RIPOTA PANORAMA
UWANJA wa mchezo wa gofu ambao ni bora zaidi duniani umeanza kujengwa katika eneo la Fortikoma, lililopo nje kidogo ya Hifadhi ya Serengeti.
Mradi wa ujenzi wa huo umebuniwa na Bodi ya Wadhamni ya TANAPA na unatekelezwa kwenye eneo la ukubwa wa ekari 450.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni ofisini kwake, Jijini Arusha, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Juma Kuji alisema gharama za ujenzi wa uwanja huo ni Shilingi bilioni 9.5
Msimamizi wa mradi huo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Mhandisi Mshauri, Richard Matolo (Phd) ameiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa uwanja huo utajulikana kwa jina la Serengeti National Park Golf Course.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) Juma Kuji
āNi mradi wa kipekee ukilinganisha na viwanja vingine vya gofu duniani. Upekee wa uwanja huu siyo kwa sababu unajengwa kwenye eneo la Hifadhi ya Serengeti, bali upekee wake unatokana na sifa za makusudi zilizoongezwa kwenye kuubuni,ā amesema Dk. Matolo.
Dk. Matolo amezitaja baadhi ya sifa za uwanja huo kuwa ni pamoja na mashimo kuwekwa mbalimbali ili kuacha nafasi katikati na pia mashimo hayo yameongezewa urefu na kuwekewa vikwazo vya kupindisha ili kuufanya usiwe rahisi kuchezeka kama vilivyo viwanja vingine duniani.
Amesema uwanja huo utawafanya wachezaji wanapocheza wafikiri zaidi kutokana na changanoto zilizowekwa kwa makusudi ili kuufanya uwe na ushindani zaidi.
āNi watu wachache sana ambao ni wachezaji bingwa wa gofu watakaoweza kucheza na kumaliza. Kama vilivyo viwanja vingine vya kimataifa vya gofu, huu nao una mashimo 18 lakini yameongezewa urefu,ā amesema Dk. Matolo.
Ujenzi wa uwanja huo ulizinduliwa Desembe 29, 2022 na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Jenerali Mstaafu, George Marwa Waitara na ulitarajiwa kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara akiwa na wajumbe wa bodi na viongozi wa TANAPA, muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Uwanja wa Gofu wa Kimataifa bora zaidi duniani unaojengwa eneo la Fortikoma, nje kidogo ya Hifadhi ya Serengeti, Desemba 2022.
Hata hivyo, Dk. Matolo amesema uwanja huo hadi sasa haujakamilika kujengwa kwa sababu ya changamoto za kifedha zinazoikabili TANAPA lakini serikali inafanya juhudi za makusudi za kuendeleza ujenzi wake na inatarajiwa utakamilika ndani ya miezi sita.