine waliopata kutikisa anga za muziki za dansi ndani na nje ya Tanzania.

Simulizi mbalimbali za watu waliopata kuwa karibu naye zinaeleza kuwa, Remmy Ongala alizaliwa mwaka 1947 katika Mkoa wa Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Alizaliwa katika Kijiji cha Kindu ambacho hakiko mbali sana na mpaka wa Tanzania na DRC ambako wenyeji wanazungumza Lugha ya Kiswahili chenye rafudhi ya kikongo.

Kwa mujibu wa simulizi zilizopo, baba yake Remmy alikuwa mpiga  tumba mashuhuri katika bendi mbalimbali za wakati huo katika Mkoa wa Kivu na mama yake alikuwa mama wa nyumbani.

Inasimuliwa kwamba kabla ya kuzaliwa kwa Remmy, mama yake alipata ujauzito mara mbili na kujifungua salama lakini baada  kujifungua, watoto walifariki.  

Marehemu Ramadhani Mtoro Ongala.

Kwamba alipopata mimba ya Remmy, alifunga safari hadi kwa mganga wa kienyeji kuomba ushauri ni nini afanye baada ya kujifungua ili mtoto wake asifariki. Mganga huyo alimweleza asiende kujifungua hospitalini bali akishikwa uchungu wa kujifungua, afunge safari hadi porini, akamzae mwanaye huko.

Mganga alimweleza mama Remmy kuwa iwapo atajifungua salama, asiomnyoe nywele mwanae na akishajitambua amweleze kuzingatia sharti hilo la kutonywea nywele zake maisha yake yote.

Inasimuliwa kuwa Remmy alizaliwa akiwa na meno mawili ya mbele hivyo alionekana kama mtoto wa ajabu na baada ya kuzaliwa, wazazi wake walimwita Ramadhani Mtoro, hivyo jina lake kamili ni Ramadhani Mtoro Ongala.

Wazazi wake walihama kutoka Mkoa wa Kivu kwenda Kisangani akiwa bado mtoto mchanga na wakati wa utoto wake iliaminika kuwa atakuja kuwa mganga wa kienyeji kwa sababu alizaliwa na meno mawili ya mbele.

Alianza kufundishwa muziki na baba yake mzazi akiwa kijana mdogo na marafiki zake wa utotoni wanasimulia kuwa aliamini kuwa kama ilivyo kwa watoto waliosoma au kufundishwa kisha kuwa madaktari, wanasheria na au walimu, yeye angekuwa mwanamuziki kutokana na mafunzo ya muziki aliyokuwa akipatiwa na baba yake na hadi mwaka 1960, tayari Remmy alikuwa mcharaza gitaa mzuri.

Baba yake alifariki dunia mwaka 1963 na muda mfupi baada ya kifo cha baba yake alijiunga na shule ya msingi lakini hakumaliza elimu ya msingi kwa sababu ya ukata kwani mama yake alishindwa kumudu kulipa ada ya shule.

Mwaka mmoja baadaye, mama yake Remmy naye alifariki na kumuacha akiwa na jukumu la kulea wadogo zake, wakati huo akiwa na umri wa miaka 17.

Marehemu Ramadhani Mtoro Ongala.

Baada ya kuondokewa na wazazi wake wote wawili, Remmy alianza kupambana na maisha ili kujikimu yeye mwenyewe na kuwalea wadogo zake kwa kutumbuiza kwenye hoteli mbalimbali nchini Kongo.

Akiwa na kundi la wanamuziki vijana walilolianzisha na kulipa jina la Bantu Success, walitumbuiza pia kwenye maeneo ya wazi na mahali popote walipoitwa kutoa burudani na kadri siku zilivyosonga, ujuzi wa Remmy wa kupiga gitaa uliongezeka. Remmy akawa na uwezo mzuri wa kipiga ngoma na gitaa.

Remmy alifanya kazi ya muziki kwa miaka kadhaa nchini DRC akiwa na bendi kadhaa maarufu za wakati huo zikiwemo Success Muachana na Grand Mickey Jazz iliyoundwa na wanamuziki wengi kutoka nchini Uganda.

Katika moja ya mahojiano aliyopata kufanya na wanahabari,  Remmy alisema alijifunza mwenyewe kupiga gitaa na  muziki wa Cuba ambao wakati huo ulikuwa maarufu barani Afrika, ulimsaidia kupata staili ya kipekee ya ucharazaji gitaa.

Katika mahojiano hayo, Remmy alisema uimbaji wa Joseph Kabasele na Franco Lwambo Makiadi ulimsaidia kupata staili yake ya uimbaji.

Inaelezwa kuwa Remmy aliliishi agano la mganga na mama yake la kutonyoa nywele na yeye mwenyewe alipata kukaririwa akieleza kuwa awali alikuwa anaona aibu kuwa na nywele ndefu tofauti na wenzake wengi.

Marehemu Ramadhani Mtoro Ongala.

Kwa mujibu wa Remmy, mwonekano wa marehemu Bob Marley akiwa katika kilele cha umaarufu na muziki wake wa raggae ndiyo uliomfanya aanze kuzipenda nywele zake ndefu zinazofahamika zaidi kwa jina la rasta.

Mwaka 1978 Remmy aliingia jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mjomba wake, mzee Kitenzogu Makassy ili kujiunga na bendi maarufu ya wakati huo ya Orchestra Makassy iliyokuwa chini ya Makassy. Huo ukawa ndiyo mwanzo wa maisha yake nchini Tanzania.

Akiwa na Bendi ya Orchestra Makassy, alitunga wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama ā€˜Siku ya Kufa.ā€™ Remmy alitunga wimbo huo kumkumbuka marehemu rafiki yake ambaye historia iliyopo haimtaji jina, tarehe na sababu ya kifo chake.

Wimbo huo ndiyo uliompatia umaarufu nchini Tanzania na hata nchi jirani kabla ya kusambaa sehemu mbalimbali duniani.

Miaka mitatu baada ya Remmy kujiunga na Bendi ya Orchestra Makassy, mzee Makassy aliamua kuihamishia bendi yake nchini Kenya lakini Remmy hakutaka kwenda huko hivyo alijiunga na bendi ya Matimila.

Matimila ni jina la kijiji kimoja kilichoko Kusini mwa Tanzania na muda mfupi baada ya Remmy kujiunga na benki hiyo alichaguliwa kuwa kiongozi.

Chini ya uongozi wake, Remmy aliisuka upya bendi hiyo na kuibadilisha jina ikaitwa Orchestra Super Matimila.

Rammy akaanza kutunga tungo za kuvutia na zenye ujumbe unaogusa jamii, Orchestra Super Matimila na Remmy wakavuma kwenye anga za muziki wa Tanzania na nje ya nchi kutokana na tungo hizo.

Mashairi ya tungo za Remmy yaligusa mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, afya, siasa na ukimwi. Remmy na Orchestra Super Matimila wakazidi kupaa kimuziki na hadi mwishoni mwa miaka ya 1980 walikuwa maarufu katika Bara la Afrika.

Katika moja ya simulizi zake Remmy mwenyewe kama zinavyokaririwa na watu waliokuwa karibu naye, anaeleza kuwa kupata mialiko kwenda kutumbuiza nje ya nchi ni jambo lililokuja kama mchezo tu.

Marehemu Ramadhani Ongala akishambulia jukwaa sambamba na wanamuziki wenzake wa kundi la Orchestra Super Matimila.

Kwamba moja ya kaseti yenye nyimbo zake ilichukuliwa mmoja wa rafiki zake, raia wa Uingereza aliyekuwa shabiki wake mkubwa wakati akiondoka Tanzania kurudi  kwao Uingereza.

Akiwa huko, kaseti hiyo alilipatia shirika linalilokuwa likijishughulisha na kupandisha chati wanamuziki na wasanii wa nchi za dunia ya tatu  lililojulikana kwa jina la World of Music, Arts and Dance (WOMAD).

Kwamba WOMAD walivutiwa na tungo za Remmy na kwa mara kwanza, yeye na Orchestra Super Matimila walialikwa kushiriki maonyesho ya shirika hilo yaliyofanyika barani Ulaya, mwaka 1988.

Baada ya kurudi kutoka Ulaya, Remmy na Orchestra Super Matimila walitoa album ya ā€˜Nalilia Mwana,ā€™ baadhi ya nyimbo zilizokuwa kwenye albamu hiyo ni ā€˜Ndumilakuwiliā€™ na ā€˜Mnyonge hana hakiā€™

Mwaka 1989 Remmy na Matimila walirudi tena Ulaya kwa mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo walipopata nafasi ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ya Stud Real World Studios  iliyokuwa ikimilikiwa na mwanamuziki Peter Gabriel.

Akiwa katika kilele cha mafanikio, Remmy aliimba wimbo wa kipenda roho aliomuimbia mkewe mzungu aliyekuwa amemzalia watoto watatu.

Marehemu Ramadhani Ongala.

Mwaka 1990, Remmy na Orchestra Super Matimila walikwenda tena Ulaya walikorekodi albamu ya Mambo katika studio za Real World. Baadhi ya nyimbo kwenye albamu hiyo aliziimba kwa Lugha ya Kiingereza ili kukihidhi kiu ya wapenzi na mashabiki wake wasiojua Kiswahili. Baadhi ya nyimbo hizo ni No money no life na One world.

Mwaka 1990 aliimba wimbo wa ā€˜Mambo kwa soksiā€™ lakini baadhi ya watu waliupinga kwa hoja kuwa haukuwa na maadili mema kwa jamii lakini yeye mwenyewe alisema ulilenga kuwaasa watu hususani vijana kutumia kondomu ili kuepuka maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Remmy aliimba nyimbo nyingi akiwa na Orchestra Super Matimila zikiwemo Bibi wa mwenziyo, Kipenda roho, Asili ya muziki, Ngalula, Mwanza, Mama nalia, Harusi, Hamisa, Mnyonge hana haki, Ndumilakuwili na Mtaka yote.

Baadaye Remmy alianza kusumbuliwa na maradhi ya kisukari, akaamua kuachana na muziki wa dansi kwa kile alichosema umejaa mambo mengi ya kishetani. Akawa mlokole, akatubudu na kuanza kupiga muziki wa Injili.

Baada ya kuugua kwa muda mrefu, Remmy alifariki dunia jumatatu ya Disemba 13, 2010 nyumbani kwake, Dar es Salaam huku akiacha alama ya kuwa msanii na pengine mtu wa kwanza Tanzania kukemea ngono zembe katika wimbo wake wa mambo kwa soksi.

Viongozi wa serikali na dini walifuata mfano wa Remmy baadaye kukemea na kuelimisha jamii kuepuka ngoni zembe.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya