Wednesday, December 25, 2024
spot_img

YANGA INAPOSIMAMIA KANUNI, TFF IKISAKA BUSARA

 

Wallace Karia

MWANDISHI WA PANORAMA 

GUMZO kubwa mwishoni mwa wiki iliyopita ni mechi ya watani wa jadi iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na wadau wa soka sio tu ndani mbali hata pia nje ya nchi kutibuka. 

Mei 8, mwaka huu ilikua siku muhimu kwa mashabiki wa Simba na Yanga ukizingatia mechi inazokutanisha timu hizi mbili kongwe imeorodheshwa miongoni mwa ‘derby’ kubwa barani Afrika. 

Sekeseke lilianza na taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) siku ya mechi ikieleza kuwa imepokea maelekezo ya mabadiliko ya muda wa kuanza mchezo kati ya Simba na Yanga iliyokuwa ipigwe Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. 

Japo TFF haikueleza kwa kina sababu iliyotolewa na Serikali kupitia wizara yenye dhamana ya michezo, hata hivyo ilisisitiza timu zote mbili zimeshapewa taarifa ya mechi hiyo iliyokuwa imepangwa kuanza saa 11 jioni hadi saa 1 usiku. 

Mechi hiyo ya Mei 8 ilikuwa itoe taswira ya mbio za ubingwa msimu huu wa 2020/21 kwani ushindi kwa Yanga ambayo ipo nafasi ya pili ungepunguza pengo lao na watani zao Simba kuwa pointi moja licha ya kucheza mechi mbili zaidi

Wakati huo huo, ushindi kwa Simba inayoongoza ligi ungewafanya kuwaacha Yanga kwa pointi saba na kuwafanya kukaribia kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa nne mfululizo. Aidha Simba walihitaji mechi hii kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika mwishoni mwa wiki hii dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. 

Mkude


Hata hivyo mechi hiyo la ligi ilishindwa kufanyika kutokana na timu moja kuwasili uwanjani tayari kwa mtanange kuanza saa 11 jioni na baada ya mpinzani kushindwa kufika waliondoka, huku timu nyingine ikifika uwanjani tayari kwa mechi ya saa 1 usiku. 

Yanga ambao waliingia uwanjani kwa ajili ya mechi iliyopangwa kuanza saa 11 jioni walisisitiza katika taarifa yao kwa umma kuwa mabadiliko yaliyofanywa na TFF ni kinyume na kanuni ya 15(10) za Ligi Kuu inayohusu taratibu za michezo. 

Kanuni hiyo inasomeka kama ifuatavyo: “Mabadiliko yoyote ya muda wa kuanza mchezo yatajulishwa ipasavyo kwa pande zote husika za mchezo angalau saa 24 kabla ya muda wa awali.” 

Kimsingi, Yanga wapo sahihi kwa kusimamia kanuni kutokana na TFF kutoa taarifa ya muda wa mechi kuanza kusongezwa mbele siku ya mechi husika. 

Sababu iliyotolewa na TFF mechi kusongezwa mbele kwa saa mbili haikuwa na mashiko kwa sababu ilionekana kama ni maelekezo kutoka wizarani na tafsiri yake ni Serikali kuingilia shughuli za soka kinyume na taratibu za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). 

Macho yote sasa wapo kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, kutoa taarifa ni kwanini mechi hiyo ya watani ilisongezwa kwa saa mbili huku waathirika wakubwa wakiwa mashabiki waliolipa fedha zao kushuhudia mtanange huo. 

Katika kupata suluhu, TFF inaonekana kusaka busara ikieleza kwenye taarifa yake kuwa itakutana kwa haraka na klabu za Simba na Yanga ambapo kuna kila dalili tarehe mpya itapangwa kwa timu hizi kongwe kukutana. 


TFF pia imesisitiza imekuwa ikishirikiana na Serikali kama mdau wake mkuu, na itaendelea kushirikiana nayo kuhakikisha kwamba mechi zote za mpira wa miguu zinafanyika kwa amani na usalama, hii pia ikitoa taswira labda mechi ya watani ilisongezwa mbele kuhakikisha kunakuwa na usalama wa kutosha. 

Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), imepewa maelekezo na TFF kutoa taarifa ya kina kuhusu kuahirishwa kwa mchezo huo pamoja na kushughulikia hatma ya wapenzi wa mpira wa miguu waliolipa viingilio kuingia uwanjani. 

Hapa TPLB itahitajika kutumia busara na wakati huo huo linaposhughulikiwa jambo hilo kwa haraka italazimika kufuata taratibu za kikanuni. 

Swali linabaki, kama kanuni za mchezo zitazingatiwa, nani anastahili pointi tatu na mabao mawili baada ya mechi kushindwa kuchezeka? Mpira sasa upo mikononi mwa TPLB kukata mzizi wa fitina. 

 

 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya