Tuesday, December 24, 2024
spot_img

RC MWANZA AAHIDI KUWAPIGANIA WAANDISHI WALIO MAHABUSU, ASEMA UPELELEZI KESI YA DK. NAWANDA UNAENDELEA

RIPOTA PANORAMA

MKUU wa Mkoa wa Mwanza (RC), Said Mtanda (pichani hapo juu)ameahidi kufuatilia kwa karibu sababu ya waandishi wa habari watatu kuwekwa mahabusu kwa muda mrefu bila kupewa dhamana katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Mkoa wa Mwanza.

RC Mtanda ametoa ahadi hiyo leo alipozungumza na Tanzania PANORAMA Blog iliyomuuliza sababu za waandishi kukamatwa na kunyimwa dhamana huku kukiwa na taarifa zinazodai kuwa mmoja wa waandishi walio mahabusu ni mgonjwa.

Waandishi walio mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Mwanza ni Dina Maningo ambaye ni mmiliki wa Dima Online aliyekamatwa nyumbani kwake Tarime mkoani Mara Juni 13, 2024 na kusafirishwa usiku hadi Mwanza ambako aliwekwa mahabusu.

Dina Maningo

Tovuti inayomilikiwa na Maningo ilikuwa ya kwanza kuripoti tuhuma kuhusu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda kumlawiti mwanachuo wa kike mkoani Mwanza na Juni 11, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan alimfukuza kazi.

Waandishi wengine waliokamatwa na kuwekwa mahabusu ni Samweli Mwanga na Constatine Mathias inaodaiwa kuwa, pamoja na Maningo waliandika taarifa za siri za upepelezi kuhusu skandali ya Dk. Nawanda kulawiti mwanachuo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza ametafutwa na Tanzania PANORAMA Blog bila mafanikio kuzungumzia suala hilo kwani simu yake ya kiganjani kila inapopigwa haikupokewi na hata Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime licha ya kutafutwa mara kadhaa lakini amejitenga mbali kuizungumzia skendali ya Dk. Nawanda licha ya kuomba aandikiwe maswali ili ajibu lakini alipoandikiwa, hakujibu, alikaa kimya kabisa.

Mtanda ameiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa kwa mujibu wa taratibu, msemaji wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Wilbroad Mutafungwa na alipoambiwa kuwa kila anapotafutwa hapokei simu, alisema atawasiliana naye ilia toe ushirikiano kwa waandishi wa habari.

Amesema, dhamana ni haki ya mtuhumiwa hivyo atalishauri na au kulielekeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kutoa dhamana kwa waandishi hao kwa sababu ni haki yao.

“Kwa mujibu wa taratibu zetu, msemaji wa Jeshi la Polisi ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa na kwa Mkoa wa Mwanza msemaji anaitwa RPC Mutafungwa. Lakini niseme kwa suala hilo kwa sababu mimi nipo nje ya Mkoa wa Mwanza kikazi, nitawasiliana na kamanda wa polisi wa mkoa nijue kama kuna waandishi watatu wanashikiliwa, wanashikiliwa kwa sababu gani lakini kama kesi wanazoshikiliwa nazo zinadhaminika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa

“Dhamana ni haki ya mtuhumiwa kwa hiyo nitawasiliana naye nifahamu sababu ya kuwashilikia kama hakuna sababu za msingi nitafahamu na mimi nitalishauri Jeshi la Polisi au nitaliekeza Jeshi la Polisi kutoa dhamana kwa watu hao kwa sababu ni haki yao,” alisema Mtanda.

Alipoulizwsa kuhusu tetesi zilizopo kuwa waandishi hao wanashikiliwa kwa sababu ya kuripoti skandali ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Nawanda kulawiti mwanachuo, Mtanda alisema haamini hilo kwa sababu skandali hiyo ilitolewa maamuzi ya Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba hivi sasa uchunguzi unaendelea.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda

“Kwanza kutuhumiwa ni suala moja na kuthibitika na tuhuma ni suala jingine. Kwa hiyo kama wameandika habari kuhusiana na jambo hilo, mamlaka zinazohusika, kwa sababu jambo hilo lipo kwenye uchunguzi, ikithibitika kwamba RC alifanya jambo hilo kwa sababu hakuna aliye juu ya sheria atapelekwa mahakamani.

“Kwa hiyo mimi sioni hata sababu kwa nini mtu mwingine kushikiliwa kwa sababu aliandika kwa sababu hata kama asingeandika, jambo hilo limefanyiwa maamuzi na mheshimiwa rais (Rais Samia) lakini pili kuna tuhuma zinachunguzwa zifikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema Mtanda.

Akizungumzia kuhusu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Mutafungwa kutotoa ushirikiano kwa waandishi wa habari, Mtanda alisema atawasiliana naye kumshauri kupokea simu za waandishi.

“Mimi siku zote nipo ‘positive’ kwa waandishi wa habari na jana nilisikia mtu mmoja akisema kuna watu watapelekwa mahakamani kuhusiana na suala la waandishi kushikiliwa ili wakaseme huko mahakamani kwanini wamewashikilia na nikaona ametaja na RC wa Mwanza kwa maana ya wadhfa wake.

“Sasa nikawa najiuliza, RC wa Mwanza anahusikaje na kushikilia watu kwa sababu mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa lakini sina mamlaka ya ukamataji na kama ninakamata ninatoa maelekezo kwa jeshi la polisi na ninawaelekeza taratibu za kisheria zinazotakiwa kufuatwa wakati wa ukamataji ili uwe ukamataji halali kisheria.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime

“Nitawasiliana na kamanda wangu, nitamwambia azungumze na wana habari ,  na kama wanawashikilia baadhi ya polisi, aeleze kwanini wanashikiliwa kwa sababu polisi wanaweza kushikiliwa kwa uchunguzi, ni kitu cha kawaida.

“Na kama waandishi wa habari pia wameshikiliwa kwa uchunguzi ni jambo la kawaida umma ujue wanashikiliwa kwa tuhuma moja, mbili, tatu na haki zao ni zipi,” alisema.

Mtanda alisema yeye ni mdau mkubwa wa wanahabari na amekuwa akipigania maslahi yao na kwamba haogopi chombo cha habari au kutoa taarifa anapofikiwa au kutafutwa na waandishi.

“Mimi hata nikituhumiwa katika jambo lolote lile huwa ninakuwa ‘very cool’, na ninajibu hoja ninayotuhumiwa nayo…. Nitamtafuta kamanda wangu wa polisi nimuunganishe na ninyi waandishi mpate taarifa sahihi. Nakuahidi suala la waandishi kuwekwa mahabusu bila dhamana nalifanyia kazi,” alisema Mtanda.

Akizungumzia mwenendo wa upelelezi wa tuhuma zinazomkabili Dk. Nawanda, alisema uchunguzi bado unaendelea na kwamba utakapokamilika jalada lake litapelekwa kwa mwendesha Mashtaka kwa ajili ya hatua zaidi.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya