Wednesday, December 25, 2024
spot_img

BITEKO AZINDUA KITUO CHA KUPOZA UMEME IFAKARA

TERESIA MHAGAMA –

IFAKARA

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema kituo cha kupoza umeme kilichozinduliwa Wilaya ya Ifakara kitaboresha upatikanaji wa umeme.

Amesema kituo hicho kitachochea zaidi uwekezaji wa viwanda vya uongezaji thamani mazao ya kilimo na kitawezesha upatikani wa umeme wa uhakika kwenye taasisi za elimu zilizopo kwenye wilaya hiyo.

Biteko aliyasema hayo Mei 31, mwaka huu alipokuwa akizindua kituo kikubwa cha kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara (20MVA) kitakachokuwa kinahudumia wananchi wa Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga.

Alisema upatikanaji wa uhakika wa Nishati ya Umeme ni kipaumbele cha serikali kwa sababu inatambua kuwa umeme siyo anasa kwa watanzania bali hitaji muhimu.

Biteko alisema ujenzi wa mradi huo uliogharimu Shilingi bilioni 25 ulianza mwaka 2020. Gharama za mradi zilitolewa na serikali na Umoja wa Ulaya (EU).

Aliwataka watendaji wa REA kufanya kazi kwa ufanisi ili kufanisha lengo la serikali la kufikisha umeme wa uhakika kwa watanzania wote.

“Napenda kuwapa hamasa wote mnaohusika na Sekta ya Nishati, REA na Tanesco kuongeza nguvu ya utekelezaji wa miradi hii muhimu itakayochochea kukua kwa uchumi wa watu wetu na imarisheni usimamizi wa miradi hii ili iende sawa na thamani ya fedha zinazotolewa,” alisema Biteko.

Alisema kupatikana kwa umeme wa uhakika katika Wilaya ya Ifakara kutachochea uwekezaji ambapo viwanda 54 vya kuongeza thamani mazao vinatarajiwa kufunguliwa na ujenzi wa mgodi unaoendelea Wilaya ya Ulanga.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko (katikati) akizindua kituo kikubwa cha kupoza na kusambaza umeme cha Ifakara (20MVA) wilayani Kilombero mkoani Morogoro. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima na kushoto kwake ni Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Christine Grau (Picha na Teresia Mhagama)

“Serikali imeamua kujenga laini ya umeme kilomita 68, kupeleka umeme kwenye migodi hiyo kwa thamani Shilingi bilioni 104,” alisema Biteko.

Aidha, alisema serikali itafungua Ofisi ya Tanesco ngazi ya mkoa kwenye Kanda ya Morogoro Kusini ili kusogeza huduma zake kwa wananchi wanaotegemea kupata huduma kutoka Ofisi ya Mkoa iliyopo Morogoro Mjini.

Biteko aliishukuru Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kwa kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa mradi huo na kuiomba isaidie kuongeza transfoma nyingine eneo hilo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya, Christine Grau aliipongeza Wizara ya Nishati, REA, Tanesco na wakandarasi kwa kukamilisha mradi huo.

Alisema Tanzania na Umoja wa Ulaya zinashirikiana kwa muda mrefu kwenye masuala ya nishati kwasababu ndiyo injini ya kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.

Grau alisema mradi huo wa Ifakara utawezesha wananchi na taasisi kupata umeme wa uhakika na utasaidia wananchi kujiendeleza kiuchumi kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao yao.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu alisema REA ilijenga kituo hicho kwa kutambua kuwa eneo hilo ni la kimkakati kutokana na uzalishaji wa mpunga na migodi.

Alisema wateja 1858 wameunganishiwa umeme kupitia mradi huo katika vijiji nane vya Wilaya ya Kilombero. Mwisho.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya