Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Hanifa Hamza |
RIPOTA PANORAMA
0711 46 49 84
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imelitafuta bila mafanikio faili la kesi ya mgogoro wa kiwanja namba 16, kitalu J kilichopo eneo la Magomeni, Dar es Salaam, inayodaiwa kuwa ni kesi nambari 26 ya mwaka 1982.
Aliyekuwa Naibu Msajili Mfawadhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam ambaye hivi sasa amepangiwa kazi nyingine aliyejitambulika kwa jina la V. Nongwa, alieleza kutopatikana kwa faili hilo katika barua yake ya Julai 19, 2022.
Barua hiyo ambayo Tanznania PANORAMA Blog imeiona ikiwa na kumbukumbu namba AB.43/286/03 iliyokuwa na kichwa cha maneno ‘Yah maombi ya shauri namba 26/1982 Hassan Mwenegoha versus Mvumbagu Ahmed Sunzu’ ilikuwa ikijibu barua ya Shaban Mohamedi Mbwana ya Juni 27, 2022 iliyokuwa ikiomba kujua iwapo kesi hiyo ilipata kusikilizwa na kutolewa hukumu katika mahakama hiyo.
Sehemu ya barua hiyo inasomeka, ‘husika na kichwa cha habari hapo juu, pia rejea barua yako ya tarehe 27/6/2022 na barua kutoka ofisi hii ya tarehe 30/8/2018. Nakujulisha kwamba jitihada za kutafuta shauri tajwa hapo juu hazijaweza kuzaa matunda. Hata hivyo jitihada za kutafuta jalada hili bado zinaendelea.’
Katika mahojiano aliyopata kuyafanya na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu mgogoro wa kiwanja hicho anachodai kupokwa na Mvumbagu na pia akiwatuhumu baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni kwa kupotosha ukweli kuhusu mmiliki halali wa kiwanja hicho, Mbwana alieleza kuwa aliiandikia barua Mahakama Kuu kuomba taarifa za kesi hiyo baada ya kutilia shaka taarifa alizopewa na maofisa wa Idara ya Ardhi ya Halmashauri ya Kinondoni kuwa umiliki wa kiwanja ulikwishaondolewa kwake na mahakama hiyo.
Baadhi ya nyaraka ambazo zimeonwa na Tanzania PANORAMA Blog zikielezea kuhusu uamuzi huo unaodaiwa kuwa wa Mahakama Kuu ni barua iliyosainiwa na Godfrey Mwamsojo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Kinondoni ya Machi 16, 2018 inayoeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni imeshindwa kushughulikia maombi ya Mbwana kwa sababu kumbukumbu zilizopo katika ofisi hiyo zinaonyesha kuwa kiwanja hicho kinamilikiwa na Mvumbagu Ahmed Sunzu.
Barua hiyo ilikuwa ikijibu barua ya Mbwana ya Agosti 17, 2017 kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa, Wilaya ya Kinondoni ikiomba hati mpya ya kiwanja namba 15, kitalu J, kilichopo Magomeni.
Sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Mwamsojo inasomeka hivi; ‘tunapenda kukujulisha kuwa tumeshindwa kushughulikia maombi yako kwa sababu kwa mujibu wa kumbukumbu zetu zinaonyesha kuwa kiwanja hiki kinamilikiwa na ndugu Mvumbagu Ahmed Sunzu.
‘Umiliki huu ulitokana na maamuzi ya Mahakama Kuu yaliyotolewa katika kesi ya madai na 26/1982 iliyokuwa baina ya ndugu Hassan Mwenegoha dhidi ya Mvumbagu Ahmed Sunzu ambaye kwa mujibu wa madai haya, ndugu Hassan mwenegoha alirejewa kama muuzaji na ndugu Mvumbagu Ahmed Sunzu alirejewa kama mnunuzi wa kiwanja tajwa hapo ambapo mahakama ilitoa maamuzi tarehe 17/10/1990 na iliamuru kufuta jina la umiliki wako katika kiwanja hiki na kuandika jina la Mvumbagu Ahmed Sunzu.
“Baada ya uamuzi wa Mahakama uliandikiwa barua na ofisi ya msajili ya tarehe 29/01/1991 yenye kumbukumbu namba LT/T/28688/19 ambapo ulitakuwa kurejesha hati namba 28688 ya kiwanja namba 16/J/Magomeni ambapo hukurejesha,’
Awali, Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Kinondoni, Hanifa Hamza kuhusu madai ya Mbwana kupokwa kiwanja hicho na Mvumbagu na tuhuma kuwa taarifa zinazotolewa na maofisa wa halmashauri aanayoiongoza zikiihusisha Mahakama Kuu ya Tanzania hazina ukweli na yeye alielekeza Afisa Ardhi, Godfrey Mwamsojo kujibu madai na tuhuma hizo.
Mwamsojo katika majibu yake alisema ofisi yake inayo nakara ya hukumu hiyo na ndiyo iliyoitumia katika mgogoro huo lakini alipoombwa kuionyesha ili kuondoa utata alikataa na kuelekeza ikatafutwe Mahakama Kuu.