RIPOTA PANORAMA
MFUMO wa malipo ya ada ya viingilio kwenye Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro unadaiwa kuwa wa kikatili.
Madai haya yametolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wakala wa utalii wanaohudumia wageni wanaotembelea Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo mkoani Arusha.
Wamesema ada ya viingilio kwenye Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni ya kikatili kwa sababu haitoi hati ya mkopo (credit note) kwa wageni wanaopata dharura hivyo kuahirisha au kuchelewa kuingia hifadhini.
Madai haya yamekanushwa na Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) iliyoeleza kuwa siyo ya kweli kwani wakala wanaoshindwa kuleta wageni hutakiwa kuwasiliana na mamlaka, angalau saa 24 kabla.
Kaimu Meneja uhusiano kwa umma wa NCAA, Hamis Dambaya ameiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa wateja wote wanaoshindwa kuleta wageni kwa tarehe waliyopanga awali wanapewa ‘credit note;’ na hapo hapo akasema suala la ‘credit note’ mamlaka inalishughulikia ili wateja waweze kufanya wenyewe kupitia mfumo huo.

Kaimu Meneja Uhusiano kwa Umma wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Hamis Ndambaya.
Wakizungumza kwa sharti la majina yao kuhifadhiwa, mawakala hao walidai fedha wanazolipa kwa ajili ya wageni kuingia hifadhini, inapotokea wanashindwa kusafiri kwa dharura yoyote ya kibadamu ikiwemo ugonjwa au msiba, hazirudishwi na hakuna nafasi ya kutumiwa na mtalii husika anayefika nje ya muda.
“Wakala wa utalii tunapolipa fedha NCAA kwa ajili wageni kuingia hifadhini lakini ikatokea wakashindwa kufika kwa wakati kwa sababu ya dharura za kibinadamu, ikiwemo changamoto za usafiri, kuugua au kupata msiba, NCAA hairudishi fedha wala hairuhusu mgeni kutumia kiingilio hicho kwa muda mwingine hata kama kachelewa siku moja tu.
“Wakala wa utalii wanalazimika kutafuta fedha nyingine kumlipia kiingilio mgeni akifika, sasa fikiria una wageni kumi, wamekulipa fedha zao tena kwa Dola za Marekani na wakala umelipa NCAA halafu mgeni kachelewa, inabidi utafute fedha nyingine ulipe kwa sababu mgeni hawezi kujua hayo ya kudhulumiwa. Huu ni ukatili kwetu, watu wanafilisika.
“Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) alishasema hataki mapato ya dhuluma, hawa wanasema wanakusanya fedha nyingi lakini ni za dhuluma, wanatudhulumu wananchi, tunaomba mama alijue hili, tunamuomba atuhurumie, uchunguzi ufanyike ili likomeshwe kwa sababu hifadhi nyingine zina utaratibu mzuri tu tofauti kabisa na huu,” alisema mmoja wa wakala wa utalii.
Sambamba na hilo, waliendelea kudai kuwa wamekwishawasilisha maombi kwa NCAA ibadili mfumo huo lakini imekuwa ikipuuza maombi hayo kwa muda mrefu na kwamba wageni wanaopata taarifa za maumivu ya kiuchumi wanayokutana nayo mawakala hao, wanasikitika.

Rais Samia Suluhu Hassan
Alipoulizwa Kaimu Meneja uhusiano kwa Umma wa NCAA, Hamis Dambaya kuhusu madai hayo alisema hayana ukweli kwani wakala wote wanaoshindwa kuleta wageni kwa kadri ya ratiba zao, hutakiwa kuwasiliana na mamlaka angalau saa 24 kabla ya tarehe kufika.
Dambaya alisema NCAA inapopokea taarifa saa 24 kabla, wakala wa utalii huruhusiwa kutumia fedha zake kwa kundi lile lile kwa siku nyingine au kutafuta wageni wengine ambao hutumia malipo hayo na kwamba suala la ‘credit note’ linashughulikiwa na mamlaka ili wateja waweze kufanya wenyewe kupitia mfumo.
Akijibu kuhusu fedha zinazolipwa na wakala wa utalii kisha NCAA kukataa zisitumike kwa wageni husika wanapochelewa kuingia hifadhini hivyo wakala kulazimika kulipa fedha nyingine, alisema changamoto hiyo imeishafanyiwa kazi na kwamba hivi sasa mteja anaweza kubadilisha tarehe ya matumizi ya kibali iwapo wageni wamebadili ratiba ya safari.
“Kwa maana hiyo siyo kweli kwamba NCAA inachukua fedha haramu kwa wateja wake na kuwazuia wageni kuingia hifadhini,” alisema Dambaya.
Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza pia Dambaya kuhusu NCAA kupuuza kilio cha wakala wa utalii kubadilisha mfumo wa sasa wa malipo naye akijibu alisema, maombi hayo yamezingatiwa na hivi sasa yanafanyiwa kazi na wataalamu wa ndani wa mamlaka hiyo.
“NCAA imezingatia maombi ya wadau wa utalii kubadili mfumo huo na wakati wote tunathamini juhudi za wadau katika kuongeza idadi ya watalii. Maombi ya wakala wa utalii ya ubadilishwaji wa mfumo yanafanyiwa kazi na wataalamu wetu wa ndani ili kurahisisha kazi kwa watumiaji na kuruhusu ‘flexibility,’” alisema Dambaya.

Sehemu ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro
Aliongeza kuwa kazi ya maboresho ipo kwenye hatua za mwisho za majaribio na inategemewa kukamilika hivi karibuni ambapo wadau watajulishwa.
Dambaya alizungumzia pia madai kuwa wageni wanaokataliwa kuingia hifadhini kwa sababu ya kuchelewa licha ya kuwa wamelipiwa, wanapopewa taarifa hizo wamekuwa wakieleza kuwa licha ya uzuri wa hifadhi hiyo hawana mpango wa kurejea kwa sababu ya utaratibu mbovu uliopo.
Alisema madai hayo hayana ukweli na kurejea kauli yake kuwa wakala wa utalii wanaoshindwa kuleta wageni kadiri ya ratiba zao wanapaswa kutuma barua pepe angalau saa 24 kabla ya tarehe husika na zikipokelewa, maandalizi ya ndani hufanyika ili kumuwezesha wakala wa utalii kutumia fedha zake kwa kundi hilo la wageni, siku nyingine.
Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza pia Dambaya iwapo msuguano baina ya NCAA na wakala wa utalii hautaathiri jitihada za Rais Samia kukuza Sekta ya Utalii; tofauti na majibu yake ya awali, alisema NCAA haina malalamiko yoyote mezani kwani wateja wake wote walioshindwa kuleta wageni kwa tarehe waliyopanga awali hupewa ‘credit note’ ili waweze kutumia malipo yao siku za mbele kwa tarehe watakayopanga kuingia na wageni hifadhini.
Alisema changamoto pekee inayoweza kuwepo ni ya kimawasiliano baina ya pande zote mbili lakini madai ya wakala hao kuwa NCAA inakusanya mapato haramu si ya kweli.
SOMA TANZANIA PANORAMA BLOG KUFAHAMU MENGI ZAIDI YA HIFADHI YA NGORONGORO.