Monday, December 23, 2024
spot_img

NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI ANA DOA LA RUSHWA, MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA

RIPOTI MAALUMU (1)

CHARLES MULLINDA

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Pastory Mnyeti ana doa la rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, kukiuka misingi ya utawala bora na inapendekezwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ashtakiwe mahakamani.

Viashiria vya harufu ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka vinatajwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwenye ripoti ya uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka ambayo pamoja na mambo mengine inaeleza uhusiano wa Mnyeti na Salum Al Amry wa kumchimbia visima vya maji wakati wa uchaguzi mkuu wa 2020. Amry ana mgogoro wa kibiashara na Dk. Hamis Kibola ambaye ndiye aliyemfikisha Mnyeti mbele ya Tume.  

Doa la Mnyeti lililofichuliwa mwaka 2021 na ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora lilififia lakini halijapata kufutika hadi zama hizi za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amepata kutamka maneno haya;

“Haki za binadamu… zimetambuliwa kwenye Katiba yetu… tumesaini na kuridhia mikataba ya kikanda na kimataifa kuhusu haki za binadamu… tumeanzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora hapa nchini ambapo moja ya majukumu yake ni kupokea malalamiko na kuyafanyia uchunguzi.. pia nchi yetu inaongozwa na sheria, hakuna aliye juu ya sheria.    

Kauli hii ya Rais Samia inaakisi kazi iliyofanywa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora chini ya Mwenyekiti, Jaji Mathew Mwaimu, iliyomtia doa hilo Mnyeti katika ripoti yake ya Oktoba 25, 2021 baada ya kuchunguza tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka alipokuwa Mkuu wa Mkoa (RC) wa Manyara.

Tanzania PANORAMA Blog imeiona ripoti ya tume hiyo na kwa kuzingatia uzito wake; na pia ikizingatia kauli ya Rais Samia kuhusu kuanzishwa kwa tume hiyo na majukumu yake na pia kutambuliwa kwa haki za binadamu kikatiba, hapa inaripoti kwa umma. Hii ni RIPOTI MAALUMU. 

Rais Samia Suluhu Hassan

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ilipokea malalamiko ya Dk. Hamis Kibola dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, sasa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti na aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Emboreet, Belinda Sumari. Dk. Kibola anadai kuwa alikamatwa kwa amri ya Mnyeti, akawekwa mahabusu bila kufikishwa mahakamani kwa muda mrefu na alizuiwa kuingia kwenye kitalu chake cha uwindaji kwa miezi nane.

Ikitumia mamlaka yake ya kikatiba na Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, ilichunguza malalamiko hayo na kutoa ripoti inayoeleza kuwa akiwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mnyeti alikiuka taratibu za utendaji kazi serikalini, alitoa kauli zisizo na ukweli mbele ya Tume, alitumia madaraka yake vibaya na alikiuka haki za msingi za binadamu.

Katika ripoti yake, Tume inaeleza kuwa uchunguzi wake kwenye malalamiko yaliyofikishwa mbele yake na Dk. Kibola, ilibaini Mnyeti alimuamuru Sumari kumzuia Dk. Kibola kuingia kwenye kitalu chake cha uwindaji huku akiwa na vibali vyote halali vilivyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii vya umiliki wa kitalu hicho.

Kwamba Mnyeti mwenyewe aliiambia Tume uamuzi wake ulilenga kuruhusu uchunguzi dhidi ya tuhuma za ujangili zilizokuwa zikimkabili Dk. Kibola.

Lakini ripoti ya Tume inaeleza kuwa uamuzi wa Mnyeti haukufuata taratibu za mawasiliano ya utendaji kazi serikalini unaoelekeza Mkuu wa Mkoa kumjulisha kwa maandishi Katibu Tawala Mkoa kuhusu uamuzi wake huo ambaye naye amgemjulisha Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Simanjiro.

Ripoti inaeleza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Simanjiro naye angemjulisha Afisa Mtendaji Kata ya Emboreet, Sumari kutekeleza agizo la kumzuia Dk. Kibola kuingia kwenye kitalu chake; lakini badala yake Mnyeti alitoa maelekezo moja kwa moja kwa Afisa Mtendaji Kata ya Emboreet, Sumari kwa simu.

Jaji Mathew Mwaimu

Tume inaeleza pia kwenye ripoti yake kuwa Dk. Kibola alimuandikia Mnyeti ampe barua ya kumzuia kuingia kwenye kitalu chake lakini Mnyeti hakumjibu na pia Dk. Kibola alimuandikia Afisa Mtendaji Kata, Sumari kumuomba amuandikie barua ya zuio, naye hakumjibu.

Mnyeti anakaangwa zaidi na ripoti ya Tume hiyo inayoonyesha kuwa maelezo aliyoyatoa mbele ya Tume alipokuwa akihojiwa kuwa kulikuwa na barua ya malalamiko ya wananchi kuhusu kuwepo uwindaji haramu kwenye kitalu cha Kampuni ya HSK Safari Ltd ambayo inamilikiwa na Dk. Kibola hayakuwa na ukweli kwani hakukuwa na barua kama hiyo kutoka kwa wananchi.

Inaongeza kuwa hakukuwa na zuio lolote lililokuwa limewekwa na mahakama na au Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye ana mamlaka ya kisheria dhidi ya wanyamapori kumzuia Dk. Kibola kuingia kwenye kitalu chake na kufanya shughuli zake.

Aidha, wakati Mnyeti akimzuia Dk. Kibola kuingia kwenye kitalu chake hicho, Wizara ya Maliasili na Utalii ilikuwa imeiandikia barua kampuni yake ya HSK kuipongeza kwa utii wa taratibu, kanuni na sheria za wanyamapori.

Ripoti ya Tume inataja tarehe ya barua iliyoandikwa na Waziri wa Maliasili na Utalii kuwa ni Agosti 13, 2015 ambayo pamoja na pongezi kwa kampuni hiyo kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria za wanyamapori, ilikuwa inaiongezea muda wa umiliki wa kitalu hicho kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2022.

Naibu Waziri wa Kilimo, Alexander Mnyeti

Tume inasema maelezo ya barua ya Waziri wa Maliasili na Utalii yanathibitisha kuwa Kampuni ya Dk. Kibola haikuwa inajihusisha na shughuli za uwindaji haramu na ujangili kama ilivyoelezwa na Mnyeti mbele ya Tume kuwa kampuni hiyo ilikuwa ikijihusisha na uwindaji haramu na ujangili kwa zaidi ya miaka kumi.

Lakini pia ripoti hiyo inaeleza kuwa uchunguzi wa Tume ulibaini kuwa Mnyeti alikuwa hana mamlaka ya kisheria ya kuweka zuio kwenye mambo ya uwindaji kwani mwenye mamlaka hayo, kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi na Wanyamapori, sura ya 283, kifungu cha 38(1) ni Waziri wa Maliasili na Utalii.

Sehemu ya ripoti hiyo inasomeka; ‘kwa mujibu wa kifungu cha 38(12) na 38 (15) vya Sheria ya Usimamizi wa Wanyapori, sura ya 283, iwapo kuna madai ya ukiukwaji masharti ya umiliki wa kitalu cha uwindaji, baada ya kushauriwa na Kamati ya Ushauri wa Uwindaji wa Kitalii, Waziri wa Maliasili na Utalii ndiye mwenye mamlaka ya kuchunguza na kusitisha kibali cha uwindaji na siyo mamlaka nyingine kisheria.

‘Aidha, Ofisi ya TAWA Kanda ya Kaskazini walipohojiwa na Tume, tarehe 3/7/2021 mkoani Arusha, walieleza kuwa hawakujua kuwepo kwa suala la zuio na wala hawakushirikishwa katika jambo lolote linalomuhusu mlalamikaji.’

Ripoti ya Tume inazungumzia pia kamati iliyoundwa na Mnyeti kuchunguza masuala ya wanyamapori kuwa haikuwa na mamlaka ya kufanya uchunguzi wa masuala ya uwindaji wa wanyapori kwa kuwa mamlaka ya kuunda kamati hiyo yako nje ya mamlaka ya kisheria ya mkuu wa mkoa.

Kwamba pamoja na kamati hiyo kufanya uchunguzi, mapendekezo yake hayakuwafikia walengwa ambao ni Dk. Kibola na Wizara ya Maliasili na Utalii lakini pia hata muundo wa kamati yenyewe iliyoundwa na Mnyeti, haukuhusisha taasisi zinazojihusisha na shughuli za usimamizi wa wanyamapori.

Ripoti ya Tume inaeleza bayana kuwa kwa ushahidi huo uliobainika kwenye uchunguzi wake, Mnyeti (Mkuu wa Mkoa) hakuwa na mamlaka ya kuweka zuio aliloweka dhidi ya Dk. Kibola na alifanya kazi nje ya mipaka yake kisheria.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ilifanya uchunguzi huo na kutoa ripoti yake kwa mujibu wa Ibara ya 130(1) (c ) (f) na (g) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, ikisomwa pamoja na vifungu vya 6(1) (c) (f) na (g), 11 (I) (b) (i) na 22(5) (a) vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, sura ya 391 ambavyo vinaipa Tume mamlaka ya kufanya uchunguzi.

ITAENDELEA KESHO.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya