Monday, December 23, 2024
spot_img

CCM YAMSHAMBULIA MPINA HOJA YA UCHUNGUZI KIFO CHA RAIS MAGUFULI

RIPOTA PANORAMA

MWENENDO wa mambo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu siyo shwari baada ya Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kulieleza Bunge haja ya kuundwa kwa Tume Huru ya uchunguzi itakayochunguza alichokisema utata wa kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Pombe Magufuli.

Mpina, pia amelieleza Bunge kuwa Tume Huru ya uchunguzi, itabaini watu waliokataa kuapishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Tanzania, kama yalivyo matakwa ya kikatiba.

Aliyasema hayo Aprili 19, 2024 bungeni Dodoma, alipokuwa akichangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Siku chache baada ya Mpina kutoa kauli hiyo bungeni, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shamsa Mohamed akiwa katika mkutano wa ndani na wana CCM wa Itilima mkoani Simiyu, alimshambulia kwa maneno makali kuwa ameshindwa kutekeleza majukumu yake ya kibunge na badala yake anafanya siasa za majitaka na kuchafua viongozi wa kitaifa.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu, Shamsa Mohamedi

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Itilima wakimsikiliza Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Simiyu, Shamsa Mohamed (hayupo pichani) alipokuwa akiwahutubia wilayani humo, hivi karibuni

Akizungumza na wana CCM hao, Shamsa alisema wananchi wa Jimbo la Kisesa wanalia kwa sababu wana changamoto nyingi lakini Mpina haonekani na kwamba hajapata kukanyaga kwenye baadhi ya maeneo ya jimbo lake tangu alipochaguliwa miaka miatano sasa.

Shamsa alimshambulia Mpina kwa kushindwa kushughulikia kero za wananchi wa jimbo lake na badala yake anahangaika kutafuta sababu za kifo cha Rais Magufuli.

Alisema, “wabunge wangu wa Mkoa wa Simiyu wakafanye yale wananchi waliyowatuma. Waachane na siasa za maji taka za kuchafua viongozi wa kitaifa hali ya kuwa wananchi waliokutuma ukawatatulie maendeleo huyapeleki wala hawakuoni jimboni.

“Jana nimetoka Tarafa ya Kisesa, Jimbo la Kisesa, wananchi wanalia kwa sababu wana changamoto nyingi, Mbunge wao haonekani. Toka wamemchagua miaka mitano sehemu zingine hajawahi hata kufika, hata kukanyaga.

“Mtafute mbunge yuko wapi, yupo anahangaika na kifo cha Magufuli badala ya kuhangaika na matatizo ya wananchi akayapambanie bungeni, yupo anahangaika kutafuta sababu ya kifo cha Magufuli,” alisema.

Akiendelea, Shamsa alihoji kama kuna mtu anayeweza kusema sababu ya kifo zaidi ya Mungu anayejua siku na saa ya kifo cha mwanadamu.

Akimlenga moja kwa moja Mpina, alisema amekuwa akisema mawaziri hawafai wakati yeye alipokuwa waziri alikuwa hawasalimii wananchi na alihoji alichosaidia Mpina kwenye Mkoa wa Simiyu wakati akiwa waziri.

Wananchi wa Jimbo la Kisesa wakiwa wenye furaha wakimvika vazi la jadi mbunge wa jimbo hilo, Luhaga Mpina katika moja ya mikutano ya kisiasa na kukutana na wapigakura ya mbunge huyo.

Sehemu ya maneno ya hotuba hiyo inasema; “Na alitusaidia nini wana Simiyu akiwa waziri. Arudi jimboni akatatue kero za wananchi. Wananchi wake wana maboma hayajaisha, yanahitaji fedha. Wananchi wake wanateseka na tembo, aende akapambane na Waziri wa Maliasili wananchi waache kuteseka. Asiende kupambana na mipango ya Mwenyezi Mungu anapochukua watu wake.

“Mbunge akishirikiana na chama na mwenyekiti wa mkoa tukaenda kupambania maendeleo ya wananchi yatatufikia. Wana Kisesa wanasikitika sana na jana walikuwa wanasikitika kwa sababu yale waliyomtuma haendi kuyatekeleza na kuna sehemu nyingine hawezi hata kukanyaga. Mimi ndiye mwenyekiti wake wa mkoa, hakanyagi kwa wananchi kule, watamzomea.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akiwa katika moja ya mikutano yake ya kisiasa uliokuwa umefurika mamia ya wananchi.

