RIPOTA PANORAMA
MAZAO ya wakulima wa Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, yamefyekwa na kikundi cha watu kinachodaiwa kuwa ni kikosi cha walinzi wa maeneo ya hifadhi za misitu wilayani humo.
Kikundi hicho kinadaiwa kufyeka mazao ya wakulima katika vijiji vya Ugansa, Ntitimo, Kangeme na Luganjo Kitaleni na kimefyeka Mpunga, Mahindi, Karanga, Mihogo, Ufuta na Alizeti; mazao ambayo yalikuwa tayari kwa kuvunwa.
Sambamba na hilo, kikundi hicho kinadaiwa kupora mazao ya wakulima waliyoyahifadhi nyumbani na kwamba kinatekeleza vitendo hivyo kwa kutumia mwamvuli wa jumuiya iliyoanzishwa na wananchi wa vijiji 11 vya Wilaya ya Kaliua, kwa ajili ya shughuli za uhifadhi ambayo hata hivyo haijapata kusajiliwa na serikali. Jumuiya hiyo inafahamika kwa jila la Igombe and Sagala Wildlife Management Area (ISAWIMA).
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimedai kuwa kikundi hicho kimekuwa kikivamia mashamba ya wakulima kinaowatuhumu kufanya shughuli za kilimo ndani ya eneo la hifadhi ya msitu uliopo Wilaya ya Kaliua na hadi sasa zaidi ya kaya 5000 zimeathiriwa na vitendo hivyo.
Zimetaja baadhi ya matukio ya kufyeka mazao ya wakulima yaliyotekelezwa na kikundi hicho katika Kijiji cha Ugansa ni pamoja na shamba la mahindi lenye ukubwa ekari saba lililotarajiwa kuzalisha junia 140 na shamba jingine lenye ukubwa wa ekari nne lililotarajiwa kuzalisha junia 80.
Mashamba mengine yaliyotajwa kufyekwa katika kijiji hicho ni lenye ukubwa wa ekeri 12 lililotarajiwa kuzalisha junia 240 na jingine lenye ukubwa wa ekari nane lililotarajiwa kuzalisha junia 160.

Wakulima wa wilayani Kaliua mkoani Tabora wakiangalia mazao yao jinsi yalivyofyekwa na kikundi cha ISAWIMA (Picha kwa hisani ya wanakijiji)
Inadaiwa, kikundi hicho kimekuwa kikipita nyumba kwa nyumba kikipora mazao ya wakulima na baadhi ya matukio ya uporaji yanayotajwa, linamhusisha mkulima mmoja (majina yote ya walioguswa na vitendo hivyo tumeyahifadhi kwa sababu maalumu), aliyekuwa na akiba ya junia 28 za mahindi, alizeti junia mbili na debe tatu pamoja na choroko debe mbili.
Mkulima mwingine wa kijiji hicho anayedaiwa kukutana na ukatili wa kikundi hicho ameporwa junia tisa za mahindi na junia nane za mpunga. Mwingine junia 24 za mchele na mahindi junia 17 huku ghala la mahindi lililokuwa na junia 250 likiteketezwa kwa moto.
Katika Kijiji cha Liganjo Kitaleni, kikundi hicho kinadaiwa kuchoma junia 10 za mahindi, Kijiji cha Kangeme kinadaiwa kufyeka shamba lenye ukubwa wa ekari 12 na katika Kijiji cha Ntitimo, mashamba mawili yamefyekwa; la kwanza likiwa na ukubwa wa ekari 10 na jingine ekari nane.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Mazingira na Ufugaji Wenye Tija Tanzania (CHAMAUTA), Jeremiah Wambura, jana aliiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa kwa muda mrefu amefanya jitahada za kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Kaliua dhidi ya ukatili wa kikundi hicho bila mafanikio.
“Kuna mgogoro mkubwa ambao unaweza kuhatarisha maisha ya watu. Hicho kikundi ni masalia ya jumuiya ya uhifadhi ambayo ilianzishwa na wananchi lakini haikusajiliwa baada ya kutofautiana kuhusu mwenendo wake. Wajanja wachache wakaing’ang’ania kwa sababu inawapa maslahi, sasa wakulima wanaoipinga ndiyo wanaofanyiwa huo ukatili,” alisema Wambura.
Alisema taarifa alizozipata serikalini wakati akifuatilia mgogoro huo zinaonyesha kuwa eneo ambalo wananchi wamefyekewa mazao yao lina changamoto ya uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.

Wakulima wilayani Kaliua mkoani Tabora wakiangalia mazao yao walivyofyekwa (Picha kwa hisani ya wanakijiji)
Wambura alisema taarifa kilizonazo chama chake kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori Tanzania (TAWA) zinaonyesha mamlaka hiyo ilichukua eneo lenye ukubwa wa hekta 1300 ambalo lilikuwa mali ya wanakijiji na kuwabakizia hekta 500.
“TAWA walisema ndani ya hekta 1300 walizochukua kutoka kwa wananchi na hata katika Hifadhi ya Igombe hakuna mwanakijiji aliyeingia kufanya shughuli za kilimo wala hakuna oparesheni iliyofanyika ikihusisha kufyeka mazao ya wananchi isipokuwa, taarifa walizonazo oparesheni hiyo inafanywa na kikundi cha ISAMIWA chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya,” alisema Wambura.
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta mmoja wa viongozi wa ISAMIWA na kumuuliza kuhusu ufyekaji huo wa mashamba na kupora mazao ya wakulima naye alizungumza kwa sharti la jina lake kuhifadhiwa kwa kueleza kuwa yeye ni miongoni mwa wanachama na viongozi wa ISAMIWA ambayo haina usajili asiyekubaliana na inachokifanya kwa wakulima lakini hawezi kuzungumza hadharani kwa sababu baadhi ya wakubwa wananufaika na mazao wanayoporwa wakulima.
Alisema mashamba yote yaliyofyekwa hayapo ndani ya eneo la hifadhi na mazao wanayonyang’anywa wakulima wanagawana waporaji na walio nyuma yao huku wakulima wakibaki bila chakula na katika hali ya umasikini mkubwa.
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta kwa bidii kubwa lakini pasipo mafanikio, Kamishna Mkuu wa TAWA ili kupata kauli yake kuhusu eneo la wanakijiji linalodaiwa kuchukuliwa na mamlaka yake na iwapo askari wake wanahusika kwenye oparesheni inayoendelea sasa Wilaya ya Kaliua ya kufyeka mazao ya wakulima waliolima ndani ya hifadhi.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Rashid Chuachua alipoulizwa alisema hakuna mwananchi aliyefika ofisini kwake kutoa taarifa ya mazao yake kufyeka na kwamba anafikiri wakulima hao hawatoi taarifa kwa sababu wako ndani ya eneo la hifadhi.

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Rashid Chuachua
Alisema mwananchi ambaye hayuko ndani ya hifadhi lakini shamba lake limefyekwa aende ofisini kwake ili achukue hatua.
“Jaribu kufikiria tu hawa wananchi wanasema wamefyekewa mazao yao, wamevuka ofisini kwa DC, wakavuka ofisi ya mkuu ya mkoa, unanielewa vizuri? Kwa sababu sidhani hata kama mkuu wa mkoa ana hizo taarifa, then wanakuja kwa mwandishi wa habari.
“Mimi sina tatizo katika hilo lakini kama tunataka kuona namna ya kuwasaidia wananchi waambie waje ofisini kwangu twende yalikokatwa mazao halafu nitakujulisha kuwa hawa walivuka ofisini kwangu, hawakuja kwa sabahu wapo ndani ya hifadhi,” alisema Chuachua.
Chuachua alisisitiza kuwa yeye anaishi Wilaya ya Kaliua na ofisi yake ipo hapo hivyo mwananchi aliyefyekewa mazao yake yaliyo nje ya hifadhi aende ofisini kwake.
“Mimi naishi Kaliua, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ipo Kaliua, mwananchi yeyote aliyefyekewa mazao nje ya hifadhi, sizingumzii ndani ya hifadhi kwa sababu ni kosa hata wewe mwandishi wa habari huwezi kuingia ndani ya hifadhi bila kibali.
“Kama mwananchi amefanya kilimo ndani ya hifadhi, hata mimi mkuu wa wilaya siruhusiwi kuingia ndani ya hifadhi bila kibali na mazao yanayofyekwa ndani ya hifadhi huwa hata wenyewe hawawezi kuwepo kwa sababu akiwepo atakamatwa kwa kuwa ni kosa kulima ndani ya hifadhi. Tunalo jukumu la kulinda hifadhi lakini pia tunalo jukumu la kulinda maslahi ya wananchi wanaofuata sheria.
“Kama mazao yapo nje ya hifadhi, nasema sasa hivi ninao uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya waliofanya ukatili huo. Kilicho ndani ya hifadhi ni mali halali ya mwenye hifadhi, hakuna serikali inayoweza kuruhusu mazao yaliyo nje ya hifadhi yafyekwe,” alisema Chuachua.
Alipoulizwa iwapo jibu lake linamaanisha yapo mazao ya wakulima waliolima ndani ya hifadhi ambayo yamefyekwa alisema hilo hajui kwa sababu hajapewa taarifa hizo.
Tanzania PANORAMA Blog ilimuuliza Chuachua ni kwanini wananchi wanaoingia ndani ya hifadhi kulima wanaachwa mpaka mazao yanapofikia hatua ya kukomaa ndipo yanafyekwa naye akijibu alihoji ni kwanini wananchi hao wanaingia katika nyumba ambayo siyo ya kwao.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe hakupatikana mara moja kuzungumzia jambo hilo na Tanzania PANORMA Blog inaendelea kumtafuta ili kupata msimamo wa serikali kuhusu malalamiko ya wananchi pamoja na mambo mengine yanayoendelea katika Wilaya ya Kaliua.