RIPOTA PANORAMA
RUMANYIKA ORUGUNDU, alikuwa Mtemi wa Kabila la Wanyambo aliyetawala Himaya ya Karagwe, mahali ilipo Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe, kuanzia mwaka 1855 hadi 1882.
Mtemi Rumanyika alikuwa mtu hodari na aliheshimika sana katika jamii ya Wanyambo kutokana na uwezo wake wa kiuongozi na uhodari wake katika medani za kivita. Katika kipindi cha takribani miaka 30 ya utawala wake, aliwaongoza Wanyambo kuvuka vipindi vigumu vya njaa na kupigana vita na maadui zao.
Historia inamtaja Mtemi Rumanyika kama kiongozi wa Himaya ya Karagwe aliyepigana na kushinda vita alizoongoza za kulinda ardhi yenye rutuba na msitu wa kiasili wa kiikweta, mahali ilipo Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe.
Kutokana na uongozi wake mzuri na jinsi alivyowaongoza watu wake kukabiliana na nyakati ngumu, yakiwemo majanga mbalimbali, mwaka 2019, Serikali ilipoipandisha hadhi Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe, jina lake lilipewa heshima ya kutumika kuitambulisha hifadhi hiyo.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Charles Ngendo ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe, katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni kuhusu ustawi wa shughuli za utalii katika hifadhi hiyo anasema dunia bado haijatolewa tongotogo za macho ili kuweza kuona Bioanua za aina mbalimbali zilizopo Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe.
Anaanza na historia ya eneo ilipo hifadhi hiyo akieleza kuwa, historia ya uhifadhi Tanzania imepitia vipindi tofauti, ikianzia enzi za utawala wa machifu uliohifadhi na kulinda maeneo yenye maumbile ya kidunia ya kipekee kwa taratibu za mila na desturi na ilipobidi hata kwa kupigana vita na maadui waliotaka kuyavamia maeneo hayo na kuyaharibu.
Kamishna Msaidizi Ngendo anasema historia ya uhifadhi Tanzania inaonyesha kuwa wakati wa utawala wa kikoloni, watawala hao walitumia sheria kuhifadhi maeneo muhimu na baada ya Tanzania kupata uhuru yaliendelea kutunzwa.
Anasema Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe ni miongoni mwa Hifadhi za Taifa tano zilizotangazwa mwaka 2019. Ilitangazwa kwa tangazo la Serikali nambari 510 na ilianzishwa rasmi Julai 5, 2019 ikiwa karibu sana na Hifadhi ya Taifa ya Ibanda – Kyerwa.
“Hifadhi hii ipo Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Kyerwa na ni miongoni mwa Hifadhi za Taifa 21 zilizo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
“Kabla Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe kupandisha hadhi, ilikuwa pori la akiba likisimamiwa na Mamlaka ya Uhifadhi Wanyamapori (TAWA) na kabla ya kuwa pori la akiba, eneo hilo lilihifadhiwa kwa taratibu za mila na desturi za wenyeji ambao ni Wanyambo,” anasema.
Kamishna Msaidizi Ngendo anasema Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe ni ya kipekee ikiwa na milima yenye misitu ya Kiikweta ambayo inahifadhi bioanua za aina mbalimbali na Bonde la Kishanda lenye maziwa makubwa matano yanayohifadhi viumbe wa majini na kutiririsha maji yake kwenye maziwa na aridhi oevu. Maji ya maziwa hayo hutiririka hadi Mto Kagera ambao nao hutiririsha maji kwenye Ziwa Victoria.
Ziwa Victoria
Anasema ni eneo lenye maumbile ya kidunia ya kipekee likiwa na milima na mabonde na mandhari nzuri zinazovutia kuangalia. Ni makazi ya aina mbalimbalia za wanyama na uoto wa asili. Imepambwa na maeneo ya tambarare za ukanda wa chini, miti ya aina mbalimbali na nyasi ndefu.
Hifadhi hiyo ni makazi ya wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo nyati, sitatunga, nyani, chui, digidigi, mbweha, pongo, nguchiro, tumbili na wengineo.
Mbweha
Nguchiro
Anataja pia uwepo ndege wa majini, nchi kavu na msituni ambao ni adimu sana duniani wanaopatikana kwenya hifadhi hiyo yenye maziwa ya Kabugwe, Kamuzinzi, Mkashambya, Mkanyasi na Mrundana ambayo hufanya eneo la hifadhi kuwa la kuvutia zaidi.
“Maziwa matano yaliyopo hifadhini yanaipa thamani kubwa kwani ndiyo ambayo tunatarajia yatatumika zaidi katika shughuli za utalii wa uvuvi baada ya mikakati iliyopo sasa ya kuboresha shughuli za utalii na ujenzi wa miundombinu kwenye hifadhi kukamilika.
“Ni maziwa yenye mandhari nzuri kwa maana ya mwonekano wake. Maziwa yote yana mandhari ambazo zinatofautiana na pia uwepo wa maziwa hayo yanafanya wanyama waliopo kuwa na uhakika wa kupata maji misimu yote tofauti na hifadhi zilizo maeneo ambayo yana ukame,” anasema Kamishna Msaidizi Ngendo.