“Badala ya kutengeneza siasa yako ya jimbo unakwenda kutengeneza siasa ya kutukana viongozi wa kitaifa kwa sababu wewe, si uhame sasa Kisesa…. kitaifa kule ili wananchi wa Kisesa wachague mtu mwingine wa kuwaletea maendeleo.

“Si hivyo wana Itilima. Nayasema haya kwa sababu nina uchungu. Ulipewa uwaziri, kipi kizuri ulichokifanya wewe kuanzia kwenye mkoa, kwenye wilaya yako husika. Ni mbunge anayeongoza hata kwa kutokushiriki vikao vya chama, ni mbunge anayeongoza hata kwa kutokwenda kwa wananchi wake kuwasikiliza.

“Kila siku yupo kwenye magazeti, yupo kwenye vyombo vya habari. Inasikitisha sana. Unakwenda kuhoji bungeni kifo cha mtu aliyetangulia mbele ya haki, ndicho wananchi walikutuma?”

ALICHOKISEMA MPINA KUHUSU KUUNDWA TUME HURU YA KUCHUNGUZA KIFO CHA RAIS MAGUFULI

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akizungumza bungeni

Akichangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora 2024/2025 bungeni, Dodoma na kurejea kauli yake hiyo nje ya Bunge alipozungumza na waandishi wa habari, Mpina alisema kauli iliyotolewa na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo, Machi 16, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kifo cha Rais Magufuli na yaliyojiri bada ya kifo hicho, imemshawishi kulishawishi Bunge liruhusu kuundwa Tume Huru ya kuchunguza utata wa kifo hicho.

Kwa maneno yake mwenyewe, alisema; “Baada ya kusikiliza kwa kina maelezo ya Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo aliyoyatoa Machi 16, 2024 nimeshawishika na ninawashawishi wabunge wenzangu kuruhusu kuunda Tume Huru ya kuchunguza utata wa kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Joseph Magufuli ili kumtenda haki.

“Lakini na watu wengine waliotajwa, aidha kwa wema au kwa ubaya katika suala hili linalohusiana na kifo cha Magufuli. Tume hiyo itabaini pia hata watu waliokataa kuapishwa kwa Rais Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati lilikuwa takwa la kikatiba.

“Kwa mambo yaliyosemwa, tena na taasisi ambayo siyo ya kutiliwa mashaka. Na mtu ambaye siyo wa kutiliwa mashaka, kuna haja ya hii tume kuundwa na hii itatuletea taarifa zote za mambo yaliyopo katika hili jambo au utata wa kifo cha Rais Magufuli.

“Tumefanya makosa mengi sana katika mfumo wetu wa utumishi wa umma na katika mfumo wetu wa utawala bora.

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea heshima ya kijeshi muda mfupi baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania Ikulu, Dar es Sar es Salaam. pembeni yake ni Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenetali Venance Maboye na mpambe wake, Kanali Nyamburi Mashauri.

“Ni muda muafaka sasa wa kurekebisha kasoro hizo na kutengeneza taifa lenye misingi mizuri ya utawala bora, misingi ya utawala wa sheria, misingi ya kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kulifanya taifa letu lionekane mbele ya mataifa kwamba tulishaamua kujenga taifa la kizalendo, lenye mafanikio makubwa.

KAULI YA JENERALI MABEYO KUHUSU KIFO CHA RAIS MAGUFULI

Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo.

Jenerali Mabeyo alifanya mahojiano na waandishi wa habari wa Gazeti la Serikali la Daily News, Machi 17, 2024; siku ambayo Tanzania iliadhimisha miaka mitatu ya kifo cha Rais Magufuli.

Katika mahojiano hayo, Jenerali Mabeyo alizungumzia hali ilivyokuwa saa 24 kabla ya kifo cha Rais Magufuli, kilichojiri baada ya Rais Magufuli kukata roho na yaliyotokea saa 40 kabla Rais Samia kuapishwa kuwa Rais.

“Wakati anaugua sisi tulishirikishwa kama vyombo vya ulinzi na usalama, tujue hali ya Mheshimiwa Rais inakwendaje. Na wakati wote tulikuwa tunakwenda kumuona, asubuhi na jioni kwa hiyo tulikuwa na nafasi yetu na sisi kama wakuu wa vyombo.

