MAKALA MAALUMU
DK. DOTTO Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati amepiga hatua sita muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya wizara anayoiongoza pamoja na mipango ya ofisi yake kwa mwaka ulioisha wa 2023/2024.
Hatua hizo ni utekelezaji wa vipaumbele muhimu sita alivyovitangaza kwenye Bunge la Bajeti alipowasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2024/25 aliyosema maudhui yake yamezingatia Hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2023/24 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2024/25.
Dk. Biteko alitangaza vipaumbele hivyo akianza na kukamilika kwa miradi mbalimbali ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na wizara yake za kuimarisha uzalishaji.
Kipaumbele cha pili alichokitaja ni usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini na cha tatu ni kuendelea kupeleka umeme vijijini, vitongojini, katika visiwa na maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa, vituo vya afya na pampu za maji, wachimbaji wadogo wa madini, maeneo ya kilimo na viwanda, mashuleni na katika mahakama za mwanzo vijijini.
Hapo, alitaja pia utekelezaji wa mikakati na programu mbalimbali za kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia (clean cooking) nchini.
Dk. Biteko alitaja kipaumbele cha nne kuwa ni kuanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia kuwa kimiminika, (Liquefied Natural Gas – LNG).
Alitaja kipaumbeke cha tano ni kuendelea kutekeleza mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Mkoa wa Tanga, Tanzania (EACOP).
Bomba la mafuta linalojengwa kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania.
Alisema katika kipaumbele hicho, pia kuna shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya kimkakati, usambazaji wa gesi asilia viwandani, majumbani na nchi jirani, kuimarisha matumizi ya Gesi Asilia iliyoshindiliwa, (Compressed Natural Gas CNG) katika magari pamoja na kunadi vitalu vilivyo wazi katika maeneo ya nchi kavu na baharini ili viendelezwe.
Na sita, alisema wizara yake ilielekeza nguvu kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli kwa kuzingatia umuhimu wake katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii pamoja kuimarisha ufanisi katika kushughulikia bidhaa hizo.
Dk. Biteko alisema utekelezaji wenye mafanikio wa vipaumbele hivyo ulitokana na Bunge kuidhinisha matumizi ya Shilingi trilioni 3.04 kwa Wizara ya Nishati ambapo Shilingi trilioni 2.6 ziliidhinishwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Shilingi bil. 87.9 kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Hata hivyo, Dk. Biteko alisema hadi Machi, 2024, wizara yake ilipokea Shilingi trilioni 1.8 ambapo Shilingi bil. 27,07zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi trilioni 1.7 zilikuwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Katika hotuba yake hiyo, Dk. Biteko alizungumzia utekelezaji wenye mafanikio wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme mwaka 2023/24 kuwa ni kuongezeka kwa uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa ambao hadi Machi 2024 ulifikia megawati 2,138 kutoka megawati 1,872.1 zilizozalishwa mwaka 2022/23 na kwamba hilo ni ongezeko la asilimia 14.2.
Alieleza zaidi kuwa uzalishaji wa umeme kupitia Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 umeanza kwa kuzalishaji Megawati 235 kupitia mtambo namba tisa.
Bwawa la kuzalisha Umeme la JNHPP.
Alisema matarajio yaliyopo ni mradi huo kukamilika Disemba, 2024 kwa mitambo yote nane yenye uwezo wa kuzalisha Megawati 235 kila moja kuwa inazalisha umeme.
Aliendelea kueleza kuwa ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi I Extension inayozalisha megawati 185; kila mmoja unafua umeme kiasi cha megawati 40 inafanya kazi na inaingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa.
Muonekano wa Kinyerezi I Extentation
Kazi nyingine iliyotekelezwa kwa mafanikio ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Rusumo unaozalisha megawati 80 ambao umejengwa kwa ushirikiano wa nchi tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda kwa mgawanyo sawa wa umeme kwa kila nchi.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kunaiwezesha Tanzania kupata megawati 27 zinazoingia kwenye Gridi ya Taifa.
“Ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa jua mkoani Shinyanga wa megawati 150 unaendelea na matarajio ni umeme huo kuanza kuzalishwa ifikapo Januari, 2025.
“Serikali pia iliendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya kuzalisha umeme ikiwa ni pamoja na Malagarasi megawati 49.5, Ruhudji megawati 358, Rumakali megawati 222, Kakono megawati 87.8 na Kikonge megawati 321 ambapo hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake ni kama inavyofafanuliwa katika hotuba yangu,” alisema Dk. Biteko.
Hotuba hiyo ya Dk. Biteko inazungumzia pia usafirishaji na usambazaji umeme nchini kuwa, umeme ukishazalishwa hauna budi kusafirishwa na kusambazwa ili uweze kuwafikia watumiaji hivyo ni muhimu kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Alisema mafanikio yaliyopatikana mwaka 2023/24 kwa kuimarisha miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme ni miundombinu ya kusafirisha umeme kuongezeka hadi kufikia jumla ya urefu wa kilomita 7,745.4, ikiwa ni ongezeko la asilimia 21.7 ikilinganishwa na kilomita 6,363.3 za mwaka 2022/23.
Alitaja pia kuanza kutumika kwa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 kutoka JNHPP hadi Chalinze pamoja na kituo kipya cha kupoza umeme cha Chalinze cha kilovoti 400/220/132 kinachotumika kupoza na kusafirisha umeme unaotoka JNHPP na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
Alisema mradi wa njia ya kusafirisha umeme, msongo wa kilovoti 220 kutoka Morogoro hadi Dodoma kwa ajili ya uendeshaji wa treni ya umeme (SGR Lot II) umekamilika kwa asilimia 99.
Treni ya mwendo kasi ambayo inatumia umeme kutoka Gridi ya Taifa
Pia aliutaja mradi wa njia ya kusafirisha umeme, msongo wa kilovoti 400 kutoka Singida, Arusha hadi Namanga kuwa umekamilika kwa asilimia 99.4.
Akiendelea kusoma hotuba yake hiyo bungeni, Dk. Biteko alisema ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme, msongo wa kilovoti 400 kutoka Arusha hadi Namanga yenye urefu wa kilomita 114.3 umefikia asilimia 97.5 na kituo cha kupoza umeme cha Lemugur kimekamilika kwa asilimia 100 na tayari kimewashwa.
Alizungumzia pia kuongezeka kwa miundombinu ya kusambaza umeme hadi kufikia kilomita 176,750.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 4.9 ikilinganishwa na kilomita 168,548.5 za mwezi Mei, 2023.
Alisema hadi Machi 2024, wateja 4,784,297 wameunganishiwa umeme, idadi ambayo ni ongezeko la asilimia 9.4 ikilinganishwa na wateja 4,319,258 waliokuwa wameunganishiwa umeme Juni, 2023.
Dk. Biteko aliitaja miradi mingine ya usafirishaji wa umeme iliyoendelea kutekelezwa kuwa ni njia ya kusafirisha umeme, msongo wa kilovoti 220 kutoka Rusumo hadi Nyakanazi na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma (TAZA).
Mingine ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma na mradi wa kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Projects) – Gridi imara.
Kuhusu kuimarisha utoaji wa huduma ya umeme kwa wananchi, Dk. Biteko alisema hatua mbalimbali zilichukuliwa ikiwa ni pamoja na kupanua kituo cha huduma kwa wateja (Call Center) kwa kuongeza vifaa na wapokea simu kutoka mawakala 63 hadi 100.
Pia kuanzisha mfumo unaomuwezesha mteja kuhudumiwa kwa haraka zaidi bila kupiga simu kwa njia ya ujumbe wa simu (CHATBOT) na kuanzisha mfumo utakaowawezesha wateja kupata taarifa maalumu za hali ya upatikanaji wa umeme kwa haraka kwa njia ya ujumbe wa simu ambayo ipo katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji.
Mpango wa kupeleka nishati vijijini nao aliuzungumzia kwenye hotuba yake hiyo akieleza kuwa Serikali iliendelea kuchukua hatua za kuimarisha upatikanaji wa nishati vijijini ambapo hadi Machi, 2024 vijiji 11,837 sawa na asilimia 96.37 ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vilikuwa vimeunganishwa na umeme.
Wizara ya Nishati imefanikiwa kupelekea umeme vijijini kwa asilimia 96.37
Kwamba, wizara yake kama mtekelezaji wa mipango ya Serikali katika Sekta ya Nishati, imefanikiwa kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi vijijini ambapo taasisi 63,509 zinazotoa huduma kwa jamii ikiwemo elimu, biashara, pampu za maji, vituo vya afya na nyumba za ibada zimeunganishiwa umeme ikilinganishwa na taasisi 43,925 za Aprili, 2023.
Alisema katika kipindi hicho, Serikali iliendelea kuchukua hatua za kupeleka umeme vitongojini, visiwani na maeneo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa; pia kwenye vituo vya afya na pampu za maji, wachimbaji wadogo wa madini, viwandani, kwa wakulima na mashuleni pamoja na mahakama za mwanzo vijijini.