VATICAN
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francisco amesema ushoga na usagaji haupaswi kuchukuliwa kama kosa la jinai bali hali ya kibinadamu.
Amesema mashoga na wasagaji wana haki zao za msingi na ni watoto wa Mungu ambaye anawapenda kwa jinsi walivyo.
Msimamo huu Papa Francisco aliutoa mapema mwaka huu alipofanya mahojiano maalumu na mwandishi wa habari, Nicole Winfield wa Shirika la Habari la Associated Press (AP).
Mahojiano hayo yaliyofanyika kwa lugha ya kihispania na kuchapishwa na tovuti rasmi ya Vatican, yalidumu kwa takriban saa mbili ambapo Papa Francisco alisititiza msimamo wake wa kutofautisha ushoga na usagaji dhidi ya jinai.
Alisema mashoga na wasagaji, kila mmoja anapaswa kujitahidi kupambania utu, heshima na haki zake za msingi lakini kuwa shoga au msagaji si kosa la jinai linaloweza kusababisha kuhukumiwa kifungo au kupewa adhabu ya kifo.
Papa Francisco alisema ushoga na usagaji ni dhambi hivyo kuna haja ya kutofautisha kati ya kosa la jinai na dhambi na kwamba hata kukosa upendo kwa jirani yako, ni dhambi.
Papa Francisco alisema anapinga sheria zinazowatia hatiani mashoga na wasagaji na alitoa wito kwa maaskofu wa Kanisa Katoliki kusaidia kujenga uhusiano mwema na jumuiya za watu wa aina hiyo kwa kuwaheshimu, kuwahurumia pamoja na kuwa waangalifu, mintarafu mafundisho ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki.
Papa Francisco akiongoza ibada Kanisa la Mt Peter
Alisema mwelekeo huo unapaswa kuwa hata kwa wauaji na watu katili katika jamii kwani kila muumini anapaswa kuwa na kile alichokiita ‘dirisha’ la maisha yake la kushuhudia matumaini na hatimaye kuona utu wa Mungu.
Hata hivyo, Papa Francisco alisema ushoga na usagaji ni tabia zinazokinzana na mila, desturi na tamaduni nyingi duniani, sanjari na imani kwa watu wengi.
“Katekisimu ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa imani, sakramenti za kanisa, maisha adili na sala kuhusu makosa dhidi ya usafi wa moyo inasema, ‘shauku ya jinsia ya aina moja inamaanisha uhusiano kati ya wanaume au kati ya wanawake wanaoonja mvuto wa kijinsia kuelekea kwa watu wa jinsia ileile au wanaoonja mvuto zaidi kwa watu wa jinsia ileile.
“Shauku hii imechukua sura mbalimbali katika mwenendo wa karne na katika tamaduni mbalimbali. Mwanzo wake kisaikolojia unabaki hauelezeki,” alikaririwa Papa Francisco akisema.
Aliendelea kwa kueleza kuwa ushoga na usagaji ni vitendo viovu na mapokeo yametamka daima kwamba vitendo vya kujamiana watu wa jinsia moja ni vitendo viovu.
Papa Francisco alisema ushoga na usagaji ni vitendo dhidi ya sheria ya maumbile vinavyotenga paji la uhai na tendo la kijinsia hivyo havipaswi kuidhinishwa kwa namna yoyote ile.
“Idadi ya wanaume na wanawake waliozama katika mwelekeo wa shauku ya jinsia ya aina ileile sio ya kupuuzia.
“Uhusiano nao unapaswa kuwa wa heshima, huruma na uangalifu. Kila ishara ya ubaguzi usio wa haki iepukwe. Watu hawa wanaitwa kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yao na kama wakristo, kuunganisha magumu wanayoweza kukutana nayo kutokana na hali yao na sadaka ya msalaba wa bwana,” alinukuriwa zaidi Papa Francisco.
Alisisitiza kuwa mashoga na wasagaji wanaitwa kuwa na usafi wa moyo na kwa fadhila, sala na neema ya sakramenti, wanaweza kubadilika polepole na kukaribia ukamilifu wa kikristo.