“Na mimi nikiwa kama mwenyekiti wao wa wakuu wa vyombo, lazima tunashauriana tunafanyaje. Baadaye tukampeleka Mzena, pale kidogo kulikuwa na utulivu. Si watu wengi wanaweza kuingia kule, wachache wanaweza kuingia lakini hata hivyo tuliwe limit namba ya watu ili awe na nafasi ya kupumzika vizuri. Kwa hiyo matibabu yakahamia pale na madaktari wote walipelekwa pale kumwangalia wakati wote.

“Siku moja kabla ya kifo chake, hali ilibadilika kidogo. Na yeye alijitambua kwamba hali imebadilika na nadhani alijua, Mwenyezi Mungu alimuongoza kwamba hatapona.

“Alichosema, nirudisheni nyumbani, nikafie nyumbani. Tukasema mheshimiwa hapana. Hapa upo kwenye mikono salama, madaktari wapo waendelee kukutibu.

“Niseme jambo ambalo labda halikuwahi kusemwa huko nyuma kwa sabahu nilikuwepo pale, aliniita CDF njoo. Akaniambia, siwezi kupona, waamuru hao madaktari wanirudishe nyumbani. Nikamwambia mheshimiwa sina mamlaka hayo.

“Akasema yaani CDF unashindwa kuwaamuru madaktari wanirudishe nyumbani, nikamwambia suala la afya siyo la CDF, mheshimiwa naomba ubaki utulie, madaktari watatuambia.

“Siku hiyo hiyo, baadaye alipoona kwamba nimekuwa na msimamo huo akaniambia niitieni paroko wangu, Paroko wa Oysterbay au St,. Peter’s, alikuwa anaitwa Father Makubi, lakini akaongeza akasema namuomba Kardinali Pengo naye aje.

Kardinali Polycarp Pengo

Hayati Rais John Magufuli akiwa na Padre. Dk. Alister Makubi

“Hiyo ni asubuhi sasa, kesho yake asubuhi. Tukamtafuta Kardinali Pengo alikuwa kwenye ibada, hakupokea, akaniuliza CDF hujampata Pengo? Nikamwambia yupo kwenye ibada baba atakapotoka atakuja, tumeishampelekea na dreva wa kwenda kumchukua, akanyamaza.

“Kwa hiyo wakaja wote, Kardinali Pengo na Father Makubi wameongozana. Sasa katika taratibu za kikatoliki wanamsalia pale ibada na kumpa Sakramenti ya upako wa wagonjwa, aliyekuwa katika hatari ya kufariki. Walipomaliza kumsalia akapumzika.

Hayati Rais John Pombe Magufuli

“Lakini ilipofika saa 8 mchana wakatupigia watu wa hospitali, wakanipigia mimi kama Mkuu wa Majeshi, wakampigia DGIS na IGP. Hali ya mheshimiwa siyo nzuri sana, hebu njooni

Profesa Lawrence Maseru

Profesa Mohamed Janabi

“Tukaenda kule tukakuta ametulia lakini alikuwa hawezi kuongea tena. Tukaendelea pale tunasubiri, tukawaita sasa madaktari wengine. Nakumbuka tulimwita Profesa Maseru, Profesa Janabi alikuwapo muda wote naye aliongezea nguvu yule, wakajaribu kumuhudumia pale wakasema ngoja tuangalie, tukaendelea kukaa mpaka jioni.

“Ilipofika jioni saa 12.30 hivi au saa moja kasoro, akakata roho. Wakuu wa vyombo tupo pale, sisi watatu. Mimi, IGP na DGIS,” Jenerali Mabeyo aliyasema hayo katika mahojiano yake na waandishi wa habari.

Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo

Mkurugenzi wa Idara Usalama (DGIS) Mstaafu, Diwani Athuman

Inspekta Jenerali (IGP) Mstaafu, Simon Sirro.

Akizungumza kuhusu kilichotokea baada ya kifo cha Rais Magufuli, Jenerali Mabeyo alisema baada ya Rais Magufuli kukata roho, yeye na makamanda wenzake walianza kupanga mikakati ya kufanya. Kwa maneno yake mwenyewe, alisema;

“Tulianza kustrategie’s tufanye nini, nani wa kumtaarifu wa kwanza. Makamu wa Rais wakati huo hayupo Dar es Salaam, alikuwa Tanga. Waziri Mkuu hakuwa Dar es Salaam, nadhani alikuwa Dodoma au somewhere else.

“Katibu Mkuu Kiongozi naye hakuwepo Dar es Salaam, naye alikuwa Dodoma. Kwa hiyo tuliokuwa Dar es Salaam tulikuwa watatu tu.

“Tukasema kwa kuwa Makamu wa Rais yupo Tanga, hebu tumwambie kwanza Waziri Mkuu na Katibu Mkuu kiongozi waje bila ku-disclose. Kwa hiyo tukamuomba Waziri Mkuu aje na Katibu Mkuu Kiongozi.

“Bahati nzuri wakaja mapema. Sasa mimi kama mwenyekiti wa wakuu wa vyombo, nilipaswa ku-disclose. Mheshimiwa Rais ameishatutoka. Kwa hiyo tukaanza kushaurina tunafanyaje? Nani anatakiwa atangaze hizi habari kwenye vyombo vya habari wananchi wajue.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Bashiru Ali

“Ndiyo tukaanza kutafuta Katiba sasa inasema nini. Mtu pekee anaweza kutangaza kwenye vyombo vya habari ni Makamu wa Rais. Yeye yuko Tanga, tunamwambiaje? Tunampigia simu au tunamwambiaje. Ikabidi yafanyike mawasiliano mengine kumweleza akiwa Tanga.

“Lakini kabla ya kutangaza tukasema familia yake haijui. Mke wake yupo hapa Ikulu, hajajua. Mama yake anaumwa yupo Chato, hajaambiwa. Hatuwezi kumwambia kwa simu, nani anakwenda kumwambia mama? Mke wake. Anafikishaje ule ujumbe.

“Bahati nzuri tukawapa watu pale wakaenda kule na mwingine kwenda Chato. Tukatafuta cherter plane, kabla ya kutangaza kwenye vyombo vya habari wale wawe wameishapata taarifa, wasipate taarifa kupitia vyombo vya habari.  Ndiyo maana toka saa 12.30 ilikuja kutangazwa saa 5.30.

KUCHELEWA KUMWAPISHA RAIS SAA 48 KINYUME CHA KATIBA.

Jenerali Mstaafu Mabeyo alizungumzia pia sababu ya kuchelewa kuapishwa kwa Makamu wa Rais wa wakati huo, Rais Samia, kuwa Rais, alisema;

Rais Samia Suluhu Hassan akiapa kuwa Rais.

Task kubwa, namna ya kumwapisha Rais… aapishwe Rais baada ya kuzika au aapishwe kabla ya kuzikwa, nayo ilikuwa kidogo kuna kamjadala lakini logic ikaja kwamba kuna marais wengine watatoka nje ya nchi kuja kumzika mwenzao. Watapokelewa na Makamu wa Rais au na Rais. Lazima awepo Rais.

“Ndiyo maana tukafikia maamuzi kwamba Makamu wa Rais aapishwe kama Rais. Nadhani ndiyo maana zilipita siku mbili. Kikatiba haitakiwi, within 24 hour’s ilitakiwa awepo. Sasa 17, 18 ikapita 19 ndiyo alikuja kuapishwa, kulikuwa na majadiliano hapo lakini tunashukuru Mungu amelikubali.

“Lakini namna ya kumwapisha nako kukawa na mjadala, tunamwapishaje? Wengine wakasema isiwe ni ceremony wengine wanasema iwepo. Sasa mimi kama Mkuu wa Majeshi nilichosema ni kwamba paredi lazima iwepo, Bendera ya Amiri Jeshi Mkuu lazima ipande kwa gwaride, lakini kidogo kulikuwa na kamvutano kwamba tupo kwenye msiba, hakuna paredi wala nini na nini.

“Nikasema huyu ni Amiri Jeshi Mkuu anayeapishwa. Asipoapishwa kwa taratibu hizo za kitaifa, jeshi halitamtambua, hatuna Amri Jeshi. Kwa hiyo tukamaliza.

Jenerali Mstaafu Mabeyo alizungumza pia kuhusu Rais Samia kuitwa Amirat au Amiri Jeshi Mkuu, alisema; “Sisi tuliwambia jeshini hatuna mwanamke, jeshini tuna afisa na askari. Hakuna mwanaume na mwanamke, kwa hiyo hata Amiri Jeshi neno lile litabaki kuwa Amiri Jeshi, ni Commanding Chief. Hiyo Amirat ni kiongozi wa dini.

“Tukawauliza na BAKITA wakaeleza tu vizuri maana ya Amirat ni nini, basi tukasema tuendelee hapo hapo. Mimi ilibidi niseme pale pale, kulikuwa na kamjadala kwamba ni Amirat, nikasema hapana, ni Amiri Jeshi Mkuu.”

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya