Monday, December 23, 2024
spot_img

BOSS TSN ‘AKACHA’ KUJIBU SKANDALI YA MKOPO WA MABILIONI

RIPOTA PANORAMA

MMILIKI wa makampuni ya TSN, Farouq Baghoza (pichani hapo juu) ‘amekacha’ kujibu madai yanayoelekezewa kampuni anazozimiliki kukopa mabilioni ya fedha kutoka benki za ndani kisha kukataa kulipa kwa kukimbilia mahakamani.

Baghoza aliulizwa jana na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu jina lake kutajwa moja kwa moja kwenye skandali hiyo katika andiko lililosambazwa mitandaoni na kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni kisha kuibua mjadala mkubwa katika jamii.

Baghoza alipigiwa simu akapokea na kuelezwa kuwa anazungumza na mwandishi wa Tanzania PANORAMA Blog aliyemuomba ushirikiano wa kujibu maswali aliyokuwa nayo, lakini alipoulizwa kuhusu jina lake kutajwa moja kwa moja kweye skandali hiyo, alisema anapanda ndege kuelekea Dodoma hivyo apigiwe simu saa 10 jioni atakuwa kafika.

“La, umesema Tanzania PANORAMA Blog, aisee, sasa napanda ndege kuelekea Dodoma baada ya muda mfupi tu nitakuwa nimefika, nipigie saa 10 jioni nitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kujibu swali hilo,” alisema Baghoza.

Alipopigiwa simu saa 10 jioni, simu yake iliita bila kupokewa na alipopigiwa tena na tena, Baghoza alikuwa akikata simu.

Leo Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta tena Baghoza kwa kumtumia ujumbe wa maneno kwenye simu yake ya kiganjani  ikimkumbusha kujibu swali aliloulizwa, aliusoma lakini hakujibu chochote.

Makampuni ya TSN yanadaiwa kukopa Shilingi bilioni 15 kutoka Benki ya NMB na Shilingi bilioni 80 kutoka Benki ya Equity kwa utaratibu wa kudhaminiwa na Benki hizo (letter of credit) kisha ilikataa kulipa mikopo hiyo.

Inadaiwa TSN ilikwenda mahakamani kupinga kulipa mikopo hiyo ambako ilitetewa na wakili mmoja maarufu na ambaye naye anadaiwa kutetea makampuni kadhaa yaliyokopa kwenye benki za ndani kisha kukataa kulipa mikopo kwa kukimbilia mahakamani.

Inadaiwa zaidi kuwa kesi nyingi za kampuni zilizokopa mabilioni ya fedha kwenye benki za ndani zimekuwa zikisikilizwa na jaji mmoja wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara ambaye amekuwa akitoa hukumu zinazofanana kwenye kesi hizo.

Mikopo inayodaiwa kuchukuliwa na makampuni ya TSN na mengine ikiwemo kampuni ya Kahama Oil Mills Limited ambayo inadaiwa kuchukua mikopo ya mabilioni ya shilingi kwenye benki tatu tofauti kisha kukataa kulipa kwa mtindo ule ule wa kukimbilia mahakamani ni moja ya sababu za kupaa kwa deni la taifa.

Tanzania PANORAMA Blog kesho itaanza kuripoti hukumu ya kesi hizo ambazo zimeibua mjadala mkubwa katika jamii, ikianza na hukumu ya jaji aliyekataa kujitoa kwenye kesi kati ya makampuni ya TSN na Benki ya Equity. Na aidha, itaripoti kwa kina jinsi mikopo hiyo ilivyochukuliwa na kampuni hizo kabla ya kudaiwa kukataa kulipa kwa kukimbilia mahakamani.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya