RIPOTA PANORAMA
SERIKALI imeshindwa kesi ya kuuza mifugo ya wafugaji watatu, wakazi wa Loliondo kwa njia ya mnada.
Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo ni kuiamuru serikali kuwalipa wafugaji hao Shilingi 169,264,200.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Utetezi ya Mtandao wa Watetezi Wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ambao uliwasimamia wafugaji hao mahakamani, hukumu iliyoibwaga serikali ilitolewa na mahakama Februari 14, 2924.
Inaeleza kuwa mahakama imeamuru serikali kuwalipa Oloomu Kursas, Sinjore Maitika na Ndagusa Koros Shilingi 169,264,200 kutokana na mauzo kwa njia ya mnada usio halali wa mifugo ya wafugaji hao.
Kwamba mnada huo usio halali ulifanyika Novemba Mosi, 2023 ukihusisha kuuzwa kwa ng’ombe 806, kondoo 420 na mbuzi 100.
Taarifa inaeleza kuwa serikali ndiyo iliyofungua kesi kwanza, Oktoba 30, 2023 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, ikiiomba mahakama kutoa amri ya kuuzwa kwa mifugo hiyo kwa njia ya mnada.
Kwamba mawakili wa serikali katika kesi hiyo namba 10 ya mwaka 2023, walidai mahakamani hapo kuwa mifugo hiyo ilikamatwa na askari wa wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Walidai mifugo hiyo ilikutwa eneo la Long’osa wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara na kuhifadhiwa katika Kituo cha Askari Wanyamapori cha Lobo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mawakili wa serikali waliendelea kudai mahakamani hapo kuwa mifugo hiyo haikuwa na mwenyewe ndipo Oktoba 31 Oktoba, 2023 mahakama ilitoa amri ya kuiuza kwa njia ya mnada na kuteuliwa msimamizi wa mnada aliyetakiwa kuzingatia sheria na taratibu zote za uendeshaji wa minada.
Taarifa ya THRDC inaeleza zaidi kuwa baada ya amri ya Mahakama, Oloomu Kursas, Sinjore Maitika na Ndagusa Koros walifungua maombi Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala ya Musoma, wakiiomba Mahakama Kuu irekebishe Amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, itamke kuwa mifugo hiyo ilikuwa ni mali yao.
Wakisimamiwa na mawakili wa THRDC, watatu hao walidai madai ya Jamhuri hayakuwa ya kweli na walifungua shauri la maombi ya marekebisho namba namba 8 ya 2023.
Mkuu wa Idara ya Utetezi, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Wakili Paul Kisabo
Katika maombo hayo, hata kama mwenye mifugo hakujulikana, bado taratibu za kisheria za kuiuza hazikufuatwa. Sheria inaelekeza mali ambazo mmiliki wake hajajulikana, zitangazwe hadharani ili wamiliki waweze kujitokeza.
Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Hifadhi za Taifa na kifungu cha 47 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi. mali ambazo mmiliki wake kajajulikana zinapaswa kutangazwa hadharani.
Sambamba na hatua hiyo, wafugaji hao chini ya usaidizi wa kisheria ya THRDC walifungua maombi ya zuio, wakiiomba Mahakama Kuu izuie kuuzwa kwa njia ya mnada mifugo hiyo. Maombi hayo yalipokelewa mahakamani na kupewa namba 35 ya 2023.
Novemba Mosi, 2023 Mahakama Kuu iliamru uuzwaji mifugo hiyo usitishwe kwa sababu wafungua maombi walinyimwa haki ya kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na Novemba 10, 2023 ilitengua Uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi ikiamuru kesi hiyo kusikilizwa upya.
Hata hivyo, taarifa ya THRDC inaeleza kuwa dalali wa mahakama alitangaza mnada Novemba Mosi, 2023 na kuuza ng’ombe, kondoo na mbuzi, siku hiyo hiyo.