Monday, December 23, 2024
spot_img

‘PAZIA JEUSI’ TUHUMA ZA RC KULAWITI MWANACHUO

‘RIPOTA PANORAMA

SAKATA la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda kutuhumiwa kumuingilia kinyume na maumbile na kumlawiti mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), kilichopo jijini Mwanza linadaiwa kufunikwa na ‘pazia jeuzi.’

Yanayodaiwa kufunikwa na ‘pazia jeusi’ kwenye sakata hilo ni washirika wake wa karibu ambao amekuwa akiambatana nao kwenda sehemu  mbalimbali za starehe maeneo ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kuburudika na kusaka wasichana warembo.

Mmoja wa watoa taarifa aliyezungumza na Tanzania PANORAMA Blog amedai kuwa Kanda ya Ziwa upo mtandao wa viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara wanaotumia ushawishi wa fedha na madaraka kuwaingilia wanafunzi hususan wanachuo kinyume na maumbile na kuwalawiti.

“Kanda ya Ziwa kuna mtandao unaohusisha baadhi ya watu wenye madaraka makubwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao huwashawishi kwa fedha wanachuo kuingia nao kwenye uhusiano wa kimapenzi kisha huwataka wafanye nao tendo hilo kinyume na maumbile. Mbali na huyo mkuu wa mkoa wapo wengine walio nyuma ya pazia jeusi. Lakini kwa jinsi hili jambo linavyofunikwa sijui kama watafikiwa. Jamii yetu  inaangamia,” alisema mmoja wa watoa taarifa.

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda

Tayari aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Ismail Nawanda ametuhumiwa kumlawiti mwanafunzi wa SAUT na tayari Rais Samia Suluhu Hassan amekwishamfukuza kazi na kumteua Kenani Kihongosi kuchukua nafasi yake.

Kwa mujibu wa madai ya mlalamikaji kama yalivyoripotiwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari, Dk. Nawanda alimuahidi mwanachuo huyo kubadilisha hali ya maisha yake kiuchumi kama angekubali kuingiliwa kinyume na maumbile kwa kumpatia Shilingi 500,000 kila mwezi na angemsaidia dada yake kupata ajira.

Dk. Nawanda mwenyewe amekwishazungumza na baadhi ya waandishi wa habari na mahojiano yake yamesambazwa kwenye mitandao ya kijamii akieleza kuwa tuhuma za ulawiti zinazomuandama zimepikwa na maadui zake.

Mmoja wa watu wanaodaiwa kuwa nyuma ya pazia jeusi katika sakata hilo ni mbunge wa zamani wa Meatu, Salumu Hamis Selemani, maarufu zaidi kwa jina la Salumu Mbuzi, lakini amekanusha madai hayo katika mahojiano aliyofanya jana na Tanzania PANORAMA Blog.

Salumu Hamisi Selemani, (Salumu Mbuzi)

Akikanusha; Salumu Mbuzi ametoa maelezo yanayojichanganya huku akikiri kuwa karibu na Dk. Nawanda na kwamba alikuwepo kwenye sherehe iliyowakutanisha Dk. Nawanda na mwanachuo anayedai kulawitiwa na mkuu wa mkoa huyo wa zamani.

Taarifa zilizopatikana zinadai kuwa siku ya tukio, Juni 2, 2024 Dk. Nawanda alifika baa ya The Cask akiwa ameambatana na watu wengine wawili, mmoja kati yao akiwa Salumu Mbuzi.

Inadaiwa mwanachuo aliyelawitiwa alifika baa ya The Cask akiwa na wenzake watatu ambao aliwaacha wakiongea na rafiki zake Dk. Nawanda huku yeye akienda kuongea naye ndani ya gari aina ya Toyota Crown ya rangi nyeupe, yenye namba za usajili T 496 BND, iliyokuwa kwenye maegesho ya baa hiyo.

Taarifa zaidi zinadai kuwa mwanachuo huyo alipigiwa simu na Salumu Mbuzi kuelezwa kuhusu uwepo wa mtu wake Jijini Mwanza, hivyo akakutane naye na mwanachuo huyo aliomba kufika eneo la tukio akiwa na wenzake, ombi ambalo lilikubaliwa bila kipingamizi.

Inadaiwa zaidi kuwa gari lililotumika kumlawiti mwachuo huyo, Toyota Crown, yenye namba za usajili T 496 BND, mmiliki wake ni mfanyabiashara Salumu Mbuzi.  

Salumu Mbuzi ametafutwa jana na Tanzania PANORAMA Blog kwa simu yake ya kiganjani na kuulizwa kama ni mmiliki wa gari hilo; alikanusha katakata akieleza kuwa hana gari la aina hiyo wala kampuni yake haimiliki gari la aina hiyo.

“Hiyo gari ipo wapi? sina Toyota Crown. Hiyo gari ina usajili wa nani? Hiyo ni gari ya muhusika mwenyewe. ‘Statement’ si imeandikwa hiyo gari. Kama unauliza ‘issue ya Cask’ kwenye ‘statement’ imeeleza gari hiyo usajili wake na kila kitu. Ni muhusika mwenyewe,” alisema Salumu Mbuzi.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa siku ya tukio la ulawiti aliingia baa ya The Cask akiwa ameambatana na Dk. Nawanda pamoja na mtu mwingine alisema madai hayo siyo ya kweli na alipoulizwa kuhusu madai kuwa alimpigia simu aliyelawitiwa kumtaarifu uwepo wa Dk. Nawanda Jijini Mwanza hivyo ajiandae akakutane naye, madai hayo nayo, Salumu Mbuzi aliyakanusha.

“Usinipeleke huko wewe. Usitake kunitengenezea maneno. Hiyo ‘statement’ inavyoonyesha huyo dada alivyoeleza alikuja hapo na mimi? Mimi nilikuwepo Januari siyo leo. Hiyo ni Januari tunayozungumzia,” alisema Mbuzi.

Akielezea zaidi kuhusu tukio la Januari, 2024 lililowakutanisha Dk. Nawanda na anayedai kulawitiwa, Salumu Mbuzi alisema; “Januari nilikuwepo, mambo ya kumpigia simu sijampigia simu mimi na sikuwa peke yangu nilikuwa na watu kibao tu.

“Hatukuwa watu watatu, sisi tulikuwa zaidi ya watu tisa na wao walikuwa kwenye meza nyingine kabisa. Wao ndiyo walikuwa kwenye ‘birthday’ yao, sisi wala hatukufanya ‘birthiday,’ sisi tulikuwa tuna maongezi yetu tu pale.

“Isipokuwa meza zilikuwa karibu, maingiliano yalikuwepo na ndipo mahali ambako nafikiri walipopeana namba,” alisema Mbuzi.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa ana mawasiliano ya mara kwa mara na aliyelawitiwa, Salumu Mbuzi alisema; “Nyie mna matatizo nyie, kwanza wewe namba yangu umetoa wapi? wewe namba yangu umetoa wapi?” alihoji kwa ukali Salumu Mbuzi na mwandishi alimweleza kuwa namba hiyo anayo tangu yeye Salumu Mbuzi akiwa Mbunge na mwandishi amekuwa mwandishi wa habari za Bunge kwa miaka mingi.

Baada ya kuambiwa hivyo, Salumu Mbuzi alibadilisha kauli ghafla na kueleza hivi,” Namba yangu siyo ‘issue’, kila mmoja anayo lakini ukiniambia mimi nitumie namba yangu kumwita, mimi kuwadi?

“Unaweza kunambia mimi nilimwitia, ngoja, ngoja nikueleze wewe Charles, mimi umeniambia hivi, namba yako ilitumika kumwita, mimi siwezi kuwa kuwadi.

“Mimi nilikuwa simjui wakati wanakutana, wao walikutana …wao wana ‘birthday’ yao, wakaja kutuletea keki na sisi tukala keki ndiyo maneno ninayosema. ‘Birthday’ ilikuwa ya kwao. Huyo mwenye tukio ndiyo ilikuwa ‘birthday’ yake alikuwa na wenzie siyo mmoja, alikuwa na wenzie zaidi ya sita.

“Basi, kama watu wengine tukashiriki, karibuni keki, ‘happy birthday,’ tukawapigia makofi lakini mambo ya mahusiano wanajua wao,” alisema Salumu Mbuzi.

Alipoulizwa kama aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ni rafiki yake, Salumu Mbuzi alisema; “Ni rafiki yangu ee, mimi natoka Simiyu. Ni mkuu wa mkoa wa kwangu na siku ile pale wala hatukuwa na mkuu wa mkoa mmoja, palikuwa pana ‘function.’ Walikuwa wakuu wa mikoa kama wawili hivi.”

Tanzania PANORAMA Blog alimuuliza wakuu wa mikoa wengine waliokuwa kwenye sherehe hiyo ya ‘birthday’ naye alisema “siyo kazi yangu kusema, mkuu wa mkoa hakualikwa kwenye ‘birthday’ mnapomuingiza kwenye hilo jambo hakualikwa wala kwenye pati. Sisi tulikuwa na hamsini zetu pale wao walikuwa na pati yao.”

Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza Salumu Mbuzi kuwa, ikithibitika kwamba ana mawasiliano na aliyelawitiwa, … lakini kabla ya kumaliza kuuliza swali, Mbuzi aliidaka mdomo; “hapo ndiyo unaniambia nini sasa, hata kama niliongea naye, wewe mbona unaongea na mimi?

“Mimi sikumuunganisha naye wala sikumpigia simu kwa ajili ya kumuunganisha. Mimi nawasiliana na kila mtu, mimi simu yangu kila saa inaongea.

“Sikiliza, nakuona wewe unanitafuta maneno mengine kabisa. Ninakwambia hivi mimi nawasiliana na kila mtu. Muhusika si mnaye? Mbona mnaanza kutafuta vitu vingine, nimekuwa nawasiliana naye, nikipigiwa simu niache kupokea.

