RIPOTA PANORAMA
HUKUMU ya Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, Deo John Nangela (pichani juu) aliyekuwa akisikiliza kesi ya kibiashara namba 25 ya mwaka 2021 ambapo wadaiwa waliomba ajitoe kuisikiliza kwa sababu msimamo wake dhidi yao ulikuwa unajulikana inaeleza kuwa, mawakili wa washtakiwa walihoji mantiki ya kiutawala ya mahakama hiyo katika upangaji wa kesi.
Kwamba mawakili hao walisema tabia ya upangaji kesi nyingi, ikihusisha wahusika wale wale kwa Jaji yule yule inavuruga imani ya wadaiwa.
Jaji Nangela alitoa hukumu dhidi ya maombi yaliyowasilishwa na wadaiwa ambao ni Benki za Equity Tanzania na Equity Kenya katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara wakiomba ajitoe kusikiliza kesi namba 25 ya mwaka 2021 ambayo ilifunguliwa na Kampuni za TSN Oil Tanzania, TSN Supermakert, TSN Logistics na TSN Distributors Limited kwa sababu msimamo wake dhidi yao ulikuwa unajulikana.
Katika hukumu yake hiyo aliyoitoa Juni 30, 2023 akianza kwa kufafanua barua ya wadaiwa ya Mei 12, 2023 iliyopokelewa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara Mei 15, 2023 ya kuomba asijihusishe katika usikilizaji wa kesi namba 25 ya mwaka 2021, Jaji Nangela anaeleza kuwa barua hiyo ilifikishwa kwake siku ambayo mahakama ilipanga kutoa maagizo kuhusu uwasilishaji wa hitimisho baada ya kufunga usikilizaji wa kesi hiyo.
Jaji Nangela anasema alilazimika kusitisha mchakato kwa sababu wahusika wa kesi wanapaswa kusikilizwa kila wanapowasilisha suala ambalo mahakama inaitwa kuliamua na sababu ya pili ni mahakama ilikuwa haijatoa hukumu ya kesi hiyo.
Hukumu hiyo ya Jaji Nangela ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona inaeleza kuwa kuhusu uelewa kamili wa hitaji hilo zuri la msingi la haki ya asili, aliwaelekeza mawakili wasomi husika wa kesi hiyo kushughulikia mambo na wasiwasi uliotolewa na wadaiwa kwa kuuwasilisha kwa njia ya maandishi.
Wakili Emmanuel Saghan
Anasema wadaiwa waliokuwa wakiwakilishwa mahakamani na mawakili wasomi, Mpaya Kamara na Emmanuel Saghan waliwasilisha maandiko ya pamoja wakishughulikia mambo yaliyotajwa katika barua ya wadaiwa na wakiweka pingamizi kwenye vifungu vya 5 na 7 huku wakiacha vingine.
Kwamba kwa mujibu wa mawakili hao, suala la kuamuriwa kutokana na barua ya wadaiwa ni Jaji anayehusika kujitoa kwenye kesi hiyo.
Sehemu ya hukumu ya Jaji Nangela iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza, kwa tafasri isiyo rasmi ya lugha ya Kiswahili inasomeka; “Katika kushughulikia suala hili, Kamara na Saghan waliunga mkono msimamo wa washtakiwa kwamba, kama Jaji anayesimamia suala hili na masuala mengine ambayo washtakiwa ni wahusika ninapaswa kujiondoa kwenye usimamizi wa mashauri hayo.
“Msingi wa hoja za mawakili wasomi wa wadaiwa ni kwamba kujiondoa kwa Jaji kutoka katika usimamizi wa suala ambalo yeye ndiye anayesimamia si jambo jipya katika mamlaka yetu.
“Ili kuendeleza hoja yao kwa hatua zaidi, walidai kwamba mtu yeyote ambaye ni mhusika katika kesi au hata wakili anayemwakilisha mhusika huyo anaweza kumuomba Jaji anayesimamia kujiondoa kwenye usimamizi wa kesi hiyo.
“Mawakili wasomi waliegemea kwenye kesi ya Issack Mwamasika na wengine 20 dhidi ya Benki ya CRDB, marejeo ya kesi ya madai namba 6 ya mwaka 2016. Kutoka kwenye msingi huo na kama sababu ya maombi ya kukataa kwa wadaiwa ambayo mawakili wasomi wanaunga mkono kikamilifu, ilikuwa hoja yao kwamba maombi ya wadaiwa yanajitosheleza kwa sababu ya kesi nyingi ambazo Jaji wa kesi anaendesha zinazowahusisha wadaiwa. Mawakili wasomi walisema kwamba wateja wao wameibua maswali mengi katika akili zao na imani yao imepungua.
“Ili kuthibitisha hoja yao iliyotolewa kwanza, kwamba Mheshimiwa Nangela aliongoza kesi ya kibiashara namba 105 ya mwaka 2021 kati ya NAS Hauliers na wengine 20 dhidi ya Benki ya Equity (T) Ltd na Benki ya Equity (K) Ltd na kutoa uamuzi dhidi ya wadaiwa na pili kwamba mheshimiwa pia anaongoza kesi ya kibiashara namba 103 ya mwaka 2022 iliyowasilishwa na ZAS Investment dhidi ya Benki za Equity (T) Ltd na Equity (K) Ltd na tatu mheshimiwa sasa anaongoza kesi hii ya kibiashara namba 25 ya mwaka 2021 kati ya TSN Oil (T) Ltd na wengine 30 dhidi ya Benki za Equity (T) Ltd na Equity (K) Ltd.
“Kulingana na hali hizo za kimazingira, mawakili wa wadaiwa walihoji mantiki ya kiutawala ya mahakama hii ya upangaji wa kesi na walisema kwamba tabia ya upangaji kesi nyingi sana ambayo inahusisha wahusika wale wale kwa Jaji huyo huyo inavuruga imani ya wadaiwa.”
Tanzania PANORAMA Blog inaripoti hukumu hii na nyingine zilizoibua mjadala mkubwa kwenye jamii kuhusu kampuni zinazodaiwa kukopa mabilioni ya fedha kwenye benki za ndani kisha kukataa kulipa kwa kukimbilia mahakamani.
Farouq Baghoza
Katika andiko la hivi karibuni lililosambaa kwenye mitandao ya kijamii, inadaiwa TSN Group ilikopa Shilingi bilioni 15 kutoka Benki ya National Macro finance Bank (NMB) na Shilingi bilioni 80 kutoka Benki ya Equity kwa utaratibu wa kudhaminiwa (latter of credit); fedha ambazo imekataa kulipa kwa kukimbilia mahakamani ambako ilipewa ushindi.
Tanzania PANORAMA Blog imemfikia bosi wa TSN Group, Farouq Baghoza kwa simu yake ya kiganjani kumuuliza kuhusu jina lake kutajwa kwenye skandali hiyo lakini ‘alikacha’ kujibu swali hilo.
Baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti skandali hiyo vilieleza kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara aliyesimamia na kuhukumu kesi ya TSN Group dhidi ya Benki ya Equity na kesi nyingine za wafanyabiashara waliokopa benki kisha kukataa kulipa mikopo hiyo kwa kukimbilia kwenye mahakamani hiyo amehamishwa.
Inadaiwa, baadhi ya wafanyabiashara hao wanaichafua mahakama kwa kutamba kuwaweka mifukoni baadhi ya majaji na pia kwamba hakuna wa kuwafanya lolote hapa nchini.
Katika mitandao ya kijamii ambako kumekuwa na mjadala mkubwa tangu kuibuliwa kwa skandali hii, baadhi ya wachangiaji wanaeleza kuwa kuna kundi la wafanyabiashara wanaotumia kigezo cha wawekezaji wa ndani wanaofilisi benki za ndani kwa kukopa mabilioni ya fedha kisha kukataa kulipa.
Kwamba kundi hilo la wafanyabiashara ndiyo chanzo cha deni la taifa kupaa kwa kiwango kikubwa na baya zaidi, wafanyabiashara hao wanahusishwa na baadhi ya viongozi waandamizi serikalini.