Anasema eneo la Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe lina misimu miwili ya mvua, wa kwanza ukianza mwezi Machi hadi Mei na msimu wa pili wa mvua huanzia mwezi Septemba hadi Disemba.
“Mvua za muda mfupi za vuli huanza kunyesha Novemba hadi Disemba na mvua za muda mrefu wa masika huanza Machi hadi Mei. Maeneo haya yanapata wastani wa mvua za mililita 729 hadi 995 kwa mwaka na hali ya joto ni ya wastani wa nyuzi joto 13 hadi 26. Muda mzuri wa kutembelea hifadhi ni mwezi Januari hadi Februari na Juni hadi Agosti.
Akizungumzia ustawi wa hifadhi hiyo katika kipindi cha miaka takriban sita sasa tangu ilipoanzishwa, Kamishna Msaidizi Ngendo anasema Serikali kupitia TANAPA imeelekeza nguvu kuimarisha miundombinu ya hifadhi ili kuifungua iweze kufikika maeneo yote hivyo kutoa nafasi nzuri kwa watalii kuitembelea.
Kamishna wa Uhifadhi (CC) wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Juma Kuji
Anasema TANAPA inalenga kurahisisha utalii kwenye Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe kwa kujenga barabara za ndani na nje ya hifadhi na kwamba kazi hiyo inasimamiwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mhandisi Mshauri, Richard Matolo (Phd) na hatua ya sasa inayotekelezwa ni kuimarisha miundombinu ya barabara zilizopo kabla ya kuanza kujenga mpya.
“Hifadhi hii bado changa. Kazi kubwa inapaswa kufanyika ili iweze kufikika pande zote na tunashukuru uboreshaji miundombinu ya utalii na hasa barabara za ndani ya hifadhi ili kurahisha utalii wa kutembea kwa miguu ambao umepewa kipaumbele chini ya usimamizi wa Kamishna Msaidizi Dk. Matolo. Kazi inafanyika inaonekana.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mhandisi Mshauri, Dk. Richard Matolo
“Sisi wasimamizi wa hifadhi hii tunasimamia maelekezo ya Kamishna wa Uhifadhi, Juma Kuji kwa umakini mkubwa. Amekuwa akisisitiza kuwa kila mhifadhi atembee chini ya unyayo wa mama (Rais Samia Suluhu Hassan) katika kazi zake ili tufikie lengo lililowekwa. Tunakwenda hivyo licha ya changamoto za kifedha zinazokwamisha baadhi ya utekelezaji wa miradi maana kama mnavyofahamu siku hizi fedha ni lazima itoke hazina, sasa zinapotokea changamoto za dharura kwa kazi yetu hii inakuwa tabu kidogo lakini tunasonga mbele,” anasema.
Kamishna Msaidizi Ngendo anasema katika Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe kuna maeneo matatu ambayo yametengwa kwa ajili ya uwekezaji wa kujenga hoteli na nyumba za muda.
Anasema menejimenti ya hifadhi inashirikiana kwa karibu na TANAPA kuvutia watalii wa ndani wakiwemo wanafunzi ambao kwao kutembelea hifadhi hiyo ni kwenda kujifunza zaidi badala ya kutalii tu.
Na ili kufanikisha hilo, anasema mikakati iliyopo sasa ni kuwasiliana na mawakala wa utalii (tour operator) wanaoleta watalii kwenye Hifadhi za Taifa zilizopo kaskazini mwa nchi ambako shughuli za utalii zimestawi kwa kiwango kikubwa ili wavutike kupeleka watalii hifadhi zilizo Kaskazini Magharibi.
Anasema kuna mawakala wa utalii wachache katika Mji wa Bukoba wanaowahamasisha waanzishe utaratibu wa kuleta watalii moja kwa moja kutoka katika maeneo yaliyo jirani na hifadhi na kwamba mwitikio ni mzuri ingawa kampuni hizo bado changa.
Pia anasema hifadhi inashiriki maonyesho mbalimbali kwa ajili ya kuvutia wawekezaji hasa wa kitanzania na kutoka nje kwenda kuwekeza kwenye Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe.
Wanyambo wakicheza ngoma ya asili ya Amakondore
Kamishna Msaidizi Ngendo anasema Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe inafikika kutoka pande zote za nchi kwani serikali imeboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu ya usafiri.
Anasema mtalii anaweza kufika Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika – Karagwe kwa njia ya barabara akitokea Mji wa Bukoba hadi Omrushaka kisha anaingia eneo la Nyakatundu, yalipo makao makuu ya hifadhi. Barabara hiyo ina urefu wa kilometa 185.
Sitatunga
Digidigi
Njia nyingine anayoitaja ya kufika kwenye hifadhi hiyo ni barabara inayopita Mji wa Kayanga hadi lango la Nyakatundu na au mtalii anaweza kupitia Uganda au Rwanda ambako atavuka mpaka wa kimataifa wa Kikagati/ Murongo uliopo umbali wa kilomita nane kabla ya kuingia lango la Rugasha.
Mtalii anaweza pia kutumia usafiri wa anga ambapo atatua Uwanja wa Ndege wa Bukoba kisha atasafiri kwa njia ya barabara hadi hifadhini.