RIPOTA PANORAMA
PORI la Hifadhi ya Wanyamapori la Simanjiro limevamiwa na kundi la wanaodaiwa kuwa ni majangili wa kiarabu wanaowinda na kuua kwa fujo wanyamapori, wakiwemo wanaolindwa kisheria.
Inadaiwa majangili hao huingia nchini kama wageni wanaokuja kumtembelea rafiki yao mwenye makazi yake hapa nchini lakini ana uraia wa Yemen na Falme za Kiarabu (UAE).
Vyanzo vya habari vilivyo karibu na mwarabu huyo anayedaiwa kujihusisha na ujangili vimeeleza kuwa anaishi mkoani Arusha na amejipenyeza kwa baadhi ya watu wenye madaraka serikalini anaotumia majina yao kujikinga na mkono wa sheria.
Wanyama wanaodaiwa kuuawa kwa fujo ni simba, nyumbu, ndege anayejulikana kwa jina la kori bustard na lesser bustard, digidigi na impala majike.
Inadaiwa mwarabu huyo hana leseni ya aina yoyote ya kumruhusu kufanya shughuli za uwindaji nchini lakini anafanya uharamia kwa kujificha nyuma ya wazawa wenye leseni na au vitalu vya uwindaji.
Mmoja wa watu (mwarabu) wanaodaiwa kujihusisha na ujangili katika Pori la Hifadhi ya Wanyamapori la Simanjiro akiwa emeshika digidigi aliyemuua kwa kumpiga risasi. (picha zote kwa hisani ya vyanzo vya habari)
“Ni mtu hatari, hana leseni lakini mbinu anayotumia kuendesha mauaji ya wanyamapori ni pesa. Anawalaghai watanzania wenye vitalu vya uwindaji na au leseni kuingia nao ubia wa kibiashara na kwa kutumia mwamvuli huo, hutekeleza vitendo vya uhalifu.
“Lakini pia yupo karibu na baadhi ya watu wenye madaraka makubwa serikalini, anatumia majina yao kujikinga na sheria na huwa anatamba kabisa kuwa anatembea na ulinzi wa wakubwa.
“Taarifa zake zipo kwenye mamlaka za serikali kwa muda mrefu lakini yupo, haijulikani hapa anaishi kwa kibali gani, kama mfanyabiashara au ameishapata uraia lakini yupo hapa hapa.
“Analo genge la majangili wenzake katika nchi za kiarabu ambao huwa wanakuja nchini kuuwa wanyama kisha wanaondoka. Na wala hawajifichi, wanatangaza kwenye mitandao biashara ya wanyama wetu wanaowaua,” kimeeleza chanzo chetu cha habari.
Taarifa zaidi zinadai kuwa taasisi za serikali zenye dhamana ya kulinda wanyamapori na kusimamia sheria za uwindaji zimefikishiwa taarifa za kuwepo kwa genge hilo la maharamia takribani miaka mitatu sasa lakini zipo kimya.
Jitahada za kumpata Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA) kuzungumzia suala hili hazijafanikiwa, hata hivyo Tanzania PANORAMA Blog inaendelea na jitihada za kumfikia ili kupata kauli yake.