RIPOTA PANORAMA
Mawasiliano ya siri ya mbunge mmoja aliyepata kuwa waziri yanazohusu biashara ya vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi kutoka Bodi ya Sukari Tanzania yamenaswa.
Mawasiliano hayo ya siri ya mbunge (jina lake kapuni kwa muda) ni mkataba baina ya mtoa huduma (service provider) na wakala wa wafanyabiashara wasaka vibali cha kuagiza sukari nje ya nchi kutoka Bodi ya Sukari ambao unamuwezesha kuvuna mabilioni ya Shilingi.
Tanzania PANORAMA Blog imeyaona mawasiliano hayo ya barua pepe baina ya mwanasheria aliyepewa kazi ya kuandaa mkataba,mbunge, wakala wa wafanyabiashara na wafanyabishara wasaka vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi.
Mkataba huo ulitumwa kwa mbunge Julai 31, 2023 na baadhi ya vipengele vyake vinaeleza usiri wa mkataba na mavuno ya mabilioni ya fedha ambayo ataweka kibindoni kwa kufanikisha upatikanaji wa kibali cha kuagiza sukari nje ya nchi kutoka Bodi ya Sukari.
Tanzania PANORAMA Blog imethibitishiwa na vyanzo vyake vya habari vya uhakika kuwa mwanasheria huyo (pia jina lake limehifadhiwa) ndiye aliyeandaa mkataba huo kabla ya kutelekezwa alipoukamilisha.
Taarifa zinasema mwanasheria huyo alifichwa majina ya wafanyabiashara na kampuni zilizokuwa zikitafutiwa vibali na mbunge huyo na kwamba alielekezwa kuuandaa hadi utakapokamilika, kupitiwa na kuidhinishwa na mbunge ndipo angepewa majina ya wahusika kuyajaza.
Tanzania PANORAMA Blog imethibitisha kwa kuona mawasiliano ya barua pepe ya mwanasheria na mbunge huyo yaliyofanyika Juilai 31, 2023.
“Baada ya kuibuka kwa kashfa ya sukari bungeni ndiyo imejulikana sasa kuna wabunge tena waliopata kushika nyadhfa kubwa za uwaziri walioweka kibindoni mabilioni ya Shilingi kwa kuwatafutia wafanyabishara vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi kwa makubaliano ya kimkataba ya kulipwa mabilioni ya fedha.
“Mambo ni mengi, ipo pia kashfa inayomuhusu mrembo wa Tanzania wa zamani na mwanaye aliyezaa na huyu mbunge na waziri wa zamani. Huyu miss Tanzania alisingiziwa na huyu bwana kuwa ana kichaa kusudi amnyang’anye mtoto na yapo mengine. PANORAMA tuna imani na ninyi kwa kazi zenu za uhakika. Ushahidi ni huu. Ni muhimu umma ujua tuna wabunge wa aina gani,” kilisema chanzo chetu cha habari huku kikionyesha nyaraka.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina
Mbunge huyo ameulizwa na Tanzania PANORAMA Blog jana na kukiri kuwa barua pepe iliyotumika kwenye mawasiliano na mwanasheria aliyeandaa mkataba huo ni yake lakini alitaka atumiwe mkataba auone.
Tanzania PANORAMA Blog imeanza kufikishiwa nyaraka hizi za siri ikiwa ni siku chache baada ya kuibuka kwa skandali ya sukari wakati wa Mkutano wa Bunge la Bajeti uliomalizika hivi karibuni ambapo Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina alimtuhumu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe pamoja na mambo mengine kusema uongo bungeni kuhusu muda wa kutolewa kwa vibali vya kuagiza sukari kwa wazalishaji wa sukari nchini.
Baada ya Mpina kumshutumu Bashe kwa uongo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson alimtaka mbunge huyo kuwasilisha ushahidi wa tuhuma zake kwake, jambo ambalo alilitekeleza kisha akazungumza na waandishi wa habari. Uamuzi huo wa Mpina wa kuzungumza na waandishi wa habari ulijibiwa bungeni na Spika Tulia kuwa ni kumkosea adabu yeye na Bunge.
Spika alimpeleka Mpina kuhojiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka nayo iliwasilisha taarifa yake bungeni ikithibitisha kauli ya Spika dhidi ya Mpina ambaye alihukumiwa kutohudhuria vikao 15 vya Bunge.
Kabla ya kupitishwa kwa adhabu huyo, Spika Tulia aliwapa fursa wabunge kujadili ripoti ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ambapo wabunge wote waliopewa nafasi ya kuzungumza, akiwemo ambaye nyaraka zake za biashara ya kusaka vibali vya sukari zimenaswa walimshambulia Mpina.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Baada ya kuadhibiwa bungeni, Mpina alizungumza tena na waandishi wa habari akieleza kutotendewa haki na Spika na nia yake ya kumshtaki mahakamani (Spika) pamoja na Waziri wa Kilimo, Bashe na tayari zaidi na mawakili 10 wamejitokeza kumuwakilisha kwenye kesi hiyo.
SOMA TANZANIA PANORAMA BLOG KESHO KUJUA ZAIDI UNDANI WA HABARI HII NA JINA LA MBUNGE MFANYABIASHARA YA VIBALI VYA SUKARI NJE YA NCHI PAMOJA NA MALIPO YA MABILIONI YA FEDHA YALIYO KWENYE MKATABA.