RIPOTA PANORAMA
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA), imefunga mwaka 2023 ikiwa imeandika rekodi mpya ya uendeshaji na utendaji wa kifedha ambayo ni tofauti na rekodi zake zilizotangulia.
Taarifa rasmi ya TPA kuhusu mwenendo wa uendeshaji na utendaji wa kifedha ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona, inaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, shughuli za mamlaka hiyo zimechukua sura mpya.
Ripoti hiyo inaonyesha ongezeko la makusanyo ya mapato, mizigo iliyohudumiwa, ziada ya mapato na meli zinazosubiri kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa ripoti, kushamiri kwa shughuli za bandari ambako kumekuwa na matokeo chanya, pia kumebeba changamoto zinazohitaji kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuimarisha zaidi shughuli za bandari, ambazo ni pamoja mifumo ya Tehama na vifaa vya kupakia na kupakua mizigo.
Tofauti kabisa na taarifa zisizo rasmi ambazo zimekuwa zikiibua mijadala mikali kwenye majukwaa mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kuhusu mwenendo wa uendeshaji na utendaji wa TPA, taarifa rasmi inaonyesha ongezeko la makusanyo kwa asilimia 27.3.
Ripoti inaonyesha kuwa, kwa mwaka wa fedha 2022/2023, TPA imevuna mapato ya Shilingi trilioni 1.394 kwa kuhudumia tani milioni 24,899. Hilo ni ongezeko la asilimia 19.8 ya shehena ya mizigo iliyohudumiwa na TPA kwa mwaka 2021/2022.
Ripoti hiyo ya kitaalamu inaonyesha kuwepo kwa ongezeko la ziada ya fedha baada ya matumizi kwa mwaka 2022/23 la Shilingi bilioni 551,474 ambazo ni sawa na asilimia 117.4 ya lengo lililowekwa la Shilingi bilioni 537.126.
Bandari ya Mtwara inatajwa katika ripoti hiyo kuvunja rekodi ya mafanikio yake ya awali kwa kuhudumia shehena yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.628, ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 174 huku Bandari ya Tanga ikitajwa kusuasua kiutendaji ambao umeshuka kwa asilimia 0.4, ikilinganishwa na mwaka wa fedha wa 2021/2022.
Kuhusu idadi ya kontena zilizohudumiwa, ripoti inaonyesha imeongezeka kutoka 832,200 kwa mwaka 2021/2022, hadi kontena 936,286 kwa mwaka 2022/2023, ambalo ni ongezeko la asilimia 13.7
Magari yakiwa Bandari ya Dar es Salaam baada ya kushushwa kwenye meli
Takwimu zilizo kwenye ripoti hiyo zinaonyesha kushuka kwa idadi ya magari yaliyohudumiwa na TPA kwa asilimia 7.9 huku mizigo kutoka nje ikitajwa kuchangia asilimia 75 ya jumla ya mapato yaliyokusanywa na mamlaka hiyo.
Bandari ya Dar es Salaam imeorodheshwa kuhudumia asilimia 87.2 ya mizigo yote iliyohudumiwa na bandari zinazosimamiwa na TPA huku Bandari ya Mtwara ikishika nafasi ya pili kwa kuhudumia asilimia 6.7 ya shehena ya mizigo iliyopokelewa nchini.
Chini ya hizo, ipo Bandari ya Tanga ambayo takwimu zinaonyesha ilihudumia asilimia 3.7 ya shehena ya mizigo, inafuatiwa na Bandari za Ziwa Tanganyika zilizohudumia asilimia 1.2 ya mizigo, Bandari za Ziwa Victoria, asilimia 1.1 na asilimia 0.025 ilihudumiwa katika bandari zilizo kwenye Ziwa Nyasa.
Kwa upande wa usafirishaji wa mizigo, ripoti hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inajibu maswali yanayoulizwa na wafuatiliaji wa masuala ya bandari; mizigo iliyosafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilikuwa tani 8,359,120, ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.1 ikilinganishwa na mwaka 2021/2022.
Katika hilo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatajwa kuwa nchi kinara ikichukua asilimia 42 ya mizigo yote iliyosafirishwa na bandari zinazosimamiwa na TPA. Inafuatiwa na Zambia ambayo ina asilimia 23, Rwanda asilimia 19, Malawi asilimia 7, Burundi asilimia 6, Uganda asilimia 2 na asilimia moja inagawanwa na nchi za Sudani Kusini, Zimbabwe na Msumbiji.
Meli kubwa ya mizigo ikielekea kutia nanga Bandari ya Dar es Salaam
Pamoja na mafanikio hayo, ripoti inaainisha changamoto ambazo msingi wake ni ufanisi wa uendeshaji na utendaji uliopo sasa katika mamlaka hiyo kuwa ni pamoja na mifumo ya TPA na Mamlaka ya Mapato (TRA) kushindwa kusomana, uchalewaji wa usafirishaji mizigo inayotoka bandarini kupitia njia ya barabara na reli na uchache na kuharibika kwa vifaa vya upakizi na upakuaji shehena.
Ripoti inataja pia ucheleweshaji unaofanywa na ICDV wa kupeleka magari bandari kavu kutokana na umbali uliopo kati ya Bandari ya Dar es Salaam na mahali ziliko ICD
MUHIMU
TAKWIMU ZILIZONAKIRIWA KWENYE HABARI HII NI TAKWIMU RASMI ZA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BANDARI TANZANIA (TPA). KWA MAELFU YA WASOMAJI WETU TANZANIA PANORAMA BLOG TUTAWALETEA MAKALA ZENYE UCHAMBUZI WA KINA WA UENDESHAJI NA UTENDAJI WA TPA NA BANDARI ZILIZO CHINI YAKE ILI KUKATA KIU YA MASWALI MAGUMU YANAYOULIZWA SASA. TUNAOMBA MUENDELEE KUTUAMINI KAMA CHOMBO CHENU CHA KUAMINIKA KINACHOWAFIKISHIA HABARI ZA UHAKIKA, ZILIZOFANYIWA UTAFITI WA KINA NA KAMA ILIVYO ADA YETU; ZISIZOKUWA NA CHUYA.