Wednesday, December 25, 2024
spot_img

SKANDALI YA PAULINE GEKUL HAIJAPOA, YAFIKISHWA SEKRETARIATI YA MAADILI YA VIONGOZI

RIPOTA PANORAMA

SKANDALI inayomkabili Mbunge wa Babari Mjini, Pauline Gekul ya kumfanyia ukatili mfanyakazi wake, Hashimu Ally Philimone kwa kumuingizia chupa sehemu za siri, imefikishwa mbele ya Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa wa Chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo ndiye aliyewasilisha malalamiko hayo kwa Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya Gekul.

Katika malalamiko yake hayo ya Novemba 27, 2023, Nondo anadai kuwa kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma, sura ya 398 (R.E 2020), kifungu cha 25(1) kinatoa fursa kwa mtu yeyote kuwasilisha malalamiko yake dhidi ya kiongozi wa umma juu ya uvunjifu wa sheria ya maadili.

Hati ya malalamiko ya Nondo dhidi ya Gekul kwenda kwa Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona, inaeleza kuwa ibara ya 26(2) ya Katiba ya Tanzania ya 1977, inatoa agizo la wajibu na haki kwa kila mtu kulinda Katiba na sheria nyingine za nchi.

Nondo ameandika kwenye hati yake hiyo kuwa anaamini Gekul, aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria amevunja sheria ya maadili ya viongozi wa umma, sura ya 398 (R.E 2020) kifungu cha 6(1)(a) na 6(1)(b)(i) ambavyo vinahitaji viongozi wa umma kutenda majukumu yao ya kiofisi na binafsi kwa kuzingatia maadili, uaminifu, huruma na uadilifu.

Katika mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu hatua yake hiyo, Nondo alisema aliwasilisha malalamiko yake kwa Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ili aanzishe uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili Gekul.

Alisema uchunguzi huo unapaswa kuegemea kwenye Katiba ya Tanzania ya 1977, ibara ya 132(1) na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 (R.E 2020), kifungu cha 16(2)(b)(c)(e), 25(2)(b) na 25(4-7).

Kwamba ikithibitika tuhuma zinazomkabili Gekul ni za kweli, atakuwa amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kifungu cha 6(1)(a) na 6(1)(b)(i) hivyo moja kwa moja ubunge wake utakoma.

Abdul Nondo

Nondo amenukuu ibara ya 71(1)(d) ya Katiba ya Tanzania inayosema mbunge atakoma kuwa mbunge iwapo itathibitishwa kwamba amevunja masharti ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

Vyanzo vya habari vya Tanzania PANORAMA Blog, vimedokeza kuwa tayari Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma amekwishajibu kusudio hilo la Nondo kuwa hawezi kufanya uchunguzi huo kwa sababu kuna kesi mahakamani inayohusu skandali hiyo ya Gekul.

Taarifa zimeeleza kuwa Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Januari 6, 2024 alimwandikia Nondo kuwa kuna kesi jinai katika Mahakama ya Wilaya ya Babati inayomkabili Gekul, hivyo ofisi yake haiwezi kuendesha uchunguzi dhidi ya jambo lililoko mahakamani.

Hata hivyo, Nondo ameiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa ameshtushwa na kushangazwa na majibu hayo yanayoonyesha kuwa Kamishna wa Sekretariati ya Maadili  ya Viongozi wa Umma hana taarifa ya kufutwa kwa kesi hiyo.

“Nimeshtushwa sana na hili na limenishangaza, kwamba Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma na ofisi yake hawana taarifa kuwa kesi ya Jinai namba 179 ya 2023 iliyofunguliwa na Wakili Peter Madeleka, iliondolewa na Mwendesha Mashtaka (DPP), tangu Disemba 26, 2023,” amesema Nondo.

Amesema masuala ya maadili ya viongozi wa umma hayana uhusiano na kesi za jinai hivyo Kamishna wa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma hapaswi kukwepa wajibu wake kama ulivyoainishwa kwenye Katiba ya Tanzania ya 1977, ibara ya 132(1) na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura 398 (R.E 2020)) kifungu cha 16(2)(b)(c)(e), 25(2)(b) na 25(4-7) na kuongeza kuwa skandali hiyo haijaisha, bado ni mbichi.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya