RIPOTA PANORAMA
KILIO cha Wakala wa Utalii dhidi ya mfumo wa malipo ya ada ya viingilio kwenye Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kinazidi kuongezeka na sasa kimeelekezwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Utalii Tanzania (TATO), Sirilii Akko jana amezungumza na Tanzania PANORAMA Blog na kueleza kuwa kilio cha wanachama wake ni cha maumivu ya uchungu wa kuumizwa kiuchumi na Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).
Akko amesema yeye kama Mtendaji Mkuu wa TATO yupo tayari kuthibitisha kile kilichoelezwa na wanachama wake na alitoa wito kwa mamlaka za juu kusikiza kilio cha wakala wa utalii ili kukomesha alichokiita ukusanyaji mapato wa kikatili unafanywa na NCAA.
Amesema ofisi yake imekuwa ikiwasiliana na NCAA mara kwa mara kuhusu ubovu wa mfumo huo na umuhimu wa kuurekebisha pasipo mafanikio mpaka hivi karibuni kelele na vilio vilipozidi ndiyo mamlaka hiyo imekubali kuketi mezani na wadau mapema mwezi ujao.
“Mimi ndiye Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Utalii Tanzania, ninazungumza kwa niaba ya wanachama wangu wote kwa sababu wao ni vigumu kujitokeza hadharani kwani wanaweza kushughulikiwa. Kuna tatizo kubwa Ngorongoro. Watu wanaumizwa, wanalia, nani mtetezi wao? Acha tumlilie Rais, NCAA inakusanya malipo ya kikatili ya ada ya kuingia hifadhini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Utalii Tanzania (TATO) Sirilii Akko.
“TATO imekwishawasilisha NCAA malalamiko ya wakala wa utalii siku nyingi na siyo mara moja, ni mara nyingi sana lakini wameziba masikio, kilio sasa kimezidi ndiyo wamesema Aprili mwanzoni tukutane nao,” amesema Akko.
Mmoja wa wakala wa utalii aliyezungumza na PANORAMA jana akiomba kuhifadhiwa jina kwa sababu zilizotajwa na Akko, amedai kuna mtandao wa kimafia NCAA ambao unavuna fedha kikatili kutoka kwa wakala wa utalii huku pia ukipeleka makusanyo makubwa serikalini ili kuficha ukatili wake.
“Kuna mengi sana NCAA lakini wako wapi waandishi wa habari wa kutusemea ili umma usikie kilio chetu? Kuna mtandao wa kimafia hapa, unanyonya fedha zetu nyingi sana na ili kuwapumbaza wakubwa wanapeleka makusanyo makubwa, wanasifiwa lakini mioyo ya wananchi inalia kwa ukatili wanaofanyiwa.
“Huyo afisa wao aliyekanusha ndiyo kwanza tumemsikia na hatujui kaingia lini NCAA, kama kweli ni Afisa wa Jeshi la Uhifadhi Ngorongoro asingeyasema hayo maana hata majibu yake yanajichanganya, anakubali kuwepo kwa tatizo halafu hapo hapo anakanusha. Lazima atakuwa siyo huyo maana askari wanalia kwa jinsi fedha za NCAA zinazofujwa na wakubwa pale na haya yatalipuka tu maana watu wamechoka,” alidai.
Wakati Akko alieleza hayo, Kaimu Meneja Uhusiano wa Umma wa NCAA, Hamis Ndambaya katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni alikanusha madai yote yaliyotolewa na wakala wa utalii kuhusu mfumo wa malipo ya ada ya viingilio hifadhini kuwa wa kikatili.
Dambaya alisema madai hayo siyo ya kweli kwani wakala wa utalii wanaoshindwa kuleta wageni hutakiwa kuwasiliana na mamlaka angalau saa 24 kabla.
Kaimu Meneja Uhusiano wa Umma wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Hamis Dambvaya.
Katika majibu yake kuhusu madai hayo, Dambaya alisema wakala wa utalii wanaoshindwa kuleta wageni kwa tarehe waliyopangiwa awali wanapewa ‘credit note’ na hapo hapo alisema suala la ‘credit note’ mamlaka inalishughulikia ili wateja waweze kufanya wenyewe kupitia mfumo.
Wakala wa Utalii wanaituhumu NCAA kuwa ina mfumo wa kikatili wa malipo ya ada ya viingilio kwenye Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa sababu hautoi hati ya mkopo, (credit note) kwa wageni wanaopata dharura hivyo kushindwa au kuchelewa kuingia hifadhini.
Kwamba fedha wanazolipa wakala wa utalii kwa ajili ya wageni kuingia hifadhini; inapotokea wanashindwa kusafiri kwa dharura yoyote ya kibinadamu ikiwemo ugonjwa au msiba hazirudishwi na hakuna nafasi ya kutumiwa na mtalii husika anayefika nje ya muda wa awali.
“Wakala wa utalii tunapolipa fedha NCAA kwa ajili wageni kuingia hifadhini lakini ikatokea wakashindwa kufika kwa wakati kwa sababu ya dharura za kibinadamu, ikiwemo changamoto za usafiri, kuugua au kupata msiba, NCAA hairudishi fedha wala hairuhusu mgeni kutumia kiingilio hicho kwa muda mwingine hata kama kachelewa siku moja tu.
“Wakala wa utalii wanalazimika kutafuta fedha nyingine kumlipia kiingilio mgeni akifika, sasa fikiria una wageni kumi, wamekulipa fedha zao tena kwa Dola za Marekani na wakala umelipa NCAA halafu mgeni kachelewa, inabidi utafute fedha nyingine ulipe kwa sababu mgeni hawezi kujua hayo ya kudhulumiwa. Huu ni ukatili kwetu, watu wanafilisika.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika moja ya Hifadhi za Taifa
/“Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) alishasema hataki mapato ya dhuluma, hawa wanasema wanakusanya fedha nyingi lakini ni za dhuluma, wanatudhulumu wananchi, tunaomba mama alijue hili, tunamuomba atuhurumie, uchunguzi ufanyike ili likomeshwe kwa sababu hifadhi nyingine zina utaratibu mzuri tu tofauti kabisa na huu,” alisema mmoja wa wakala wa utalii.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi wa Ngorongoto wameibua tuhuma nzito za ufisadi na matumizi mabaya ya fedha wakidai kufanywa na baadhi ya maafisa wa juu wa NCAA wakiwemo waliofukuzwa kazi hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika madai yao hayo, wanaeleza kufujwa kwa mamilioni fedha za taasisi hiyo, ukabila, matumizi ya anasa yaliyopitiliza yanayofanywa na baadhi ya viongozi wa NCAA na ufisadi katika kuwahamisha wananchi wakazi wa Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga.
TANZANIA PANORAMA BLOG ITARIPOTI KWA KINA SKANDALI HIYO.