RIPOTA PANORAMA
ZIKIWA zimepita siku 52 sasa tangu wanandugu wawili walipotekwa nyara na watu wasiojulikana mkoani Singida, Jeshi la Polisi bado halijafanikiwa kuwapata.
Watu hao ambao ni ndugu, Juma Idi Mwiru na Haruna Idi Mwiru, walitekwa nyara Desemba 27, 2023 na tukio la kutekwa kwao liliripotiwa Kituo Kikuu cha Polisi Singida na kufunguliwa faili la uchunguzi lenye namba SGD/RB/7876/023.
Tangu mwaka jana, polisi walianza uchunguzi wa tukio hilo uliohusisha kuwasaka kwenye mahabusu zote za polisi na magereza bila mafanikio na leo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida ambaye amezungumza na Tanzania PANORAMA Blog kwa njia ya simu huku akikataa kutaja jina lake amesema, polisi bado wapo gizani lakini wanaendelea na uchunguzi.
Mmoja watoto wa watu hao (jina lake tunalihifadhi) katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog, hivi karibuni kuhusu kutekwa kwa ndugu zake, alisema walitekwa na watu wasiojulikana katika maeneo mawili tofauti mjini Singida.
Alisema Haruna alitekwa katika eneo la Muhanga akiwa kwenye mgahawa alipokuwa akistafutahi pamoja na rafiki yake.
“Haruna alitekwa akiwa Muhanga, alikuwa akinywa chai na rafiki yake, wakaja watu na gari aina ya Nissan wakamuita kwa jina lake alipokwenda akasalimiana na watu waliokuwa kwenye gari hilo kisha akaingia kwenye gari wakaondoka naye.
“Walipotoka hapo walikwenda kwa Juma ambaye alikuwa kituo cha mafuta cha Olimpiki kilichopo barabara ya kwenda Arusha. Naye wakafika wakamwita jiina lake, akaenda kuwasikiliza naye wakamchukua. Baada ya kuondoka hapo ndiyo hawajaonekana tena, hatujui kama wamekufa au wapo hai,” alisema.
Akiendelea kuzungumzia utekaji huo, alisema baada ya kuwatafuta ndugu zao bila mafanikio waliripoti polisi ambao walifungua jalada lenye namba SGD/RB/787/023 kisha wakaanza kuwatafuta lakini hawajafanikiwa kuwapata.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paulo Makonda akiwa kwenye ziara ya kichama mkoani Singida alitaka maelezo kutoka kwa mkuu wa wilaya na mkoa huo baada ya tukio hilo kuibuliwa kwenye moja ya mikutano ya hadhara aliyoifanya.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alipotakiwa na Makonda kulizungumzia alisema ni tukio la kweli ambalo limekwishafikishwa mezani kwa Inspekta Jenerali wa Polisi na kwamba polisi wanaendelea kuwatafuta mateka hao.
Mmoja wa viongozi wa Mkoa wa Singida aliyezungumza na Tanzania PANORAMA Blog kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa, alisema mateka hao hawajulikani walipo kwani mahabusu na magereza yote nchini hawapo.
“Hilo ni gumu na nyeti lakini RPC anahangaika. Magereza yote wametafutwa hawapo, polisi wametafuta vituo vyote hawapo, yaani tunavyosema hakuna mahabusu yoyote Tanzania ambayo wapo, sasa tunafanyaje? alisema kiongozi huyo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa alipoulizwa, alisema yupo likizo na kutoa namba ya polisi anayekaimu nafasi yake akieleza kuwa ndiye anayeweza kulizungumzia.
SOMA TANZANIA PANORAMA KUFAHAMU ZAIDI KUHUSU TUKIO HILI