“Unachojaribu unataka kunisogeza na mimi kwenye hilo jambo ambalo mimi siyo muhusika kwenye mambo ya …. (anatamka neno ambalo tumeshindwa kuliandika kwa sababu za kimaadili) lakini wewe huwezi kuniambia kwamba nisizungumze na watu, mimi ninazungmza na watu.”

Tanzania PANORAMA Blog iliendelea kumbana Salumu Mbuzi kwa kumuuliza; “mwanzoni umesema hujawahi kuongea naye, sasa nakuuliza ikithibitika umepata kufanya naye mawasiliano…,” aliidaka mdomo tena akisema, “Sasa ndiyo swali gani hilo,” nayo ilimjibu “ni swali la kawaida,” naye akasema hivi;

“Unataka niwe na kumbukumbu za kutokea Januari za kuongea na watu, kama huyu mtu alikuwa naye unaelewa walionana toka Januari. Inawezekana walikuwa naye wakiwa pamoja wakapiga simu yao nikaongea nao wakiwa pamoja. Juzi mimi sikuwepo na wala mimi sipo Mwanza.   

Wakati Salumu Mbuzi akieleza hayo, taarifa zilizoripotiwa mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari zikimkariri mwanachuo anayedai kulawitiwa zinakinzana na maelezo yake kuhusu sherehe hiyo ya ‘birthday’ iliyofanyika baa ya The Cask.

Taarifa hizo zinadai sherehe ya birthday iliyofanyika baa ya The Cask ilikuwa kwa ajili ya Salumu Mbuzi.

Tofauti na maelezo ya Salumu Mbuzi, taarifa za kufanyika kwa sherehe hiyo zinaonyesha kuwa Januari 20, 2024 majira ya jioni ndipo mlalamikaji alikutana kwa mara ya kwanza na Dk. Nawanda katika baa ya The Cask iliyopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza ilipokuwa ikifanyika sherehe ya birthday ya Salumu Mbuzi na kwamba kwenye sherehe hiyo, Dk. Nawanda alikuwa mgeni mwalikwa.

Taarifa hii inakinzana na kauli ya Salumu Mbuzi aliyoitoa kwa Tanzania PANORAMA Blog akieleza kuwa sherehe hiyo ya ‘birthday’ ilikuwa ya mwanachuo aliyelawitiwa.

Katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog, kwa maneno yake mwenyewe, Salumu mbuzi alisema; “Wao ndiyo walikuwa kwenye ‘birthday’ yao, sisi wala hatukufanya ‘birthiday,’ sisi tulikuwa tuna maongezi yetu tu pale.

“Isipokuwa meza zilikuwa karibu, maingiliano yalikuwepo na ndipo mahali ambako nafikiri walipopeana namba …. Birthday’ ilikuwa ya kwao. Huyo mwenye tukio ndiyo ilikuwa ‘birthday’ yake, alikuwa na wenzie siyo mmoja, alikuwa na wenzie zaidi ya sita.”

Kuhusu umiliki wa gari linalodaiwa kutumika kwenye kitendo cha kumlawiti mwanachuo huyo ambalo Salumu Mbuzi amesema linamilikiwa na Dk. Nawanda, taarifa zilizopo zinadai kuwa Jeshi la Polisi limetuma taarifa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Mwanza likiomba kujua mmiliki halali wa gari hilo.

Uchunguzi wa namba ya simu inayodaiwa kutumika kumwita mwanachuo huyo unaonyesha imesajiliwa kwa jina la Uliana Peter Kalinga na taarifa nyingine zinaonyesha kuwa simu ya mlalamikaji na CCTV footage vimepelekwa kwenye maabara ya uchunguzi wa kisayansi, Ofisi ya Mkemia Mkuu Mkoa wa Mwanza kwa uchunguzi zaidi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa ametafutwa tangu jana, Juni 11, 2024 majira ya asubuhi bila mafanikio kuzungumzia mwenendo wa uchunguzi wa kesi hiyo na iwapo anayetuhumiwa ameishakamatwa na kama wanaotajwa kuwa washirika wake  wameishahojiwa. Kila simu hiyo ilipopigwa haikupatikana.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime naye ametafutwa kwa simu yake ya kiganjani lakini ilipokewa na msaidizi wake aliyesema yupo kwenye kikao atufutwe muda wa mchana na alipofutwa muda huo hakupokea simu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime

Badaaye alituma ujumbe wa maneno kwenye simu akitaka atumiwe ujumbe na alipotumiwa akiulizwa kuhusu sakata hilo hakujibu.

Haya yanaanza kuibuka huku kukiwa na tishio kubwa katika jamii la mmomonyoko wa maadili na hasa kuenea kwa kasi kwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja, vitendo vya ubakaji watoto wadogo, elimu ya ushoga kupenyezwa kwa njia ya haramu kwa wanafunzi na mapenzi kinyume na maumbile.

Serikali imekuwa katika mapambano makali dhidi vitendo hivi ingawa mtandao wa wanaoeneza vitendo hivyo unadaiwa kuwa na nguvu kubwa ya kifedha.

TANZANIA PANORAMA BLOG ITARIPOTI KWA KINA SAKATA HILI.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

2 COMMENTS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya