Monday, December 23, 2024
spot_img

UFISADI MKUBWA TAASISI YA UTAFITI WA VIUATILIFU NA AFYA YA MIMEA

RIPOTA PANORAMA – ARUSHA

TAASISI ya Utafiti wa Viuatilifu na Afya ya Mimea inadaiwa kufanya ufisadi wa mabilioni ya fedha kwa kushirikiana na mmoja wa wafanyabiashara wenye ukwasi mkubwa wa mkoani Arusha.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania PANORAMA Blog na taarifa kutoka vyanzo vya habari vilivyo ndani ya Wizara ya Kilimo, umeonyesha kuwa uongozi wa taasisi hiyo ukishirikiana na mfanyabiashara huyo (jina lake limehifadhiwa kwa muda kwa sababu hajapatikana kuzungumza) umekuwa ukiingia makubaliano ya kifisadi ya kusambaza viuatilifu feki kwa wakulima.

Tanzania PANORAMA Blog, katika uchunguzi wake imebaini mfanyabiashara huyo amekuwa akipewa zabuni za mamilioni ya fedha na taasisi hiyo naye hutengeneza viuatilifu feki.

Taarifa zinasema kuwa mwaka 2023, taasisi hiyo iliingia makubaliano na mfanyabiashara huyo ya kusambaza kiuatilifu cha kuua nzige na kwamba alilipwa zaidi ya Shilingi bil. 7.

Malipo hayo ya mabilioni ya fedha yalilipwa kwa mkupuo mmoja lakini wakulima baada ya kuanza kutumia kiuatilifu hicho, walibaini hakina uwezo wa kuua nzige.

Taarifa zaidi zilizopatikana zinaeleza kuwa kiuatilifu kilichosambazwa na mfanyabiashara huyo kilikuwa na kiwango kidogo cha sumu ya kuua nzige tofauti na makubaliano yaliyotiwa saini kuhusu ubora wake.

“Licha ya kiuatilifu hicho kukosa ubora, taasisi ilikichukua na kukisambaza kwa wakulima na matokeo yake, wakulima walipata hasara kubwa ya mazao yao kuliwa na nzige katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa yameathiriwa na wadudu hao ambao walikuwa hawafi kwa kiuatilifu kilichokuwa kinatumiwa.

“Baada ya wakulima kuanza kupiga kelele kupitia kwenye vyombo vya habari na wanasiasa kuingilia kati, taasisi ikaamua kuingia mkataba na kampuni nyingine.

“Huo mkataba mwingine uliingiwa wakati huyo bwana akiwa amekwishalipwa fedha zote na hakuna hatua zilizochokuliwa dhidi yake, kampuni iliyopewa kazi ya kuzalisha viuatilifu vingine ilifanya kazi vizuri, wakubwa wa taasisi hiyo wakarudi mashambani kupiga dawa upya,” anasema mmoja wa watoa taarifa.

Nzige

Inaelezwa pia kuwa kampuni iliyopewa zabuni ya kuiuzia taasisi kiuatilifu chenye ubora baada ya kile cha kwanza kushindwa kufanya kazi kwa sababu kilikuwa feki haijalipwa gharama zake zinazotajwa kufikia Shilingi bil 5.

Inaelezwa kuwa hata taratibu za utoaji zabuni kwa kampuni hiyo zilikiukwa jambo ambalo limezua sintofahamu kwa kampuni hiyo kulipwa madai yake.

“Hii kampuni ya pili, kiuatilifu ilichotengeneza kilifanya kazi lakini baada ya kukaguliwa na wataalamu hivi karibuni ilionekana hakijathibitishwa na taasisi husika. Sasa hapo kuna swali linalowaumiza vichwa ni kwa namna gani mamlaka ilitumia dawa ambayo haijaithibitisha,” anaeleza zaidi mtoa taarifa.

Taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa baada ya kuibuka kwa sintofahamu hiyo, Wizara ya Kilimo ilituma timu ya wataalamu waliofika jijini Arusha kwa ajili ya kuikagua taasisi hiyo na kugundua madudu mengi.

Miongoni mwa madudu yanayoelezwa kugunduliwa na wataalamu wa Wizara ya Kilimo ni taasisi hiyo nyeti kutozingatia taratibu za utoaji zabuni na mfanyabiashara anayetengeneza viuatilifu feki alikuwa mbioni kupewa zabuni nyingine yenye thamani ya Shilingi bil. 10 ya kusambaza kiuatilifu kingine.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ametafutwa bila mafanikio kulizungumzia jambo hilo na alipotafutwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu na Afya ya Mimea kuzungumzia tuhuma hizo, alisema atatoa kauli yake Ijumaa wiki hii, saa nne asubuhi.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya