RIPOTA PANORAMA
SERIKALI inahujumiwa mapato ya mabilioni ya shilingi kwa takribani miaka minne sasa na moja ya kampuni kubwa (jina tunaihifadhi kwa muda) inayochimba madini ya dhahabu hapa nchini.
Mapato hayo ni ya hisa asilimia zisizopungua 16 ambazo serikali inapaswa kulipwa na kampuni zinazomiliki leseni za uchimbaji wa kati na mkubwa kama ilivyoainishwa kwenye sheria ya madini.
Sheria ya madini ya mwaka 2019 iliyotungwa na kupitishwa na Bunge kisha ikasainiwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli, kifungu cha 10, sura ya 123 inabainisha kuwa kampuni zinazomiliki leseni za uchimbaji wa kati na mkubwa wa madini hapa nchini kuilipa serikali hisa, asilimia zisizopungua 16.
Imeelezwa kuwa tangu kutungwa kwa sheria hiyo mwaka 2019, kampuni zote zenye leseni za uchimbaji wa kati na mkubwa zimekuwa zikitekeleza takwa hilo la kisheria isipokuwa kampuni hiyo ambayo imekuwa ikitumia mbinu chafu kuhujumu mapato hayo ya serikali.
Taarifa za uhakika kutoka vyanzo vya Tanzania PANORAMA Blog zimeeleza kuwa katika kutekeleza takwa hilo la kisheria, kampuni hiyo na nyingine zinazoguswa na sheria hiyo, ilipaswa kuketi kwa majadiliano na kufikia makubaliano na timu ya serikali inayoongozwa na Profesa Palamagamba Kabudi ya kulipa hisa hizo.
Hata hivyo, taarifa ambazo Tanzania PANORAMA Blog imezinasa zinaeleza kuwa tangu mwaka 2019 kampuni hiyo imekuwa ikitumia mbinu za ‘kimafia’ zinazotajwa kutumiwa na kampuni kubwa duniani zenye rekodi mbaya za unyonyaji rasilimali za mataifa masikini kutoilipa serikali hisa zake.
Mbinu kubwa iliyotajwa na watoa taarifa wetu inayotumiwa na kampuni hiyo kuhujumu mapato ya serikali ni kubadilisha wawakilishi wake kila mara katika timu ya majadiliano na serikali ili kuchelewesha makubaliano.
“Hawa ni wezi wa kimataifa. Wana mbinu nyingi kubwa kubwa na mara nyingi huwa wanawashika baadhi ya watendaji wenye mioyo ya tamaa ili kutekeleza uovu wao. Wamehujumu mapato ya serikali kwa mabilioni kwa zaidi ya miaka minne sasa lakini hakuna anayewagusa, wanazidi kuhujumu mpaka sasa.
Hayati Rais John Magufuli
“Kampuni zote zinazoguswa na hiyo sheria zinailipa serikali kasoro wao tu. Wewe fikiria tangu mwaka 2019 sheria ilipopitishwa, wao kila wakienda kwenye majadiliano na timu ya serikali wanapeleka ‘negotiator’ mpya, naye akifika haendelei na alipofikia mwenzake, anataka waanze upya.
“Na hii kampuni ina madudu mengi sana lakini yamefumbiwa macho, sisi tumo humo ndani kama kuna sehemu ya kupaza sauti watanzania wakajua kinachoendelea tuko tayari kukitumia kipaza sauti hicho kwa sababu timu ya majadiliano ina wasomi wakubwa lakini wanachezewa tu na hawa jamaa wanaendelea kuhujumu mabilioni ya serikali,” kilisema chanzo kimoja cha taarifa hii.
Taarifa zaidi zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zinaeleza kuwa kikao cha mwisho baina ya kampuni hiyo na timu ya majadiliano ya serikali kilichopangwa kufanyika Oktoba 31, 2023 Jijini Dodoma kiliahirishwa katika mazingira ya kukutanisha.
Inadaiwa kuwa muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho cha Oktoba 31, timu ya majadiliano ya serikali ilisambaratika na Tanzania PANORAMA Blog inafuatilia kwa karibu undani wa madai hayo.
SOMA TANZANIA PANORAMA BLOG KUJUA ZAIDI KUHUSU UNDANI SAKATA HIL