BUJUMBURA, BURUNDI
RAIS wa Burundi, Evariste Ndayishimiye amesema watu wanaobainika kujihusisha na ushoga nchini humo wanapaswa kupelekwa kwenye viwanja vya michezo na kupigwa mawe.
Ndayishimiye aliyasema hayo ijumaa, wiki iliyopita katika mahojiano aliyofanya na vyombo vya habari nchini humo.
Alisema wapenzi wa jinsia moja nchini Burundi wanapaswa kupigwa mawe na kitendo cha kuwapiga mawe watu hao hakitahesabika kama uhalifu.
Ndayishime alizinyooshea kidole nchi tajiri duniani zinazounga mkono vitendo vya ushoga kuwa zinapaswa kubaki na misaada yao iwapo misaada hiyo kwa nchi yake itaambatana na wajibu wa kutoa haki kwa wapenzi wa jinsia moja.
Akitumia maandiko ya biblia, Ndayishimiye alisema Mungu anachukia mapenzi ya jinsia moja na kwamba hilo halina mjadala nchini Burundi.
“Kwangu mimi, nadhani ikiwa tutapata watu hawa nchini Burundi wanapaswa kupelekwa kwenye viwanja vya michezo na kupigwa mawe na kufanya hivyo haitakuwa kosa.
“Uhusiano wa jinsia moja ni kama kuchagua kati ya shetani na Mungu. Ikiwa unataka kumchagua shetani sasa nenda ukaishi katika nchi hizo na nadhani wale wanaojitahidi kwenda huko wanataka kuiga tabia hizo, wanapaswa kubaki huko na kamwe wasituletee,” alisema Ndayishimiye.
Rais Ndayishimiye
Mapenzi ya jinsi moja ni kinyume cha sheria nchini Burundi na adhabu yake ni kifungo cha hadi miaka miwili jela.
Agosti, mwaka huu watu saba walihukumiwa vifungo vya kati ya mwaka mmoja na miwili baada ya mahakama katika Mji Mkuu wa Kisiasa, Gitega kuwatia hatiani kwa makosa ya kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.