MWANDISHI MAALUMU
KOREA ya Kusini ndiyo nchi kinara duniani katika maendeleo ya teknolojia.
Mafanikio ya Korea Kusini kiteknolojia yamefikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa kwenye utafiti na utamaduni wa ubunifu wa raia wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na mtandao wa Global news and insght for corporate professionals, Korea Kusini imeshika namba moja kimaendeleo ya teknolojia duniani huku mataifa mengine ya Bara la Asia nayo yakiendelea kung’ara kwenye orodha ya 20 bora.
Ripoti imeyataja mataifa ya Asia yanayoshikilia nafasi za juu katika maendeleo ya kiteknolojia kuwa ni pamoja na Japan, Singapore na Taiwan.
Marekani imo katika orodha hiyo na kwa Bara la Ulaya, Ujerumani ambayo imekuwa akisifika kwa ubora katika nyanja ya uhandisi nayo imetajwa kwenye kundi la nchi zinazofanya vizuri kiteknolojia.
Israel ni ya sita ikiwa imewekeza zaidi kwenye utafiti huku kampuni zake kubwa zikipata mafanikio makubwa kisayansi, teknolojia ya kijeshi na sekta nyingine na Falme za Kiarabu (UAE) imetajwa kushika nafasi ya 18.
Japan, licha ya kuwa kwenye orodha ya nchi 20 bora, imetajwa kushuka kiviwango huku China na India zenye idadi kubwa ya watu duniani nazo zikitajwa kuungana na Japan.
Ingawa China imetajwa kuwekeza kwa kiwango kikubwa kwenye utafiti na maendeleo ya kiteknolojia, imeshindwa kufanya vizuri kinyume na matarajio kutokana na sera zake na India kwa upande wake ikiwa imewekeza kwa kiwango kidogo katika utafiti na maendeleo.
Ripoti imeainisha njia zilizotumika kufanya utafiti uliotoa ripoti hiyo kuwa ni vipimo vinavyowakilisha upana wa teknolojia, watumiaji wa mtandao wa inteneti na LTE 4G.
Pia alama za dijiti zinazokusanywa na kituo cha ushindani cha dunia (IMD), ambazo ni mkusanyiko wa maarifa ya kiteknolojia, nguvu ya sasa ya kiteknolojia, uwezo wa kuendeleza ubunifu na sehemu ya pato la taifa linalotumika katika utafiti na maendeleo ya teknolojia huko tuendako.