Monday, December 23, 2024
spot_img

KKKT MWANZA KWAFUKUTA

MWANDISHI wETU

KUNA mgogoro mkubwa unaofukuta ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria, kati ya Askofu Andrew Gulle na baadhi ya vigogo waandamizi wa kanisa hilo, wanaopanga njama za kutaka kumng’oa mamlakani.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Mwanza, vigogo wanaopanga njama za kumng’oa Askofu Gulle, wanaotumia hoja ya wanachoita, “madhaifu ya Katiba ya KKKT,” kumshinikiza kustaafu kabla ya muda wake.

Walioko kwenye mkakati wa kumg’oa Askofu Gulle, wanadai kuwa wanaungwa mkono na Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Dk. Alex Malasusa. Mtandao huu, umeshindwa kumpata Askofu Dk. Malasusa kupata maoni yake.

Lakini Moses Lauwo, aliyejitambulisha kama mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo anasema: “Wapendwa Bwana Yesu apewe sifa! Nimelazimika kutoa ufafanuzi juu ya barua hii iliyosomwa kanisani Jumapili ya jana (Jumapili iliyopita).

Barua hii ni kwa mujibu wa mapatano yetu na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Alex Malasusa. Kwa mujibu wa barua hii:

Askofu Andrew Gulle

1. Askofu Gulle alianza likizo yake tangu tarehe 21/4/2023 na atamaliza likizo yake tarehe 28/7/2024

2. Mkutano mkuu utafanyika tarehe 26/7/2024. Kwa sababu hiyo Gulle hatakuwepo wakati wa mkutano mkuu.

3. Gulle atarejea tarehe 28/7/2024 na amepewa siku mbili za kukabidhi ofisi kwa askofu mteule ambaye atachaguliwa wakati wa mkutano mkuu wa tarehe 26/7/2024

4. Tangu tarehe 21/4/2024 Gulle haruhusiwi kuingia ofisini kwa shughuli za kiofisi wala kufanya shughuli zote za kiaskofu.

5. Kwa mujibu wa mapatano yetu, safari zozote atakazofanya Gulle, hazitagharimiwa na Dayosisi na wala marafiki wa Dayosisi yetu.

Kwa nini tulifikia patano la kukubaliana na wazo la kustaafu kwake:

  • Mchakato wa kumfukuza ungechukua muda mrefu. Kwa mujibu wa katiba yetu, mchakato huu unatoa maelekezo ya kuunda tume ya uchunguzi ambayo itaongozwa na Askofu atakayeteuliwa na Mkuu wa KKKT. Wajumbe wengine wa tume ni Katibu Mkuu, afisa mwajiri ambaye shemeji yake na wajumbe wengine ambao kwa sehemu kubwa ni wateule wa Gulle mwenyewe.
  • Kutokana na muundo wa tume ya uchunguzi, tume ingemaliza kazi yake baada ya miezi sita
  • Aidha, kutokana na muundo wa tume, ingekuwa rahisi kumsafisha Gulle. Kumbukeni kwamba ukipambana na aliyeshika mpini, ni vigumu mno kushinda kesi hiyo. Aidha kutokana na muda mrefu wa tume yenyewe, wengi tungekata tamaa.
  • Kwa muda wote wa uchunguzi, Askofu Gulle angekuwa anaendelea na majukumu yake ya kiofisi. Jambo hili lingekuwa baya zaidi na lenye maumivu makali kwa wakristo wengi.

Ni kwa sababu hizo tuliridhia kwa dhati wazo lake la kustaafu kabla ya muda ili atupishe. Lakini pia, kwa mtu yeyote mwenye akili timamu, upewe siku mbili za kukabidhi ofisi na usitakiwe kufanya shughuli zozote za kiaskofu na usiruhusiwe kuingia ofisini; hii ni adhabu tosha, hata kama utaambiwa umestaafu.

Asanteni kwa kutuelewa

Ni mimi mtumishi wenu

Mchungaji Moses Lauwo:

Hata hivyo, wafuasi wa Askofu Gulle, katika waraka wao kwa Askofu Malasusa wanasema, kitendo kilichofanyika, kinapingana na Katiba ya KKKT.

Wanasema: “Mpendwa Mkuu wa Kanisa la KKKT, Salaam katika jina la Yesu. Kupitia kwako, tunapenda ujumbe huu uwafikie watu wenye fujo ya kuvuruga kanisa na kutumia nafasi yako vibaya.

“Kwa niaba ya Wachungaji na Wakristo walio kimya wa Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria-Mwanza, tunapenda kuleta masikitiko yetu kwako na kwa maaskofu wote kwa kuona kuwa kuna kundi la Wakristo wenye asili ya Dayosisi ya Kaskazini ambao kwa chuki zao binafsi waliamua kumfanyia fujo Askofu wetu mpendwa, Andrew Gulle na kufanya mapinduzi yasiyo halali. Fujo hizi zimeandaliwa muda mreefu sana.

Askofu Malasusa

“Kwa taarifa tulizo nazo watu hawa wapenda ukabila wamekuwa wakikutana Hotel ya Malaika. Baadaye waliamua kukushirikisha mpango wao wenye nia mbaya kwa Askofu wetu.

“Walipokamilisha mipango yao waliamua kuwatumia wachache huku wengi wakiwa nyuma wakiwafadhili kwa kutoa fedha nyingi sana kwa wafanya fujo hao.

“Muda wote sisi tumenyamaza kimya na wao wamefikiri wanayo nguvu ya kufanya watakavyo. Tunapenda wajuwe kuwa Dayosisi yetu siyo ya sharika za Imani na Igoma tu. Mbona jambo hili jamii moja imebeba na kufanya fujo? Tena muda mfupi kabla ya uchaguzi? Tunawauliza mnataka kumuweka nani awe Askofu.

“Tunajua mipango yenu na anayewatuma kwa sababu ya maslahi ya kikabila mngependa mtawale kila Dayosisi na nchi pia.

“Tunasikitika Kanisa limewapa nafasi ya kuwasikiliza wachache, sisi tulio wengi tumeachwa. Tuwaambie Askofu Gulle ni kipenzi cha Wana Dayosisi Mashariki ya Ziwa Victoria.

“Kama mnabisha mleteni mtu wenu ashindanishwe na Askofu Gulle muone kama ataambulia kitu. Sisi tulio wengi tunamhitaji Askofu Gule aendelee kuongoza.

“Kwa uungwana wa Askofu Gulle asivyopenda fujo aliamua kustaafu kwa hiari. Kinachoshangaza bado kundi hilo haliamini na hata halitaki afuate utaratibu wa kikatiba wa kustaafu kwa hofu kuwa ataendelea. Kustaafu kwa Askofu inaonekana ni kama kuna kosa lililothibitishwa tayari. Sisi Wakristo na wachungaji wasio na fitina tunawasihi wachague jambo moja.

“Askofu Andrew Gulle astaafu kwa utaratibu wa kikatiba, akabidhi kwa utaratibu ulivyo au afute barua ya kustaafu na kesi ifuate utaratibu tume iundwe huyo mwanamke mliyemficha huko Moshi aje kwenye tume au mahakamani atoe huo ushahidi alionao.

“Askofu Andrew Gulle amenyamaza na Wakristo walio wengi wanaompenda wamenyamaza mnadhani hana watu wampendao. Mmemdhalilisha na kumfedhehesha vya kutosha, bila hata kuwa na utu. Viongozi wenu wamekosa hekima wakishangilia haya.

“Inashangaza sana kwa kukosa ubinadamu na midomo yenu kujaa matusi namna hivyo. Sasa tunamwomba Askofu Gulle afute barua yake ya kustaafu tupambane na ninyi kwa vyovyote vile.

“Kama ni mawakili na sisi tunao watasimama kumtetea. Vinginevyo tunapenda Askofu wetu awepo kazini, ndiye aitishe Mkutano Mkuu, asimamie uchaguzi wa kumpata mrithi wake, ambariki kuwa Askofu na akabidhi kwa misingi ya katiba yetu. Hapo tutakubali astaafu kwa hishima zote.

“Tunasikitishwa sana kuona kundi la kikabila lina mapatano yake kinyume na Halmashauri Kuu ya Dayosisi ambayo nayo ina mapatano yake kuhusu jambo hili.

“Sisi hatuwezi kufuata mapatano ya kikundi kilichojipa madaraka ya Halmashauri Kuu. Tunasihi muache kuivuruga Dayosisi yetu ambayo kwa muda mreefu Askofu Gulle ameiongoza bila ukabila na sasa mnatuletea ukabila, mbona makabila mengine hawana shida kwani wao hawataki uongozi?

“Kundi hili limemshinikiza mkuu wa kanisa kukiuka katiba ya DMZV kwani katiba hiyo inasema wazi wazi Askofu ataondoka kwa njia ya tume ya uchunguzi. Wanadiriki kusema katiba ni mbovu na hawaitaki. Kama hawafuati katiba wanafuata nini?

“Ni dhambi kumhukumu mtu bila kumsikiliza wala kusikiliza ushahidi wa wengine. Kama Askofu anafanyika kuwa askofu kwa kuwaita maaskofu wengine au kama kumzika askofu wanaitwa maaskofu inakuwa askofu anatolewa ofisini bila utaratibu. Askofu huchaguliwa na mkutano mkuu na ndio utakaomwondoa au kumrudisha.

“Na hata sasa bado mjue Mkutano Mkuu ujao hautafungwa kuamua utakavyoona vyema kuhusu Askofu wetu kipenzi cha Wanadmzv. Kama wameona Jiji la Mwanza wana nguvu basi wajue sharika zingine kama vile, Geita, Misungwi, Ukerewe, Magu, Ngudu na sharika zote zipo na haziungi mkono fujo hizi.

Ni sisi Wachungaji wa DMZV.

Ni sisi Wakristo wa sharika za nje ya jiji na ndani ya Jiji la Mwanza.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

2 COMMENTS

  1. Kumbe bado Kuna voroboto….bado
    Hicho kikao chenu ni batili leteni minitis za kikao na majina yenu na namba zenu za simu mliokaa kikao…maana Kuna wachungaji wa dhambi na sio wa kondoo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya